Anatumia wadudu aina ya BSF kufuga samaki
WADUDU wanaojulikana kama black soldier fly (BSF) wana uwezo wa kupunguza gharama ya uzalishaji kwa wakulima tofauti tofauti, hususan wale wanaoshughulika na ufugaji wa samaki, kuku, pamoja na ndege wengine.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya lishe za mifugo ni kwamba, wadudu hao wana kiwango kikubwa cha protini – inayosaidia katika ukuaji wa kasi kwa samaki au kuku.
Mbali na kuwasaidia wakulima kuhakikisha kuwa samaki, kuku au ndege wengine wanaofugwa wanakua kwa kasi na kufikia uzani unaohitajika sokoni, BSF husaidia pia kupunguza gharama ya uzalishaji, endapo wakulima hao hao watajihusisha na ufugaji wa wadudu hao.
Katika eneo la Mtwapa, Kaunti ya Kilifi, mfugaji mmoja wa samaki amekuwa akiwafuga wadudu aina ya BSF ili kumsaidia kupunguza gharama ya uzalishaji, ambapo analenga kupunguza gharama ya uzalishaji kwa asilimia 50.
Eliana Nyaguthii Macharia anasema kuwa, wadudu aina ya black soldier fly wamemsaidia mno katika shughuli ya ufugaji wa samaki.
Aidha, Nyaguthie anasema kuwa, huuza mabuu ya BSF kwa wakulima wengine wanojihusisha na ufugaji wa kuku au samaki kutoka maeneo tofauti tofauti ya Kenya.
Mfugaji huyo anasema kwamba, huuza mabuu ya BSF na pia kuwapa mafunzo wale wanaonuia kujitosa katika ufugaji wa wadudu hao, ambapo wanaoyapokea mafunzo hayo hutozwa ada ya Sh500 au zaidi.

Pia, mabuu ya BSF huongezwa thamani na mfugaji huyo, kuambatana na oda za wateja.
Huongeza thamani kwa kusaga kuwa poda inayotumika hususan kwa ulishaji wa samaki wadogo wasiokuwa na uwezo wa kuzimeza lishe zenye saizi kubwa.
“Uongezaji thamani wadudu aina ya black soldier flies ni pana kwa sababu kuna wale waliokaushwa, kuna poda, na kuna oili ya BSF,” asema Nyaguthii, aliyejitosa katika ufugaji wa wadudu hao 2020, wakati wa ugonjwa wa Covid-19.
Anaongeza kwamba, wafugaji wa kuku ndio wanaonunua mabuu ya BSF kwa wingi.
“Poda ya BSF hutumiwa kama lishe za samaki wadogo kwa sababu wanapokuwa wadogo hula lishe ndogo,” asema Nyaguthii.
Anafichua kwamba, kilo moja ya poda ya BSF huuzwa kwa Sh1,000. Hata hivyo, kuna wateja wanaoomba kupunguziwa bei, ambapo huuziwa chini ya Sh1,000. Kwa wale waliokaushwa, mfugaji huyo huuza kilo moja kwa bei kuanzia Sh400 hadi Sh600.
“Wateja wengi wa BSF wanaofuga kuku hupenda kununua mabuu bila kukaushwa, ilhali wale wa samaki hupenda kununua waliokaushwa. Nina mashine ndogo ninayoitumia kusaga. Tuko katika harakati ya kununua mashine kubwa ya kusaga poda,” adokeza Nyaguthii.

Mfugaji huyo anasema kuwa, kreti moja ya mabuu ya BSF humpa kilo tano hadi sita, ambapo ana kreti kuanzia 20 hadi 30. Anasema kuwa, hutumia lishe tofauti tofauti kuwalisha wadudu wa BSF. Miongoni mwa lishe anazozitumia ni azolla.
Mfugaji huyo anasema kuwa, kuna changamoto kadhaa katika ufugaji wa wadudu hao. Mojawapo ya changamoto hizo ni kwamba, kunapokuwa na baridi, wadudu hao huwa hawazaani kwa wingi.
“Wateja wangu wengi ni wa hapa Pwani, na wengi hutaka kufunzwa jinsi ya kuwafuga wadudu hao. Kwa wanafunzi hutoza ada ya Sh500 kwa muda wa saa mbili, na Sh1,000 kwa siku nzima – hao hupata mafunzo ya ziada ya ufugaji wa samaki pia,” aongeza mfugaji huyo.