Wagonjwa walilia Ruto asiwapeleke kaburini mapema kupitia changamoto za SHIF
WAGONJWA ambao wana maradhi yasiyotibika na wanahitaji huduma za mara kwa mara za matibabu, wameililia serikali iwaruhusu watumie Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) badala ya Hazina ya Afya ya Jamii (SHIF).
Wakiongea kwenye mahojiano na Taifa Leo, wagonjwa hao walilalamika kuwa mchakato wa kupata matibabu chini ya bima mpya ya SHIF ni mgumu na unawatuma kaburini mapema.
Katika hospitali ya Kenyatta na ile ya Rufaa na Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTTRH), walisema hawawezi kupokea matibabu kutokana na changamoto mbalimbali zinazokumba matumizi ya SHIF.
“Chini ya NHIF ugonjwa wa figo ambao unaniathiri ulikuwa rahisi sana kushughulikiwa hospitalini. NHIF walikuwa wakitoa Sh8,500 nikisafishiwa damu na hiyo ilikuwa ikifanyika mara mbili kwa wiki.
“Kwa sasa, nimelazimika kulipa Sh11,000 kila wiki ili niwe hai,” akasema Salome Kamau, mgonjwa ambaye amelazwa KUTTRH.
“Ukweli ni kuwa SHIF haina manufaa yoyote,” akaongeza huku akisema mtandao wa SHIF pia umekuwa na kila aina ya changamoto. Amekuwa akiugua ugonjwa wa figo tangu 2020 na amepokea huduma za kimatibabu kutoka hospitali mbalimbali, gharama yote ikilipwa na NHIF.
Dkt Onyimba Kerama alisema kuwa Bi Kamau lazima alipe pesa ili kufanyiwa vipimo mbalimbali kabla afanyiwe upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye figo yake.
“Lazima alipe kwa sababu kile ambacho SHIF hulipia katika mpango wake wa matibabu ya wanaogua figo hakitoshi,” akasema Dkt Kerama.
Bi Kamau aliongeza kuwa kabla ya Oktoba 1 ambapo NHIF ilikuwa ikitumika, gharama zake zote za matibabu zililipwa na bima hiyo ambapo amewahi kulipiwa Sh55,000, Sh80,000 na Sh40,000.
Nje ya KUTTRH, Stephen Karanja anayeugua kansa alikuwa hana raha na alikuwa amekasirika na kusonya sana.
“Nimekuwa hapa tangu saa 12 asubuhi lakini SHIF haifanyi kazi na wameshinda wakituambia bado haijarekebishwa. Sijui nini nilimkosea Rais William Ruto kiasi kuwa sasa anataka niondoke ulimwengu huu,” akasema Bw Karanja akionekana mnyonge.
“Katika hali hii nitakufa nikisubiri kwa sababu siwezi kuhudumiwa na daktari bila kufanyiwa vipimo hivi ninavyosubiri na matokeo yake kujulikana,” akaongeza Bw Karanja.
Katika Hospitali ya Kenyatta, hali haikuwa tofauti huku wagonjwa wengi wakilazimika kujilaza kwenye eneo la mapokezi na pa kusubiria baada ya SHIF kukosa kufanya kazi.
“Tumeambiwa mashine mbili za kusafisha damu hazifanyi kazi tulipouliza kwa nini hatukuwa tukihudumiwa kwa wakati. Pia wamesema SHA haifanyi kazi ndiposa nikaandamana na rafiki yangu hapa,” akasema mgonjwa Anthony Chege.
“Maisha enzi za NHIF yalikuwa mazuri. Nashangaa kwa nini walituondoa kwenye NHIF na kutuweka kwenye SHIF ambayo inatua na uchungu,” akaongeza Bw Chege.
Haya ndiyo masaibu ambayo wagonjwa wamekuwa wakiyapitia serikali nayo ikisisitiza kuwa SHA ni bora kuliko NHIF na itahakikisha Wakenya wote wamepokea matibabu kwa usawa.
Imetafsiriwa na Cecil Odongo