Matumaini ya bei nafuu ya bidhaa za nje baada ya shilingi kusalia thabiti dhidi ya dola
SHILINGI ya Kenya ilisalia thabiti dhidi ya dola ya Amerika baada ya Benki Kuu ya Kenya kupunguza viwango vyake kwa pointi 75 hadi asilimia 12.
Kufikia Ijumaa wiki jana, Oktoba 11, Soko la Hisa la London (LSEG) lilinukuu Shilingi ya Kenya ikibadilishwa kwa 128.50 dhidi ya dola ya Amerika.
Kulingana na wachambuzi, shilingi ya Kenya ilitarajiwa kuhifadhi uthabiti wake wiki hii.
Uthabiti wa Shilingi ya Kenya kwa wiki kadha umeimarishwa hasa na kuingia kwa dola kutoka nje ya nchi na mauzo ya chai. Ongezeko la dola zinazoingia nchini limeboresha kwa kiasi kikubwa akiba ya fedha ya nchi ambayo kwa sasa inafikia dola 8.2 bilioni
Uthabiti wa sarafu za Kenya pia umechangiwa na uamuzi wa Benki Kuu kuingilia kati viwango vya kubadilisha fedha. Akizungumza hivi majuzi katika Mkutano wa Sera ya Fedha, Gavana wa CBK Kamau Thugge alisema kuwa benki hiyo iliingilia kati.
“Sera yetu ni kuruhusu kiwango cha ubadilishaji kuamuliwa na nguvu za ugavi na mahitaji, hata hivyo, tunaingilia kati kimsingi kushuka kwa viwango vya juu vya ubadilishaji,” Thugge alibainisha.
“Hiyo ni sehemu ya jukumu letu na hufanyika wakati kuna haja ya kuingilia kati wakati kiwango cha ubadilishaji kinapoanza kudhoofika,” aliongeza.
Kulingana na ripoti ya Benki Kuu, Shilingi ya Kenya imesalia kuwa sarafu iliyofanya vizuri zaidi duniani, na kupata udhabiti wa asilimia 17 tangu Februari mwaka huu.
Katika miezi ya hivi karibuni shilingi ya Kenya imeshinda vikwazo kadhaa vilivyotishia uthabiti wake ikiwa ni pamoja na maandamano ya kuipinga serikali yaliyofanyika mwezi Juni na uamuzi wa Shirika la Ukadiriaji wa Mikopo la Moody wa kushusha hadhi ya Kenya.