Afya na Jamii

Watafiti wafuta dhana kuwa mbegu za kiume zimepungua kwa wanaume

Na NA CECIL ODONGO June 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

DHANA kuwa mbegu za kiume zinaendelea kupungua miongoni mwa wanaume ulimwenguni huenda si kweli.

Hii ni kulingana na utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Cryos nchini Denmark, Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza na Chuo Kikuu cha Queens, jijini Kingston Canada.

Denmark ndiyo nchi ambayo inaongoza kwa idadi ya wanaume ambao hutoa mbegu zao kwa hiari duniani.

Tafiti mbalimbali, ambazo pia zinachambua takwimu za zamani na zilichapishwa katika vyombo vya habari, zilionyesha kuwa kuna upungufu sana wa mbegu za kiume ikilinganishwa na miaka ya zamani.

Hata hivyo, utafiti wa sasa uliowashirikisha wanaume 6,758 umekanusha hali hiyo.

Utafiti wa sasa ambao ulichapishwa kwenye jarida moja la kimataifa kuhusu uzazi na afya wiki jana, umebaini kuwa mbegu za kiume hazijapungua kwa wanaume.

Utafiti ambao ulifanywa kuhusu kiwango cha mbegu za kiume ambazo zimekuwa zikitolewa kwa miaka sita, pia unaonyesha hakuna upungufu.

Japo shirika la Cryos lilianzishwa miaka 40 iliyopita, watafiti walitumia data walizokusanya kati ya 2017-2022 na kuhakikisha kuna namna inayoweza kuaminika katika kutathmini kiwango cha mbegu za kiume kwa kila mwanaume aliyeshirikishwa kila mwaka.

“Utafiti uliochapishwa na Levine et al (2023) ulisema kuwa mbegu za kiume zimekuwa zikipungua kwa wanaume tangu 2000.

Hatukuona mabadiliko mengi kwa wanaume ambao tulishirikisha kwenye utafiti wetu kati ya 2017-2022,” akasema mmoja wa watafiti hao Profesa Allan Pacy wa Chuo Kikuu cha Manchester.

Pia hakukuwa na ushahidi kuwa aina ya virusi vya corona SARS-CoV-2 vinaathiri moja kwa moja uundaji wa mbegu za kiume.

Hata hivyo, walikiri kuwa kafyu zilichangia kubadilika kwa mtindo wa maisha hasa kikazi na kiasi cha mazoezi.

Mabadiliko haya yangeathiri kuundwa kwa mbegu za kiume japo si kwa kiwango kikubwa.