Akili Mali

Wagonjwa wanavyochangamkia maziwa ya mbuzi na kumuinua kibiashara

Na KNA, LABAAN SHABAAN October 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ROBERT Macharia ni mfugaji wa mbuzi wa maziwa mwenye tajiriba ya miaka 13.

Anaendeleza kilimo biashara eneo la Githurai 45, Kaunti ya Kiambu na amefana sana katika sekta hii yenye ushindani mkali.

Shamba lake kwa jina Mwihoko Dairy Farm lilitambuliwa katika maonyesho ya kilimo ya Nairobi mnamo Oktoba 2023.

Alikabidhiwa tuzo hiyo na Rais William Ruto aliposherehekewa kwa mchango maridhawa katika sekta ya kilimo.

Akizungumza na shirika la habari la KNA, Macharia alisema safari yake ilianza kwa kutosheleza hitaji la maziwa nyumbani kwao.

“Kilichoanza kama juhudi ya binafsi kilinawiri na kuwa biashara inayostawi sababu ya kuongezeka kwa mahitaji ya maziwa ya mbuzi yenye thamani ya juu. Kwa sasa, shamba hili lina zaidi ya mbuzi 86, huku 33 wakikamuliwa na kuzalisha takriban lita 80 za maziwa kila siku”, alisema.

Akikumbatia kanuni za kilimo mijini, Macharia anaeleza jinsi amefaulu kutumia shamba dogo zaidi ya thumni kuzidisha mapato.

Ubora wa maziwa yake hutokana na ulishaji mbuzi kwa lishe ya thamani ya juu ili kudumisha afya ya mnyama na kuendeleza hadi kwa wateja.

“Wateja wa msingi wa shamba hili ni pamoja na watu wenye mahitaji maalum ya kiafya, pamoja na wale wanaougua ugonjwa wa yabisi (athritis), maradhi ya ngozi, na matatizo ya umeng’enyaji wa sukari inayopatikana katika bidhaa za maziwa,” anaeleza.

“Takriban asilimia 70 ya wateja wanatumia dawa na wanavutiwa na faida nyingi za maziwa ya mbuzi. Kwa hivyo, hii imesababisha mahitaji kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

Zaidi ya hayo, Macharia hupata faida kutokana na kutoa mafunzo ya njia bora ya ufugaji akitoza ada ya angalau Sh2, 000 kwa mteja.

Ushirikiano

Kadhalika, anasema kuwa shamba hilo linashirikiana na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali ili kukuza biashara za kilimo miongoni mwa vijana.

Ana maono ya kuwapiga jeki watu wasiojiweza kupitia elimu ya ukulima.

Tayari ameshirikiana na vyuo vikuu kadhaa kama vile Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Chuo Kikuu cha Egerton na Chuo Kikuu cha Eldoret ambavyo hutuma wanafunzi wao kujifunza shambani mwake.

Macharia anakiri kuwa ushirikiano huu umemwongezea sifa na ushawishi katika sekta ya kilimo.

Ufanisi wake umejikita sana katika chaguo lake la kufuga mbuzi wa maziwa huku wakulima wengi wakizamia ufugaji wa ng’ombe na kuku.

Macharia analenga kuongeza mbuzi wake wafike 1000 katika kipindi cha miaka mitano ijayo atapakapoongeza thamani katika maziwa.