AKILIMALI: Binti muuguzi mjini Kitui lakini mkulima hodari Makueni
NA FAUSTINE NGILA
KWA kawaida si rahisi kumpata kijana mwenye ari ya kilimo isiyomithilika, aliyekivalia njuga kilimo liwalo na liwe, aliye tayari kukabiliana na changamoto zote za ukuzaji mimea hasa katika kaunti ambayo maji ni nadra, na zaidi ya yote awe msichana.
Akilimali ilipozuru maeneo ya kaunti ya Makueni ilipatana na msichana mmoja katika kijiji cha Wautu, Ilima, aliyejikita katika ukuzaji wa mboga bila kujali elimu yake ya juu na taaluma yake, akiamini kuwa kubadilisha jamii kunahitaji kujitolea katika kufanya unachoenzi bila kujali maneno ya vidudumtu, na hatimaye jamii hiyo itaona umuhimu wake.
Olive Mutheu ambaye tayari ni muuguzi katika Hospitali ya Kaunti ya Kitui alikuwa na msukummo wa kujitosa kwa kilimo, lakini alichohitaji tu ni mwongozo wa baba yake Bw Bonfrey Kituva ambaye amekuwa mkulima wa miaka mingi.
Binti huyu wa miaka 23 alivutiwa zaidi na ukuzaji wa nyanya mwanzoni mwa mwaka huu wakati baba yake aligura kukuza mimea ya kawaida kama mahindi na maharagwe na kuanza kukuza mboga. Hapo ni baada ya kuhitimu Shahada ya Uuguzi katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Kimathi mjini Nyeri.
Hivyo, babake alimpa kijisehemu cha shamba kutekeleza azma yake ya kuwa muuzaji wa nyanya, ikizingatiwa mita chache kutoka kwa shamba lao, kuna bwawa kubwa la maji yasiyoisha hata wakati wa kiangazi.
Lakini ndoto yake Olive haikutimia haraka kama alivyotarajia. Baada ya kutumia mtaji wa Sh10,000 kununua mbegu na dawa za kuua magonjwa, nyanya zake zilipatwa na ugonjwa wa kuoza na kutoboka kishimo cheusi wiki chache kabla ya kuvuna.
Baada ya kupata ushauri wa wakulima waliobobea kwenye ukuzaji wa nyanya, alinyunyuzia dawa za kutokomeza ugonjwa huo bila mafanikio na hivyo kuvuna kreti chache za nyanya.
Lakini uchunguzi wa Akilimali ulionyesha kuwa mchanga wa eneo hilo umekosa madini ya Calcium na kilimo chake kilikosa fatalaiza ya CAN.
Msichana huyu hakufa moyo, aliamua sasa kushirikiana na wazazi wake kukuza mimea mingine kama vitunguu, managu, sukumawiki, spinachi na kabichi huku akifanya utafiti kuhusu nyanya.
Baba yake Olive anatambulika katika eneo hilo kama mkulima shupavu aliye na ubunifu wa aina yake katika kilimo kutokana na mafunzo aliyopewa na serikali ya kaunti hiyo.
Licha ya vizingiti vya hapa na pale, ameweza kuwekeza vilivyo kwenye shamba lake. Amenunua mabomba ya maji ya urefu wa mita 80, jenereta ya kupiga maji kutoka bwawani na kujenga kidimbwi cha kuhifadhi maji kutoka bwawani.
Kwa sasa shamba nzima limejaa mimea ya kabichi aina ya Gloria F1 na managu iliyonawiri kutokana na utumizi wa mbolea, maji ya kutosha pamoja na kusharizia dawa za kuua magonjwa na wadudu hatari.
Na licha ya kupata hasara katika kilimo cha nyanya, kwa sasa Olive ana kila sababu ya kutabasamu kwani wameanza kuuza kabichi na pesa wanazopata zinawatia moyo.
“Bei ya kabichi hapa hutegemea ukubwa wake. Tunauza kati ya Sh30 na Sh70 kwa kila kabichi kulingana na kimo. Shamba hili lina kabichi 1,500. Kwa sasa baada ya kuwekeza Sh30,000 tunatarajia kupata Sh80,000,” anasema Bw Kituva.
“Kwa kawaida sisi hufanya kilimo hiki kama familia. Mume wangu hutafuta soko la mazao yetu pamoja na kutoa mwongozo kuhusu mimea tunayokuza, Olivehusaidia kwa shughuli za shambani na kutuma hela za kununua dawa, nami ninahakikisha mambo hapa shambani yamenyooka hasa katika upaliliaji na mauzo,” anasema mamake Olive, Bi Domitila Mutee.
Kwa sasa wakulima hawa wameamua kuingia kwa kilimo cha nyanya baada ya kupata ushauri tosha. Tayari wamehamisha miche kutoka kwa vitalu na inakaribia kuota maua.
“Raundi hii hatutarudia makosa tuliyoyafanya pale mwanzo. Wakati huo tulipanda nyanya aina ya Cal J lakini sasa tumepanda aina ya Kilele F1 ambayo inawiana na mchanga wa hapa. Pia tutatumia fatalaiza inayofaa kwa ukuzaji wake,” anasema babake Olive.
Lakini Olive ni vipi Olive anaweza kumudu kuhudumia wagonjwa hospitalini Kitui na kufanya kilimo hiki Makueni?
“Mimi hujulishwa kuhusu shughuli zote pale shambani kwa simu. Kama ni pesa za mbegu, nguvukazi au dawa ninaarifiwa kisha natuma. Wakati wa likizo, mimi huwa pale shambani wakati wote,” anasema mrembo huyu.
Juhudi za Olive, ukakamavu wake na mwongozo wa babake hatimaye umempa uso wa tabasamu. Anawashauri vijana watumie pesa zozote walizo nazo kuwekeza kwa kilimo.
“Kila jambo husalia ndoto hadi pale unajitolea kulitekeleza bila woga wa kufeli,” anamalizia.