Mwaka mpya, mwanzo mpya: Jinsi utarekebisha ulivyokula na kunywa likizoni
LIKIZO hii ya kusherehekea Sikukuu na Mwaka Mpya, watu wengi duniani walitangamana na ndugu, jamaa na marafiki.
Vyakula na vinywaji kwa wingi vilikuwepo huku kila mtu akila na kunywa alichotaka. Hata hivyo, baadhi ya watu walikula na kunywa zaidi ya kawaida.
Kwa vyovyote vile, ujio wa mwaka mpya huwafanya wengi kurekebisha wanavyokula na kunywa.
MaryAnne Wanza, mtalaamu wa afya anasema kuwa cha muhimu wakati huo ni kuwacha kula na kunywa kwa ghafla.
“Usijifunge kula chakula ili uzoeshe mwili kurejea ulipokuwa hapo awali au kufidia kiwango cha mlo uliokula kupita kiasi wakati wa sherehe,” anasema.
Unapaswa kujipa changamoto ya kurekebisha ulivyokula na kunywa kwa kuangazia chakula unachokula na maji unayokunywa, saa unazopumzika na mazoezi unayofanya.
Iwapo bado ninatamani kula vyakula vyenye sukari?
Bi Wanza anashauri hatua ya kuanzia inapaswa kuwa jambo ambalo ni rahisi kiasi cha kukufanya uanze kweli, lakini pia ngumu kiasi cha kukufanya uhisi kuwa inakupa changamoto.
Kwa sababu pande zote mbili zinaweza kukukatisha tamaa; ikiwa ni ngumu sana, ikiwa ni rahisi sana, hautaanza.
“Kwa mfano, ikiwa umekuwa ukila keki au biskuti badala ya chakula, unahakikisha kuwa unakula kiamshakinywa, chamcha na chajio. Iwapo umekuwa ukibugia soda, pombe au juisi badala ya maji, unajipa changamoto ya kunywa angalau lita moja kisha uongezee na robo kila siku,” anaongezea.
Ukipata tamaa ya kula vyakula vyenye sukari (sweet cravings), tafuta tunda au wanga wa hudhurungi badala ya mweupe (unga, mchele wa hudhurungi). Kula vyakula vyenye faiba sababu utahisi umeshiba kwa muda mrefu. Ongezea protini kama mayai, maharagwe, ndengu, nyama na kadhalika.
“Pia, kula vyakula vyenye mafuta kama parachichi, mbegu ya ufuta (sesame seed), alizeti. Tafuta pia mboga kwa sababu zinakupa vitamini mwilini.”
Hata hivyo, iwapo bado unataka kula vyakula hivi vyenye sukari, Bi Wanza anashauri kuboresha afya yako kwa kula chakula chenye afya.
“Kwa mfano, unaweza kula biskuti na glasi ya maziwa. Hii ni tofauti sana na kula biskuti tatu peke yake kwa sababu glasi ya maziwa ni protini nzuri yenye madini ya kalsiamu. Pia, maziwa yatakusaidia kupunguza hamu ya sukari.”
Isitoshe, Bi Wanza anasema badala ya kula vijiko vitatu vya aiskrimu, weka kimoja na uongezee strawberi, ndizi au njugu.
Unapokula kiamshakinywa chako, jaribu kuhakikisha kuwa una wanga, protini na mboga. Kwa mfano badala ya kula slesi nne za mkate, kula mbili na yai pamoja na kachumbari.
Mazoezi na saa za kulala je?
Japo ni muhimu kujishukuru unapopiga hatua, Bi Wanza anasema usijishukuru kwa njia isiyokusaidia kuendelea.
Kwa mfano, ikiwa umekuwa ukifanya mazoezi kwa wiki kadhaa, usijishukuru kwa kula piza bali kwa kununua kiatu kipya, kukandwa mwili au hata kutafuta kocha.
Pili, sio lazima uanzie mabadiliko ya afya yako mwaka mpya. Bi Wanza anashauri kuanzia wakati wowote ule kutakusaidia iwapo tu utaamua kufuatilia sio tu kungojea mwezi mpya, mwaka mpya au Jumatatu.
Iwapo unataka kupunguza uzito wako au kubadilisha mwonekano wa mwili wako, Bi Wanza anasema kuhakikisha kuwa unafanya mazoezi kila siku kutakusaidia.
Kwa mfano, badala ya kupanda lifti, tumia ngazi (stairs). Pia, kila baada ya saa mbili, simama kutoka kiti chako na utembee kwa angalau dakika tano.
Sababu likizo huwafanya watu wengi kutolala kwa saa zinazostahili, Bi Wanza anasema kuhakikisha kuwa angalau umelala saa mbili baada ya kula kutakusaidia kulala mpaka jua linapochomoza bila kuamka kutafuta chakula.
Miezi miwili kupunguza uzito ulioongezea wakati huu wa likizo
Watafiti kutoka Chuo cha Mafundisho cha Imperial, Uingereza wanasema kuwa iwapo uliongezea uzito wakati huu wa likizo, utahitaji angalau miezi miwili kuwa na uzito wa hapo awali.
Wanasayansi hao wanasema kuwa ili kufikia uzito wa hapo awali, utahitaji kufanya mazoezi kwa saa mbili na nusu kila wiki; angalau zaidi ya dakika 30 kwa siku tano.
Kula vizuri huchangia angalau asilimia 80 ya uzito wa mtu huku asilimia 20 iliyosalia ikiwa ya mazoezi.
Watu wenye umri wa miaka 19 hadi 64 wanahimizwa kufanya angalau saa mbili na nusu za mazoezi ya wastani, au dakika 75 za mazoezi yenye kutumia nguvu nyingi, kila wiki.
Kufanya mazoezi haya kutasaidia kubaki na afya bora pamoja na kupunguza hatari ya magonjwa kama mshutuko wa moyo na kiharusi.
Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni unapendekeza kiwango hicho cha mazoezi ya aerobiki kwa watu wenye BMI zaidi ya 25.