Afueni kwa wanaume wenye upara watafiti wakigundua mafuta ya kuutokomeza
TATIZ0 la upara miongoni mwa wanaume huenda likatokomea baada ya wanasayansi kugundua mafuta mapya ambayo yakipakwa yanasaidia nywele kumea kichwani.
Wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield, Uingereza na wenzao kutoka Chuo Kikuu cha COMSATS nchini Pakistan, walishiriki utafiti ambao uligundua mafuta hayo.
Kwa mujibu wa utafiti huo, mafuta yenye sukari (deoxyribose sugar) yana kemikali ya kaboni ambayo inasaidia kutokomeza upara huo. Wanasayansi waligundua hilo kibahati baada ya kuyapaka mafuta hayo kwenye sehemu ya mwili wa panya aliyekuwa amejeruhiwa na kupoteza nywele na wakapata zimemea sehemu hiyo.
Baada ya kushaajishwa na kile walichogundua, walimchukua panya mwengine ambaye hakuwa na nywele katika sehemu ya uume wake. Kwa bahati nzuri nywele zilimea sehemu hizo huku mishipa mipya ya damu pia ikichipuka na kusaidia katika kumea kwa nywele hizo.
“Utafiti wetu unaonyesha kuwa tiba ya upara ni kutumia mafuta hayo ya deoxyribose sugar. Yanaongeza kusambazwa kwa damu kwa jeni zinazosababisha nywele kumea,” akasema Profesa Sheila McNeil kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield.
Watafiti hao pia waligundua kuwa mafuta hayo yanasaidia nywele kumea kama tu dawa maarufu ya Minoxidil ambayo imekuwa ikitumika kutokomeza upara.
Hata hivyo, Minoxidil japo imebainika kupunguza uwezekano wa mtu kupoteza nywele zake, huwa haifanyi kazi kwa baadhi ya wanaume amba wana upara.
Dawa ya Finasteride ambayo imeidhinishwa kutumika na wanaume pekee kwa tatizo la upara, nayo imebainika hufanya kazi kwa kati ya asilimia 80-90.
Hata hivyo, wale walioitumia wamelalamikia athari mbalimbali za kiafya huku wengine wenye upara wakikumbatia upasuaji ili kuwasaidia kupata nywele.
Wanasayansi wamebaini kuwa zaidi ya nusu ya wanaume ulimwenguni huwa na upara wakifikisha miaka 50 na zaidi.
Kwa wanawake robo ya idadi yao ulimwenguni pia huanza kuwa na upara wakifikisha miaka 50 au zaidi.