• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:00 PM
AKILIMALI: Arejea nchini kutoka China kufunza vijana jinsi ya kushona mavazi na mapambo

AKILIMALI: Arejea nchini kutoka China kufunza vijana jinsi ya kushona mavazi na mapambo

NA RICHARD MAOSI

[email protected]

Maonyesho ya mapambo na nguo za kiasili ni kazi za mikono ,zinazohitaji ubunifu wa aina yake ambapo ubora na usasa ni mambo mawili ya kuzingatiwa.Aina mpya ya mitindo ikiwa ni baadhi ya mambo ya kutiliwa mkazo.

Mbali na kilimo biashara jukwa la mapambo na mavazi, limekuwa likiwaleta pamoja wauzaji na wanunuzi kutoka kila sehemu ulimwenguni ili waweze kubadilishana mawazo na kujiongezea soko hadi kiwango cha kimataifa.

Mashuka, shati na mitandio yenye nakshi za aina ya kipekee, zimepenya na kuimarisha utalii, ukuaji wa viwanda na kutoa fursa nzuri kwa wauzaji na wanunuzi wa nje kujenga uhusiano mzuri.

Aidha vijana wengi wamefanikiwa kujitengenezea nafasi nyingi za ajira, badala ya kutegemea kazi za ofisini ambazo ni nadra kupatikana siku hizi.

Adrienne Juma ni mmoja wa wajasiriamali wanaotumia ubunifu wa kusuka shanga, mavazi ya kiasili,bangili, mikufu, fulana na marinda kwa jinsia ya kiume na kike kwa kutumia vitambaa vya kawaida.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali anaamini kuwa msukumo wa kubuni mavazi ya kipekee unategemea semina za kitaaluma,maonyesho na hamasisho la kila mara ili kuonyesha njia kamili ya kutengenea mavazi yenye thamani.

Akiwa mkaazi wa kaunti ya Nakuru alianza shughuli yenyewe mnamo 2018, baada ya kuhitimu shahada katika maswala ya kibiashara kutoka chuo kikuu cha Shanghai China, kozi aliyosomea kwa miaka minne.

Aliporejea nchini Kenya alitaka kujianzishia biashara yake mwenyewe ili ajiongezee kipato, kwani aligundua kuwa kupata ajira sio jambo rahisi kama alivyofikiri akiwa bara Asia kama mwanafunzi kabla ya kurehjea humu nchini.

Juma alishirikiana na mwenzake Valerian Lewama, ambapo walitumia mabaki ya nguo yaliyotupwa kutoka kwenye maduka ya kijumla. Anasema hakuhitaji mtaji wowote isipokuwa ujuzi kwa sababu mabaki ya nguo ni bure wala hayahitaji kununuliwa.

“Haikupita miezi sita tulipata ufuasi mkubwa mtandaoni hususan wasanii na wanamitindo walianza kuwania huduma zetu ili tuwatengenezee mavazi au kuwaandalia hafla ya burudani katika kumbi mbalimbali,”Juma akasema.

Kutoka hapo Valerian na Adrienne waliamua kupanua biashara yao na kuwapatia watoto wanaorandaranda mitaani jukwaa la kujifundisha ufundi, wa kutengeneza mapambo na mavazi,ili waje kujipatia njia ya kujikimu kimaisha.

Valerian aliwafundisha namna ya kujitafutia soko kwa bidhaa zao wengi wao wakiwa wanatokea katika familia maskini za mitaani kama vile Pondamali, Rhonda, Freearea, Bondeni, Kaptembwa na Lanet.

Miongoni mwa stadi nyinginezo ambazo vijana walipatiwa ujuzi ni katika jukwaa la muziki,uchoraji na uchongaji wa aina mbalimbali ya vinyago ambapo baadhi yavyo huuzwa kupitia njia ya mtandaoni.

“Tumefanikiwa kuwashawishi wanunuzi kutoka Marekani ikizingatiwa kuwa wazungu wanaenzi utamaduni wa mwafrika kwa sababu ya upekee wake na stadi ya kusuka mambo kwa ubunifu,” akasema.

Adrienne anawashauri vijana kupenda na kuenzi kazi ya mikono yao kwa sababu ndio njia ya kipekee ya kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini, ambalo huenda linawakodolea macho wengi waoendapo hawatajitambua mapema na kuchukua hatua.

Akiwa kielelezo chema katika jamii anawashauri vijana kuwa sio lazima mtu apate taaluma ya hali ya juu ,ili aweze kufanikiwa maishani bali bidii ,subira na ukakamavu ni viungo muhimu katika safari ya kupata mafanikio maishani.

“Vijana ndio viongozi wa kesho na wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kusaidia taifa kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira,jambo ambalo limewafanya vijana wengi kukata tamaa maishani,” Valerian aliongezea.

Kulingana naye anaunga mkono wazo la Rais Uhuru majuzi kuwa kila siku ya Ijumaa iwe ni siku ya wakenya kuvalia mavazi ya kiasili ili kuwatambulisha kimataifa na utamaduni wao.

Anasema kuwa bei ya bidhaa zao sio ghali kama inavyofikiriwa na watu wengi, kwa sababu wanauza bidhaa kuanzia shilingi 30 hadi zile za 6000, kwa kutegemea mahitaji ya mnunuzi na hafla ya matumizi.

Cha msingi kikundi chao kinatilia maanani usasa na utamaduni,ikiaminika kuwa vijana wengi siku hizi wanataka kutambuliwa kupitia mwingiliano kati ya usasa na ukale na kulingana na Juma hii ndiyo fasheni halisi.

Sehemu ya kutia nakshi na mapambo ya rangi katika mavazi inahitaji hatua kadhaa, kwanza ni msanii au mpakaji rangi aelewe maana ya kila rangi na muktadha wa matumizi.

“Tunanunua vitambaa vya hali ya juu na rangi kutoka kwenye viwanda na sisi hupaka rangi inayokolea vizuri ili isiweze kuchujuka kwa urahisi ikutanapo na miale ya jua wala mvua,” Juma aliongezea.

Anasema kuwa ubora wa mavazi hupotea pale mnunuzi anapofua nguo zake akagundua kuwa baadhi ya sehemu muhimu zimeanza kupata uchakavu, au kopoteza rangi yake ya asilia.

Juma anasema kuwa baadhi yetu tumekuwa tukivalia mavazi bila kufahamu mazingira, na hivyo tunaishia kuwa kituko mbele yawatu waliohudhuria sherehe maalum wakiwa na lengo fulani.

Anasema kuwa sherehe nyingi siku hizi hufanyika mijini ambapo kuna matabaka ya aina tofauti ya watu ambapo bila shaka wao hutangamana kwa ajili ya kikazi au kibiashara.

“Cha msingi ni mtu ajitambue kupitia mavazi yake ambayo hayawezi kufananishwa na tamaduni yoyote ile,” aliongezea.

You can share this post!

Masaibu ya timu ya Taekwondo kutoka Maai Mahiu

Shamrashamra za Krismasi zanoga jijini Bethlehemu

adminleo