Akili Mali

Anasaidia akina mama kuunda bidhaa tofauti tofauti ili kupata riziki

Na PETER CHANGTOEK December 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BALKHISA Bashir aliposafiri kuenda Uingereza miaka ya tisini, hakujua kuwa angeenda kuanzisha shirika ambalo lingewasaidia watu kujiinua kiuchumi na kujitegemea, hususan akina mama.

Yeye ni mwasisi mwenza wa shirika lisilokuwa la serikali (NGO), linalojulikana kama Barwaqa Relief Organization, aliloliasisi na Hussein Dima.

Walilianzisha baada ya kuona changamoto ambazo wakimbizi walikuwa wakizipitia kule Uingereza.

Balkhisa aliamua kuzileta huduma za shirika hilo hadi Kenya, ambapo amekuwa akiwahamasisha akina mama kuhusu jinsi ya kuanzisha biashara na kuweka akiba ya pesa wanazozipata kutoka kwa biashara zao.

Baadhi ya ya wale wanaonufaika kutokana na Barwaqa Relief Organization, wakitengeneza sabuni ya maji. PICHA|PETER CHANGTOEK

Pia, amekuwa akiwapa mafunzo yanayojulikana kama ‘Master of Business in the Street’ (MBS), na kuwapa vyeti baada ya kumaliza mafunzo hayo. Wale ambao amekuwa akiwafunza wamepata ujuzi wa kuzitengeneza bidhaa tofauti tofauti, zikiwemo bangili, mikufu, herini, vikapu, sabuni, mishumaa, keki, na bidhaa nyingine nyinginezo za shanga.

Huwahamasisha na kuwafunza ili wajue kujitegemea, na baada ya kuzitengeneza bidhaa zao, huziuza kwa wateja tofauti tofauti, na kupata hela zinazowasaidia kujikimu. “Ni mbinu ya kujitegemea. Tunawafunza pia waweke akiba, si kuuza tu na kutumia pesa. Ninataka wawekeze ili wajitegemee. Baadhi yao huwalipia watoto wao karo za shule,” aeleza Balkhisa, akiongeza kuwa, wengi wao hutoka Kibra na Mukuru.

Balkhisa anasema kwamba, kikapu kimoja kikubwa huuzwa kwa Sh2,500, na wanapoviuza vikapu 10 hupata Sh25,000, na huwashauri kutenga angaa Sh1,000 kutoka kwa hela hizo kama akiba.

Wanaonufaika kutokana na mafunzo yanayotolewa na Balkhisa Bashir, waonyesha bidhaa wanazozitengeneza kwa kutumia teknolojia ya screen printing katika eneo la Embakasi, Nairobi. PICHA|PETER CHANGTOEK

Anaongeza kuwa, baadhi ya akina mama hao hupenda kupelekwa kwa vyuo vinavyotoa mafunzo tofauti tofauti, kama vile ushonaji, na shirika hilo hugharimia mafunzo hayo. “Kuna wale wanaojua kutumia mashine za kushona, na tunawapeleka Eastleigh. Wengine wao tayari wako kazini,” asema, akiongeza kuwa, kozi ya ushonaji huchukua miezi mitatu.

“Tunawalipia mafunzo na nauli. Wanawake hao kwa sasa hutumia ujuzi wao. Tunataka wajitegemee,” aongeza Balkhisa.  Anadokeza kwamba, kuna baadhi yao ambao hufunzwa kupika. Mafunzo ya kupika hayachukui muda mrefu; huchukua siku tatu tu, na wao hupata ujuzi wa kutosha. “Wakati mwingine sisi huwaita tunapokuwa na hafla, na huja kupika na kulipwa,” adokeza Balkhisa.

 

Wanachama wanaonufaika na mafunzo yanayotolewa na Balkhisa Bashir, katika eneo la Embakasi, Nairobi. PICHA|PETER CHANGTOEK

Anasema kwamba, mafunzo ya utengenezaji wa sabuni huchukua muda wa wiki moja kwa sababu kuna aina nyingi za sabuni wanazofaa kufunzwa kuzitengeneza. Balkhisa anasema kwamba, wengi wa wale ambao wamefunzwa katika shirika hilo Swaminathan biashara mbalimbali wanazozipenda.

Mbali na kutoa mafunzo kwa akina mama, shirika hilo la Barwaqa Relief Organisation, limekuwa likitoa usaidizi wa kifedha kwa watu wasiojiweza katika jamii, hususan wanawake. Miongoni mwa maeneo ambapo Balkhisa na shirika lake limetoa msaada ni pamoja na Mandera, Garissa, Wajir, Isiolo, Tana River, Bomet, Kajiado, miongoni mwa mwengine.