AFYA: Changamoto ilizopitia Hospitali ya Bondeni kuimarisha huduma
NA MAGDALENE WANJA
WIZARA ya Afya imekumbwa na changamoto tele kwa muda wa miaka sita sasa tangu ugatuzi ila hospitali ya Bondeni, Kaunti ya Nakuru ambayo ni mojawapo ya hospitali za zamani itakumbukwa kwa mchango wake katika maendeleo.
Hospitali hiyo ambayo iko katika kiwango cha Level Four ilianzishwa mnamo mwaka 1952 kama kituo cha kujifungua kwa wanawake ambao waliishi kusini mwa reli ya Rift Valley.
Tangu kuanzishwa kwake, hospitali hiyo inajivunia kuwasaidi wanawake kujifungua watoto ambao sasa ni watu maarufu nchini wakiwemo madaktari, wahandisi, mawakili na viongozi mbalimbali wa kisiasa.
Ata hivyo, waliozaliwa katika hospitali hiyo katika miaka ya 1970 watashangaa kupata mabadiliko ambayo yamefanyika katika hospitali hiyo ambayo kwa zaidi ya miongo mitatu ilihusishwa na walalahoi.
Hii ni kwa sababu hospitali hiyo ilijengwa katikati mwa mtaa duni wa Bondeni ambao ni mojawapo ya mitaa ya kale zaidi mjini Nakuru.
Hospitali hiyo sasa ina vifaa vya kisasa vya kuwawezesha akina mama kujifungua , jambo ambalo limewavutia wakazi wengi.
Mabadiliko hayo yalianza kufanyika mnamo mwaka 2015 kwani hospitali hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Municipal Council hadi mwaka 2014.
Kulingana na afisa msimamizi wa hospitali hiyo Daktari Salome Gachathi, imegharimu Sh 15 milioni kuirekebisha hospitali hiyo.
Marekebisho hayo ni pamoja na ujenzi wa wadi mpya unaonuiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2019.
Baadhi ya vitengo vipya ambavyo vimeanzishwa ni pamoja na duka la dawa, kile cha usafishaji, kitengo cha ununuzi na kile cha mapishi.
“Hapo hawali, tuliitegemea hospitali kuu ya Nakuru Level 5 kwa huduma nyingi kama vile chakula cha wagonjwa lakini kwa sasa tunatayarisha chakula hapa hospitalini,’ alisema Dkt Gachathi.
Hata hivyo, kulingana na Dkt Gachathi, safari ya kufanya mabadiliko katika kituo hicho cha afya haijakuwa rahisi.
“Hatua ya kwanza ilikuwa ni kubadilisha mtazamo wa wafanyikazi kwani baadhi yao walikuwa wamekwama katika tamaduni za kale za kuwahudumia wagonjwa,” akasema Dkt Gachathi.
Hospitali hiyo kwa sasa inarekodi kuzaliwa kwa watoto kati ya 170 na 200 kwa mwezi.
“Itakapokamilika, tunatarajia kuongeza idadi ya wanaojifungua katika hospitali hii kufikia 600 kwa mwezi,” akasema.
Alisema kuwa wakati wa mgomo wa madaktari ulioshuhudiwa mwaka jan, hospitali hiyo iliweza kurekodi kuzaliwa kwa watoto 600 kwa mwezi mmoja.
“Hii imesalia kuwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa ambao tumeweza kuhudumi kwa mwezi mmoja,” akasema.
Mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo Bw Boniface Mouti alisema kuwa itakapokamilika, hospitali hiyo itakuwa baadhi ya vituo vya afya vya kisasa.
“Hawali, hospitali hii iliwahudumia wakazi wenye mapato ya chini lakini katika hali yake ya kisasa , tutaweza kuwahudumia wakazi wa ngazi mbalimbali katika jamii,” akasema Bw Mouti.
Bi Prisca Maina ambaye alihudumu kama muuguzi msimamizi wa hospitali hiyo chini ya usimamizi wa Municipal Council alisema kuwa ugatuzi umechangia ktika mabadiliko katika sekta ya afya.
Aliongeza kuwa, kinyume hapo hapo hawali, hospitali hiyo sasa inaweza kujitegemea kifedha.
Mnamo mwezi Septemba, hospitali hiyo ilifungua wadi mpya yenye vitanda tisa vya kuwadumia wajawazito walio katika hatua za mwisho.