Makala

AFYA: Jinsi unavyoweza kukabiliana na mafua

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MAFUA husumbua watu wengi hasa wakati wa baridi au vumbi. Ili kujikinga na mafua, ni lazima mwili uwe na kinga ya kutosha.

Supu ya kuku

Unywaji wa supu ya kuku hasa wa kienyeji humpa mlaji virutubisho vinavyosaidia kupunguza kadhia ya mafua. Utapata virutubisho vingi zaidi ukitengeneza supu ya kuku kwa kuchanganya na mboga za majani.

Vitunguu saumu

Vitunguu saumu vina kirutubisho aina ya ‘allicin’ ambacho kina uwezo wa kutoa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ya kuambukiza.

Kitunguu saumu kinatoa kinga na kupunguza muda wa mtu kuwa na mafua. Mtu anaweza kutumia kitunguu hicho kwa kupika kwenye chakula au kwa kutafuna punje zake.

Chai

Chai, hasa ya kijani (green tea) ina virutubisho vya kuimarisha kinga ya mwili. Watu wanaotumia chai hii hawasumbuliwi mara kwa mara na mafua pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Machungwa

Ulaji wa vyakula vyenye Vitamini C kwa wingi kila siku husaidia kuondoa au kuzuia mafua. Miongoni mwa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha Vitamini C ni pamoja na machungwa, mboga za majani aina ya brokoli.

Asali

Asali ni tiba ya matatizo mengi ya kiafya, miongoni mwa hayo ni pamoja na mafua. Asali inasaida kuondoa kikohozi na muwasho kwenye koo.

Ili kuimarisha kinga ya mwili ,ulaji wa vyakula vilivyotajwa hapo juu na vingine, unatakiwa kuwa ni wa mara kwa kwa sababu mwili unapokosa kinga imara, ni rahisi kushambuliwa na maradhi ya kuambukiza.