Ajuza 115, apigania ardhi na mjukuu wake
MWANA wa aliyekuwa mkuu wa kampuni ya Gateway Insurance, marehemu Godfrey Wairegi, ameungana na mama yake katika mzozo dhidi ya nyanya yake mwenye umri wa miaka 115 kuhusu umiliki wa ardhi ya thamani ya mamilioni ya pesa eneo la Nakuru.
David Wairegi Karuri, pamoja na mjane wa marehemu Wairegi, Jelioth Wanjira, wamewasilisha kesi tofauti katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi wakidai umiliki wa mashamba mbalimbali ambayo kwa sasa yanamilikiwa na mama wa Wairegi, Esther Wangui.
Katika kesi yake, Bw Karuri anataka nyanya yake apigwe marufuku kuingilia au kufanya shughuli zozote katika shamba la Njoro Ndarugu Plot No. 17 lililoko Kaunti Ndogo ya Njoro, Kaunti ya Nakuru.
Anamlaumu nyanya yake huyo kwa kushirikiana na afisa wa ardhi kutwaa umiliki wa shamba hilo kwa njia ya ulaghai bila yeye kujua wala kuidhinisha.
Kwa mujibu wa Bw Karuri, shamba hilo lilikuwa la marehemu baba yake, ambaye kabla ya kufariki mnamo 2012, alimpa yeye na mama yake (nyanya wa Karuri).
Anadai kuwa ardhi hiyo ilikuwa imeandikishwa kwa majina yao wote hadi mwaka 2024 alipogundua kuwa nyanya yake alikuwa ametumia mbinu za ulaghai kuondoa jina lake kwenye sajili ya ardhi.
“Mlalamishi hakuwahi kutia saini hati yoyote ya kuhamisha umiliki wala kupokea malipo yoyote kwa sehemu yake ya ardhi,” alisema Bw Karuri.
Sasa anataka mahakama iamuru afisi ya ardhi kurejesha jina lake kama mmiliki mwenza wa shamba hilo na pia kuzuia nyanya yake kuuza, kukodisha au kufanya miamala yoyote hadi kesi isikilizwe na kuamuliwa.
Bi Wangui, ambaye amemkabidhi mwanawe John Gakure mamlaka ya kusimamia masuala yake kisheria, amekanusha madai hayo, akisema kesi hiyo ni njama pana ya kumhangaisha na kunyakua mali aliyogawiwa na watoto wake.
Kwa mujibu wa Bi Wangui, mjukuu wake na mkaza mwana wake wamemfungulia mashtaka mengine mawili wakilenga kumvua umiliki wa mashamba mbalimbali.
Anadai kuwa ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo kwa mujibu wa barua ya ugawaji ardhi aliyopatiwa mwaka 1988.
“Mshtakiwa anasisitiza kuwa hati ya kumiliki ardhi hiyo haijawahi kutolewa, na barua ya ugawaji pekee ndiyo thibitisho kuwa yeye ni mmiliki wa shamba hilo,” Bw Gakure alisema.
Kesi ya mjukuu huyo inaongezea mvutano mwingine ulioko mahakamani ambapo mama yake anagombania ardhi nyingine na nyanya yake.Ardhi hiyo ina nyumba ya vyumba vinne yenye thamani ya zaidi ya Sh15 milioni katika nusu ekari huko Njoro, Kaunti ya Nakuru.
Bi Wangui anadai alirithi nyumba hiyo kama zawadi kutoka kwa watoto wake, akiwemo marehemu Wairegi.
Lakini mkaza mwana anasisitiza kuwa alishiriki kuinunua pamoja na mumewe na kwamba, ilikuwa imesajiliwa kwa jina lake.
Katika kesi iliyowasilishwa mwaka 2016 na Bw Gakure, kupitia wakili Njuguna Matiri mahakama iliambiwa kuwa lilikuwa wazo la marehemu Wairegi watoto kununua nyumba na ardhi kwa ajili ya mama yao kupitia mchango wa pamoja.
Mahakama iliambiwa kuwa ndugu yao mmoja, Simon Peter Mwangi, ndiye aliyeitambua nyumba hiyo iliyokuwa inamilikiwa na Prof Francis Kibuba, huku mwingine, Dkt Tom Wairegi, akichangia Sh600,000 kutoka Amerika kuinunua.
“Ni wazi kutokana na mawasiliano kuwa kusudi lilikuwa kumzawidi mama nyumba na ardhi,” alisema Bw Gakure.Kesi hiyo iliwasilishwa baada ya kugundua kuwa mjane alikuwa amesajili ardhi hiyo kwa jina lake pekee.
Katika utetezi wake, Bi Wanjira alikanusha madai hayo, akisema alipewa umiliki kamili baada ya mumewe kufariki 2011, na kwamba wakwe zake wanatumia mamlaka ya mama yao kama njia ya kumdhulumu.Anasisitiza kuwa mama mkwe hana haki yoyote ya kisheria wala ya usawa kuhusu ardhi hiyo na huenda hata hafahamu uwepo wa mzozo huo ulio mahakamani.
“Sikufanya kosa lolote la jinai kwa kusajili ardhi kwa jina langu kwa kuwa nilifuata sheria,” alisema Bi Wanjira.Mahakama ilimpa Bi Wangui leseni ya kutumia shamba la Njoro/Njoro Block 5/309 hadi uhai wake utakapokoma, baada ya kupata kuwa alistahili sehemu ya ardhi hiyo kwa kuwa ilipatikana kupitia mchango wa wanawe.
Bi Wangui, hata hivyo, hakuridhika na uamuzi huo na akakata rufaa ambayo bado inasubiri kusikilizwa katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi.
Katika rufaa hiyo, anadai hakimu alikosea kwa kutotambua kuwa ardhi hiyo haikuwa sehemu ya mali ya marehemu Wairegi katika kesi ya urithi iliyosajiliwa mahakamani.