Jinsi akili unde, ‘AI’, inavyosaidia kuimarisha afya ya uzazi nchini Kenya
AKIWA na mimba ya wiki sita, Bi Cate, mkazi wa eneo la Watathie, Kaunti ya Kiambu, aligundua matone ya damu yakitoka ukeni, suala lililomsababishia yeye pamoja na mumewe hofu.
Hii ni kwa sababu tayari wawili hawa walikuwa wamesubiri kupata mtoto kwa miaka sita baada ya mimba mbili kuharibika, na matone haya yaliashiria hatari kwa ujauzito wake.
Lakini tofauti na awali wakati huu mumewe Bi Cate, alichukua simu na kutuma ujumbe mfupi kwa apu ya PROMPTS iliyosema “kuna damu nyingi, tufanyeje?”
“Kuvuja damu katika kipindi cha kwanza cha ujauzito sawa na ilivyoshuhudiwa kwa Bi Cate, kwa kawaida huashiria kwamba mimba imeharibika au kuna matatizo mengine, ambapo huduma ya haraka huwa muhimu,” aeleza Dkt Odero Ongéch, mwanajinakolojia na mtaalam wa matibabu ya uzazi.
PROMPTS ni teknolojia ya akili unde yaani AI inayotumika kutoa huduma ya afya kwa akina mama wajawazito kupitia arafa ya SMS. Jukwaa hili linatumia teknolojia ya AI, pamoja na usaidizi wa wahudumu wa afya, kuwapa akina mama wajawazito uwezo wa kujishughulikia na kufikia huduma za afya kwa wakati ufaao.
Katika muda mfupi, mumewe Bi Cate alikuwa ameunganishwa na mhudumu wa afya kwenye dawati la kutoa ushauri wa kimatibabu, ambaye alikagua hali ilivyokuwa na kuwashauri waende hospitalini mara moja.
Kwa kawaida apu hii hutuma jumbe za SMS kuambatana na awamu ya ujauzito wa mama, na hivyo kusaidia kutoa ushauri kwa wakati unaofaa, kumkumbusha mama, na kutoa onyo kuhusu mambo ambayo anayopaswa kuzingatia wakati huu.
Apu hii hufanya kazi kwa kutuma msururu wa jumbe ambazo zimeundwa hususan kwa minajili ya mhusika kuambatana na hali yake na awamu yake ya ujauzito, kuhakikisha kwamba wanapata habari zinazowafaa tena kwa wakati unoafaa.
Kwa hivyo, pindi mumewe Bi Cate alipotuma ujumbe huo mfupi, teknolojia hiyo ya AI ilitumia mfumo unaofahamika kama Natural Language Processing (NLP) kuelewa ujumbe kuhusu kuvuja damu, ambayo ni ishara ya kawaida ya mimba kuharibika au matatizo mengine. Kisha ikatoa tahadhari kwa ajenti aliyekuwa kwenye dawati la kutoa ushauri hospitalini, ambaye alijibu upesi na kumshauri Bi Cate kwenda hospitalini kupokea matibabu mara moja.
Kupitia jukwaa hili ujumbe kutoka kwa mumewe Bi Cate ulitambuliwa kuwa dharura.
“Tulienda hospitalini mara moja na kushughulikiwa ambapo tuliweza kupata nafuu.”
Kwa bahati mbaya, Bi Cate alipoteza mimba yake, lakini matokeo ya hali hii yangekuwa mabaya hata zaidi.
“Daktari aliniambia kwamba iwapo singefika hospitalini kwa wakati nilioshauriwa, hata maisha yangu yangekuwa hatarini,” aeleza.
Kupitia huduma hii, akina mama wanapata fursa ya maswali yao kujibiwa huku visa vya dharura vikitambuliwa mara moja, na hivyo kuhakikisha kwamba mama anaelekezwa kwenda hospitalini mara moja.
Aidha, kwa sababu apu hii inafanya kazi kupitia jukwaa la ujumbe wa SMS, inaweza kutumika kwa simu ya aina yoyote, kumaanisha kwamba huduma hii inaweza kufikiwa kwa urahisi hata miongoni mwa akina mama wa mashambani ambao huenda hawawezi mudu simu za kisasa.
