Makala

AKILIJIBU: Mbona kuku wangu hunyong’onyea, kujikunga na kujifia ovyo?

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SWALI: PAMNAS BOSIRE kutoka Lugari, Kaunti ya Kakamega angependa kujua kiini cha kuku wake kuonekana wanyonge, kujikunja sana na kufa ovyo kwa mkupuo.

JIBU: Huenda wameathiriwa na kinyong’onyea, ugonjwamaarufu kama Coccidiosis. Pania sana kubaini iwapo kuna chembe za damu katika kinyesi cha kuku wako au wana mazoea ya kunywa maji mengi nyakati za asubuhi hata kabla hujawapa lishe.

Iwapo rangi ya kinyesi itabadilika kuwa manjano baada ya muda, basi huenda wamevamiwa na vimelea vya protozoa. Dalili ya uvamizi huu ni kuku kujikunja kanakwamba wana baridi kali na hata kukosa kabisa hamu ya kula.

Fika katika maduka ya kuuza dawa za mifugo uelekezwe kuhusu namna mwafaka zaidi ya kukabiliana na viini vya Coccidia.

SWALI: DUNCAN KIMELI kutoka Bomet ni mfugaji wa ng’ombe. Anataka kujua aina bora zaidi ya nyasi zitakazozidisha kiwango cha maziwa ya mifugo wake.

JIBU: Wape mifugo wako kiwango kikubwa cha Nappier, Boma Road au nyasi aina ya Rhodes hususan X-Tozi, Elmba, Mbarara na Masaba.

Hakikisha kwamba ng’ombe wako wanapata maji ya kutosha na chakula kilicho na viini-lishe mbalimbali, hasa vitakavyochochea kuongezeka kwa kiwango cha maziwa.

Nyasi aina ya Boma ndiyo hupandwa sana hapa Kenya kwa kuwa inakubali mazingira ya aina nyingi.

Ingawa Boma hustahimili ukame, mkulima anapotengeza marobota (hay bales) kutokana na nyasi hizi, anastahili kuzikata wakati zimeota maua au zikiwa bado na rangi ya kijani. Usisubiri hadi nyasi zikauke ndipo uanze kuzikata.

SWALI: JOACHIM KIBOI kutoka Kabete anauliza kiini cha mbegu zake za sukumawiki kutoota kwa kiwango sawa ikilinganishwa na zile za mnavu au spinachi anazozikuza vilevile.

JIBU: Kuwa na mazoea ya kununua mbegu zako kutoka kwa maduka yaliyoidhinishwa kama vile Simlaw Seeds au Kenya Seed ambayo yanatambulika kwa ubora wa mbegu.

Unapotayarisha vitalu kwa ajili ya upanzi, lainisha mchanga iwezekanavyo.

Nyuzijoto za eneo ulilotaja zinaruhusu ukuzaji wa sukumawiki, hivyo mbegu zinafaa kuota bila matatizo. Usirudie upanzi katika kitalu kimoja mara mbili.

Ukipanda hapa msimu huu, msimu unaofuata tayarisha kitalu penginepo. Usipande karibu na kivuli cha miti.

Hakikisha mimea inapata jua na joto la kutosha.

Mchanga wako haufai kuwa na Nitrojeni nyingi.