• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
AFYA: Madhara ya kuchora tattoo mwilini

AFYA: Madhara ya kuchora tattoo mwilini

Na MARGARET MAINA

[email protected]

TATTOO huhusisha uwekaji wa wino kwenye ngozi ya ndani (dermis).

Kwa dunia ya sasa, kujichora tattoo ni kama fasheni fulani kwenye jamii, ukienda kuchora tattoo kuna uwezekano mkubwa sana isitoke maisha yako yote na hivyo kwa usalama wako ni vizuri ukamuona mtaalamu wa tattoo.

Kabla hujaamua kujichora tattoo basi ni vyema ukajua madhara yake.

Saratani ya ngozi

Hapo mwanzoni wataalamu walikuwa wanasema hakuna uhusiano kati ya kansa ya ngozi na kujichora tattoo, lakini hivi karibuni tafiti zinaonyesha kuna aina fulani za wino ambazo zinaweza kusababisha saratani zikitumika kuchora tattoo.

Allergy ya ngozi

Watu wengi hupata allergy baada ya kuwekwa tattoo. Utafiti unaonyesha rangi nyekundu ndiyo inaongoza kwa kusababisha allergy. mara nyingi allergy hizi huonekana mtu akikaa juani.

Makovu

Mwili unataambua tattoo kama adui wake hivyo hujaribu kuiondoa kwa njia mbalimbali na kwa kufanya hivyo, husababisha makovu ya muda mrefu ambayo yanaweza kuleta magonjwa mengine ya ngozi.

Maambukizi ya ukimwi na ugonjwa wa hepatitis

Tabia ya kurudia sindano zilezile wakati wa kuchora tattoo kunaweza kusababisha maambukizi ya virusi vya Ukimwi na maambukizi ya virusi vinavyoshambulia ini kitaalamu kama Hepatitis B. Ugonjwa huu wa Hepatitis B husababisha saratani ya ini ambayo haitibiki. Ni vizuri kuwa makini ili uone kama sindano inayotumika kwako ni mpya.

Matatizo kipindi cha kufanya kipimo cha MRI

Hiki kipimo cha MRI hutumika kupima viungo vya mwili ambavyo havionekani kwa macho ndani ya mwili wa binadamu kama eksirei inavyofanya. Tatizo ni kwamba kipimo hiki kina sumaku kali kiasi kwamba mtu hatakiwi kuingia kwenye mtambo huo akiwa amevaa chuma chochote na hata kama kiko ndani ya mwili kitavutwa nje. Sasa iko hivi; mara nyingi tattoo nyeusi huwa imetengenezwa na iron oxide ambayo ina chembechembe za chuma. Hii inaweza ikaleta changamoto kubwa kwenye vipimo.

Kubadilika kwa ngozi ya rangi

Sehemu inayochorwa tattoo hubadilika moja kwa moja na kuwa na rangi tofauti. Hakuna jinsi unavyoweza ukaitoa hiyo rangi tena, hata baada ya muda mrefu tattoo ikipungua nguvu lakini ngozi haiwezi kuwa kama zamani.

Hutaruhusiwa kuchangia damu

Mara nyingi watu wenye tattoo hawaruhusiwi kuchangia damu kwani wana hatari ya kusambaza ugonjwa kwenda kwa mtu mwingine.

Kimsingi, mtu aliyechora tattoo ya muda mfupi huenda akaruhusiwa lakini kwa sababu wakati mwingine sio rahisi kutofautisha tattoo mpya na ya zamani basi hawa watu huwa hawaruhusiwi kabisa.

Unaweza kukosa fursa mbalimbali

Kuna kampuni mbalimbali duniani haziwapi watu kazi kwa sababu wamechora tattoo kulingana na kanuni na itikadi za kampuni lakini pia kazi yoyote ya jeshi duniani hairuhusu tattoo.

Magonjwa ya ngozi

Wakati mwingine bakteria huvamia sehemu zenye vidonda vya tattoo na kusababisha kutopona haraka. Dalili huweza kuwa homa kali, maumivu na sehemu ya tattoo kuvimba.

Damu kuganda juu ya ngozi [haematoma]

Hali hii husababishwa na kuvuja kwa damu nyingi chini ya ngozi. Huonekana sana sehemu ambapo rangi ya tatoo imepita na huchelewesha kupona kwa kidonda.

You can share this post!

ULIMBWENDE: Jinsi ya kuvaa viatu mbalimbali

Paipu za maji safi zinazopitia kwenye mitaro ya majitaka...

adminleo