Kenya ni mojawapo ya mataifa yanayokumbwa na visa vingi vya vifo vya akina mama na/au watoto wakati wa ujauzito duniani. Kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO, Kenya hunakili vifo 342 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai.
Utafiti wa hivi majuzi uliofanywa na serikali ulionyesha kwamba mara nyingi vifo vinavyotokea wakati wa ujauzito nchini husababishwa na mama kuchelewa kupokea matibabu kwa wakati unaofaa.
“Wanawake wengi hasa wajawazito hukawia au kutopata matibabu bora kwa wakati unaofaa,”aeleza Dkt Ong’ech.
“Vichocheo vya kukawia huku huwa tofauti – akina mama katika sehemu za mamshambani hukabiliwa na changamoto ya kusafiri kwa mwendo mrefu kwenda hospitalini, huku wengine huenda wasitambue dalili za hatari au wanahisi kana kwamba hawana ufahamu wa kujua jambo la kufanya matatizo yanapotokea,” aaongeza.
Aidha, kulingana na mtaalam huyu, kizingiti kingine ni kufikia huduma ya afya kwa akina mama katika sehemu za mashambani ni kufikia taarifa muhimu.
“Mara nyingi akina mama hawajui dalili zinazohitaji huduma ya dharura, au kupitia taratibu complex wakati wa kutafuta huduma ya afya hospitalini.”
Ndiposa suala la kutoa huduma ya afya kwa njia ya kidijitali limechukuliwa kwa umakini hasa na baadhi ya kaunti humu nchini. Katika kongamano la kwanza huduma ya kiafya kupitia majukwaa ya dijitali mwezi uliopita jijini Kisumu, wataalam wa kiafya walisema kwamba kuna haja ya kuhusisha matumizi ya kidijitali ili kufikia huduma ya afya kwa wote.
“Wengi wetu tumekumbana na foleni ndefu katika vituo vya afya ambapo kuna baadhi ya watu wanaofika hospitalini hata saa tisa alfajiri ili wapokee huduma haraka,”alisema Dkt Joyce Wamicwe, Kaimu mkuu wa huduma ya afya ya kidijitali katika Wizara ya Afya.
Dkt Radha Karnad, mtaalam wa masuala ya matibabu kupitia njia ya kidijitali asema kwamba mifumo hii ya inawezesha wagonjwa kufikia huduma za afya bora haraka na bei nafuu.
“Aidha, inawapa wagonjwa uwezo wa kufuatilia rekodi zao za afya, na pia kuwawezesha kufikia huduma za afya mapema.”
Lakini kuna changamoto.
“Sekta hii inakumbwa na changamoto kama vile kutokuwepo kwa udhibiti hasa ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya vituo ambavyo havijaidhinishwa kutoa huduma hii, ilhali vinaendelea na shughuli,”aeleza Bw Wycliffe Waweru, Mkuu wa huduma za afya za kidijitali na ukaguzi, katika shirika la Population Services International.
Pia, kulingana na mtaalam huyu, majukwaa ya kutoa huduma za afya kupitia mifumo hii, hayana mpangilio, na hivyo kufanya wagonjwa wakose imani na huduma hizi.
“Teknolojia aidha inaimarika kwa kasi ikilinganishwa na udhibiti, kumaanisha kwamba kuna haja ya serikali kuhakikisha kwamba sera za udhibiti zipo.”
Lakini licha ya changamoto hizi, wataalam wanahoji kwamba mtazamo wa siku zijazo wa huduma za afya hasa barani utategemea sana na mifumo ya kidijitali ya kutoa huduma ya afya.
Kulingana na Dkt Jeremiah Mumo, mtaalam wa habari za kiafya katika Wizara ya Afya, itakuwa ngumu kwa nchi zinazostawi kama Kenya kutimiza ndoto ya afya kwa wote, ikiwa mifumo ya kidijitali haitachukuliwa kwa umakini.
“Hii ni hasa ikizingatiwa kwamba rasilimali za kujenga hospitali na vituo vya afya vya kutosha bado ni donda sugu hapa barani ili kukabiliana na idadi kubwa ya watu inayozidi kuogezeka. Aidha, tunakumbwa na uhaba wa wahudumu wa afya,” aeleza.