AKILIMALI: Binti mfugaji hodari wa sungura
NA PETER CHANGTOEK
UFUGAJI wa sungura ni shughuli ambayo imekuwa ikiendeshwa aghalabu na vijana wa kiume. Lakini sasa kina dada wamejitosa katika ulingo huo katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika eneo la Othaya, kaunti ya Nyeri, mwanafunzi mmoja wa kike hushughulika na shughuli ya ufugaji wa sungura, kilimo ambacho yeye huwa na fahari kwacho.
Teresa Kibiri, 22, ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo cha kitaifa cha anuwai cha Nyeri. Anasomea taaluma ya kutengeneza fasheni, lakini yeye hutumia muda wake wakati ambapo hayuko darasani kuiendeleza shughuli ya ufugaji wa sungura.
“Chuo chetu kiko karibu na hapa nyumbani, kwa hivyo, wakati siko darasani mimi huwashughulikia sungura wangu,” adokeza Bi Teresa.
Anasema kwamba alijitosa katika ufugaji wa sungura miaka miwili iliyopita, na wazo la kukianzisha kilimo hicho lilitoka kwa dada yake mkubwa, Zipporah Kibiri ambaye alimhimiza kufanya hivyo.
“Nilianzisha kwa kutumia Sh5,000 nilizopewa na mama,” asema, akiongeza kuwa aliianzisha shughuli iyo hiyo kwa kuwanunua sungura wanne aina ya ‘California white’ na ‘Flemish giant’.
Aliwanunua wawili wawili; wa kike na wa kiume na wakaongezekaongezeka hadi wakati huu ambapo ana sungura takribani tisini.
Teresa alikata kauli ya kujitosa katika ufugaji wa sungura baada ya kuyasoma makala fulani kuhusu shughuli hiyo mtandaoni. Anaongeza kwamba alipoyasoma makala yayo hayo, akagundua kuwa sungura ni wanyama wazuri.
Hali kadhalika, anafichua kuwa mtaji unaohitajika kukianzisha kilimo hicho si mwingi mno. “Mtaji unaohitajika ni kidogo kwa sababu unahitajika tu kuwanunua sungura wawili; wa kike na wa kiume, ambapo wao huongezeka upesi,” adokeza mkulima huyo.
Yeye huwalisha sungura wake kwa kuzitumia lishe tofauti tofauti, mathalan majani ya mimea mbalimbali, lishe aina ya ‘hay’, ‘pellets’, miongoni mwa lishe nyinginezo. Pia, yeye huwapa maji safi ili wayanywe.
Hata hivyo, anasema kuna baadhi ya changamoto ambazo zipo katika shughuli ya ufugaji wa sungura. Magonjwa kama vile nimonia, pamoja na wadudu kama vile viroboto, chawa na minyoo huwatatiza wafugaji, lakini huzuiwa au kuangamizwa.
Kwa mujibu wa Bi Teresa, ndaro nyingine ambayo humkabili ni ukosefu wa fulusi za kuiboresha au kuipanua biashara hiyo ya ufugaji wa sungura kusudi afaidike zaidi.
Mkulima huyo anafichua kuwa dada yake mkubwa humwauni kwa hali na mali, hususan katika shughuli ya kuwatafuta wateja mitandaoni.
Kwa mujibu wa mkulima huyo ni kuwa, kilo moja ya nyama ya sungura huuzwa kwa bei ya Sh550.
Aidha, Teresa humwuza sungura mmoja mwenye umri wa miezi miwili au mitatu kwa bei ya Sh800, ilhali yule mwenye umri wa miezi mitano na kuenda juu huuzwa kwa bei ya Sh1,500.
Anafichua kuwa nyama ya sungura huwa na soko, hususan katika mikahawa mikubwa mikubwa. Kupitia kwa mitandao ya kijamii, mathalan Facebook, mkulima huyo ameweza kuwauza sungura wake kwa wateja kutoka sehemu tofauti tofauti. “Nimeweza kuwauzia wateja kutoka sehemu za mbali kama vile Homabay,” aongeza.
Wao huzitumia mbolea kutoka kwa sungura kuikuza mimea mbalimbali. “Hutumia mbolea kukuza nyasi za ‘brachiaria’ na mahindi kwa sababu huboresha mchanga, huwa na virutubisho na ni rahisi kuzitumia,” aeleza mkulima huyo.
Mbali na ufugaji wa sungura, Bi Teresa, pamoja na aila yake, huikuza mimea ya stroberi, pamoja na mimea mingine mingineyo.
Mkulima huyo anawasihi vijana kujitosa katika shughuli za zaraa, maadamu zina faida. “Mipango yangu ya siku zijazo ni kuisajili kampuni yangu na kuwa na kandarasi na wafugaj,” asema, akiongeza kuwa soko la sungura lipo.