Vidutu kwenye sehemu za siri vinavyowahangaisha wanaume
TAKRIBANI asilimia moja ya wanaume waliopo kwenye mahusiano ya kingono huathiriwa na vipele kwenye sehemu zao za siri baada ya kuathiriwa na ugonjwa unaofahamika kama genital warts.
Vipele hivi visivyo na maumivu huenea kwa kasi hasa kwa wanaume vijana wanaoshiriki ngono. Isitoshe, sababu ya unyanyapaa wa ugonjwa huu, wanaume wengi huwa na wasiwasi mwingi wanapotambuliwa kuugua vipele hivi.
Dkt Muigai Mararo, mtaalamu wa afya ya njia ya mkojo, anaeleza jarida hili kuwa wanaume walio na umri wa miaka 18 hadi 28 ndio wanaokumbwa zaidi na ugonjwa huu almaarufu genital warts.
Maishani, mwanamume yupo kwenye hatari ya kuugua vipele hivi kwa asilimia 10.
Ugonjwa huenea vipi?
Vipele hivi kwa sehemu za siri ni uvimbe unaoota wenye rangi ya kijivuhusababishwa na aina fulani ya virusi vya Human Papillomavirus (HPV) kwa njia ya ngono, kugusana ngozi au kutoka mama hadi kwa mtoto wakati wa kujifungua.
Dkt Muigai anasema kuwa japo kuna zaidi ya aina 200 za HPV zilizotambuliwa, aina ya HPV 6 na 11 ndizo zinazojulikana kusababisha vipele hivyo kwenye sehemu za siri.
“Ingawa HPV aina ya 6 na 11 hazihusiani sana na saratani, mtu anaweza kuwa na maambukizi ya aina za HPV yenye hatari kubwa inayoweza kusababisha saratani ya njia ya uzazi, sehemu za siri, au hata kansa ya kichwa na shingo,” anasema.
Anaeleza kuwa vipele hivi huwa havisababishi saratani na ni nadra sana mgonjwa kuugua kansa ila tu kwa wagonjwa wenye kingamwili dhaifu.
Lakini vipele hivi huchukua muda gani kabla kuonekana?
“Kati ya wiki tatu hadi miezi minane. Lakini kuibuka kwa vipele hivi kwa upesi hutegemea nguvu ya kingamwili ya mtu. Watu wengi hawawezi wakapata vipele hivyo hata kama wameambukizwa HPV.”
Tabibu huyu anaeleza kuwa utatambua iwapo mtu anaugua vipele hivyo iwapo sehemu yake ya siri inaonekana kuwa na uvimbe wa kijivu au kupima sehemu ya ngozi yake.
“Iwapo unashiriki ngono bila kinga, una wapenzi wengi, au kingamwili yako ni dhaifu (kama watu wanaoishi na virusi vya HIV, wanaotumia dawa za kusisimua misuli – steroids), basi upo kwenye hatari ya kupata vipele hivi kwenye sehemu yako ya siri,” anaeleza.
Isitoshe, watu wenye historia ya kuugua magonjwa ya zinaa kama kisonono na chlamydia, wanaume ambao hawajatahiriwa na wanaougua ugonjwa wa kisukari (diabetes mellitus) pamoja na wale wanaovuta sigara wapo kwenye hatari iyo hiyo.
Mgonjwa wa vipele kwenye sehemu za siri hupokea matibabu kwa kutumia dawa za kupaka au akafanyiwa upasuaji ili kuondoa vipele hivyo.
Dkt Muigai anasema kuwa njia ya kumtibu mgonjwa huyo hutegemea, ukubwa wa vipele, maamuzi ya mgonjwa, gharama na madhara anayoweza pata anapopokea matibabu.
“Hata hivyo ni muhimu ugonjwa huu utambuliwe mapema na matibabu sahihi yafanyike kwa sababu dawa zingine za kupaka zinaweza kuwa zikitibu tatizo tofauti huku kufanya HPV kudumu kwa muda mrefu zaidi,” anasema Dkt Muigai.
Vipele kurudi baada ya matibabu
Hakuna muda maalum wa aliyeathiriwa na vipele hivi hupona kwani matibabu hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Pia, matibabu haya hutegemea matibabu anayopokea mgonjwa.
Hali kadhalika, Dkt Muigai anasema kuwa chanjo ya HPV inapaswa kupewa pia wanaume kabla hawajaanza kushiriki ngono, lakini bado inaweza kuwa na manufaa kwa wanaume wanaoshiriki ngono ili kuwalinda dhidi ya maambukizi mapya ya HPV.
“Utaweza kujizuia dhidi ya kuugua vipele hivi iwapo utapokea chanjo ya HPV, utatumia kondomu, na utakuwa na mpenzi mmoja mwaminifu wa kushiriki ngono naye,” Dkt Muigai anashauri.
Japo mgonjwa anaweza tibiwa vipele hivyo, anaweza endelea kueneza virusi vya HPV kwa kuwa virusi hivyo huenezwa kwa njia ya ngono.
Isitoshe, Dkt Muigai anasema kuwa vipele hivyo pia vinaweza vikarudi hata baada ya matibabu kwa sababu ya kuwepo kwa HPV au kingamwili duni mwilini. Ndio maana mgonjwa huyo anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara.