Akili Mali

AKILI MALI: Mkulima wa Ruiru aeleza jinsi mbolea vunde inavyoundwa

Na PAULINE ONGAJI August 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 3

KWENYE kipande chake cha ardhi eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, Bw Richard Mwangi, pamoja na wafanyakazi wake, wanaendelea na shughuli ya kuunda mbolea vunde yaani ‘organic fertilizer’.

Bw Mwangi ni mwanzilishi wa Organic Fields, kiwanda cha kuunda mbolea vunde kwa kutumia taka za sokoni, na hasa za mazao ya shambani.

“Taka hizi zinakusanywa kutoka soko la Ruiru, kuchambuliwa na kuozeshwa ili kupata kiwango cha juu cha mboji. Kisha mboji hiyo inachujwa na kuchanganywa na kaboni na jivu, mifupa iliyosagwa na mawe, kabla ya mchanganyiko huu wote kusagwa ili kutoa mbolea vunde kwa jina Hygrow Organic Fertilizer,” aongeza Bw Mwangi.

Kwa kufanya hivi, Bw Mwangi anachangia pakubwa katika kuzuia kuzalishwa kwa gesi hatari ambazo zimehusishwa na ongezeko la joto duniani.

Kulingana na wataalam, barani Afrika, matumizi mabovu ya ardhi yamechangia pakubwa mabadiliko ya tabianchi. Matumizi haya hasa yanahusisha mbinu za kilimo kwa kutumia mbolea za kemikali kali.

Kulingana na wataalam, gesi ya nitrogen inayopatikana katika mbolea za kemikali, inapokuwa wazi kwenye udongo, huathiriana na viumbe hai, na hivyo kuzalisha gesi ya nitrous oxide.

“Gesi hii ni hatari mara 300 zaidi katika kusababisha ongezeko la viwango vya joto duniani, ikilinganishwa na ile ya dioksidi ya kaboni,”aeleza Dkt Paul Matiku, mwanaekolojia na mtaalamu wa uhifadhi na ustawi wa rasilimali, vile vile mkurugenzi mtendaji katika shirika la uhifadhi mazingira la Nature Kenya.

Aidha, kemikali hizi huathiri uwezo udongo kufyonza kaboni. “Ufyonzaji wa gesi ya kaboni kupitia udongoni ndio mbinu ya kawaida zaidi ya kuondoa gesi hii hewani,” aongeza Dkt Matiku.

Kulingana na Bw Mwangi, wateja wao hasa ni wakulima wadogo, watunza bustani mijini, watunza miche na watunza bustani.

“Mwaka huu tunapanga kusambaza mbolea hii miongoni mwa wakulima 50,000 wadogo,” aongeza Bw Mwangi.

Kampuni hii imepiga hatua zaidi na kutoa mafunzo ya umuhimu wa kutumia mbolea vunde kwa wakulima 30,000 katika kaunti kadhaa.

“Tumefunza wakulima katika kaunti kama vile Kiambu, Murang’a, Nyeri, Makueni, Kirinyaga, Embu, Meru, Tharaka-Nithi, Laikipia, Nyandarua, Machakos, Kitui na Nakuru,  miongoni mwa zingine,” aeleza.

Wafanyakazi wakiandaa mbolea vunde katika shamba la Organic Fields mtaani Ruiru, Kaunti ya Kiambu. Picha| Richard Maosi

Kando na miti, kulingana na wanasayansi, udongo unasaidia sana katika kufyonza kaboni ambayo ni mojawapo ya gesi hatari zinazosababisha viwango vya halijoto kuongezeka duniani.

Utafiti uliofanywa na shirika la The Organic Center kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Northeastern University, nchini Amerika, ulionyesha kwamba mashamba ambapo kilimo asilia kinaendelezwa, yana uwezo mkubwa wa kuhifadhi kaboni udongoni kwa muda mrefu.

“Aidha, udongo wenye afya unaotokana na kilimo asili – pasipo matumizi wa mbolea za kemikali – husaidia wakulima kubadili mbinu za kilimo ili kustahimili ukame na mafuriko, majanga ambayo tayari yamekithiri kutokana na mabadiliko ya tabianchi,”aeleza Dkt Matiku.

Mchango wa Organic Fields katika kuendeleza kilimo endelevu umetambuliwa. Mwaka wa 2021, shirika hili lilipokea ufadhili wa Sh5M kutoka  kwa Wakfu wa Ustawi wa Afrika wa Amerika USDAF, kwa ushirikiano na Wakfu wa Stanbic Foundation.

“Kabla ya ufadhili, uwezo wetu wa kuzalisha mbolea hii ulikuwa mdogo sana, na hivyo hatungeweza kutimiza mahitaji ya soko letu. Aidha, kulikuwa na changamoto ya kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu mbinu hii,” aeleza Bw Mwangi.

Kupitia ufadhili huo, asema, kumekuwa na ongezeko la kiwango cha uzalishaji wa mbolea kutoka tani 4 hadi tani 20 kwa siku, huku idadi ya wafanyakazi ikiongezeka na kufikia 60.

Tatizo kuu asema ni kwamba sekta ya kuchakata taka na uzalishaji wa mbolea vunde ni mpya hapa nchini, na hivyo inakumbwa na changamoto za kidhana kutoka kwa mashirika ya serikali, taasisi za kifedha, vile vile wakulima.

Lakini wamefanikiwa kukabiliana na changamoto hii kwa kuwasiliana moja kwa moja na mashirika ya serikali.

“Tumekuwa tukiwaalika kuja kuzuru eneo ambapo shughuli zetu zinaendelea ili kujifunza na kushauriana. Pia, tumekuwa tukiwasiliana na taasisi za utafiti kama vile vyuo vikuu, KALRO na vituo vya mafunzo ya kilimo katika viwango vya kaunti,” aongeza.

Kwa sasa wanapanga kuendeleza shughuli hizi katika miji mingine kama vile Nakuru, Eldoret, Mombasa na Bungoma, ili kuongeza kiwango cha uzalishaji mbolea.

“Pia, tunapanga kupanua shughuli zetu hadi nchini Uganda mwaka huu, kwani tuna wateja ambao wameonyesha nia ya kutaka kutumia mbolea yetu huko.”

Kulingana na wataalam wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, utunzaji wa udongo ni mojawapo ya mbinu zitakazoisaidia Afrika na ulimwengu wote kwa jumla, kukabiliana na uzalishaji wa gesi nusuru Afrika kutokana na uzalishaji wa gesi hizi hatari.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Cambrige nchini Uingereza unaonyesha kwamba endapo matumizi ya mbolea za kemikali yatapunguzwa, basi uzalishaji wa gesi zinazoongeza kiwango cha joto duniani zitapunguka hadi asilimia 20.