AKILIMALI: Harufu tamu ya kahawa ‘tungu’ kibandani mwake itakutoa ute!
NA CHARLES ONGADI
ENEO la Pwani ni maarufu sana kwa unywaji wa kahawa hasa jioni baada ya pilkapilka za mchana kutwa za kusaka riziki.
Kuna aina mbili tofauti za kahawa ipendwayo na Wapwani.
Kuna ile chungu inayopendwa sana na wazee na tamu iliyo chaguo la vijana wengi.
Aghalabu ladha ya kahawa hulingana na jinsi mpishi anavyoshughulikia kinywaji hicho, kuna wale hupenda kuongezea viungo aina mbali mbali kama mdalasini na tangawizi.
Akilimali majuzi ilizuru mtaa wa Majaoni, Bamburi, Kaunti ya Mombasa na kukutana na Leonard Kithi Karisa, mpishi stadi wa kahawa chungu na tamu Mombasa.
Anapika kahawa tamu iliyo na ladha na harufu nzuri ya kuvutia na inayodondosha mate kila unapokaribia kibanda chake kilicho kandokando mwa barabara katika soko dogo la Kwa Charo.
Pia anauza njugu karanga ambazo wateja wake hupenda kutafuna wanapoburudika na kahawa chungu au tamu.
Wateja wake huanza kufurika jioni inapokaribia na ifikapo mwendo wa saa moja huwa wamefurika kila mmoja akipata utamu wa kahawa chungu au tamu kutoka kwa ‘Kanji Bai’ kama anavyojulikana na wateja wake wengi.
“Nina ufundi wa siku nyingi kuandaa kahawa chungu na tamu na ni biashara ambayo imeniwezesha kuikimu vyema familia yangu mbali na kuwalipia karo watoto wangu wawili walio shule ya upili,” anasema Kithi katika mahojiano yetu.
Awali aliajiriwa katika mojawapo ya hoteli za kitalii mkoani Pwani ila tu akaamua kuacha kazi hiyo na kujitosa katika biashara baada ya mtindo wa kusimamishwa kazi kila mara hoteli zinapokosa wageni kumchosha.
Kulingana naye, ari ya kujitosa katika biashara ilichochewa na nyanyake mzaa baba aliyekuwa mfanyabiashara na mkulima stadi Pwani.
Mwanzoni alianza na biashara ya kuuza Udongo katika soko Kuu la Kongowea kwa kipindi kifupi akisaka mtaji kabla ya kujitosa katika biashara ya upishi wa kahawa.
Je, alipata wapi ujuzi wa kupika kahawa ya kuvutia?
“Nilipata ujuzi wa kuandaa barabara kahawa chungu na tamu kipindi kile nilikuwa nikifanya kazi hotelini. Nilifunzwa na rafiki yangu aliyekuwa mweledi kwa mambo haya pale hotelini na baada ya kujua siri, nikaamua kujitoa kimasomaso katika biashara ya kuuza kahawa,” anasema.
Kithi anafichua kwamba mara baada ya kupata mtaji wa Sh500 aliamua kuanza biashara hii takribani miaka kumi iliyopita.
Mwanzoni alipitia changamoto kibao kama baadhi ya wateja wake kukopa na kukosa kumlipa kwa wakati ufaao wakati ndipo biashara ilikuwa ndio inaanza.
Anasema ili kupata kahawa nzuri na tamu ni lazima mfanyabiashara anunue kahawa halisi iliyo na harufu ya kuvutia na kisha kuchanganya na tangawizi iliyosagwa vizuri.
Kuna wakati huchanganya na viungo mbali mbali ambavyo ni nzuri kwa afya ya mnywaji.
Anauza kikombe kimoja cha kahawa chungu au tamu kwa Sh15 wakati kwa siku moja akiuza zaidi ya lita 100.
Anauza pakiti moja ya njugu kwa Sh10 na ambapo kilo moja ya njugu hutoa pakiti 26 wakati kwa siku anauza kati ya kilo 10 hadi 15.
Kithi anaeleza kwamba bei yake inalenga watu wa matabaka yote miongoni mwao wakiwa ni watu wa pato la chini, walimu, wanasiasa na hata madaktari wanaojumuika pamoja wakati wa jioni baada ya kazi.
Anaambia Akilimali kwamba uvivu ndilo jambo ambalo kwa miaka nenda miaka rudi limerudisha maendeleo nyuma maeneo mengi Pwani.
“Ikiwa vijana wetu watajitolea na kuwa wabunifu basi maisha ya uchochole tutakuwa tumeyazika katika kaburi la sahau. Siyo lazima kila kijana kuendesha bodaboda au kusoma hadi Chuo Kikuu ndio apate kazi bali pia wanaweza kubuni njia ya kujiajiri kupitia biashara,” anashauri Kithi.
Ndoto yake kuu ni kupanua zaidi biashara yake kiwango cha kuanzisha matawi katika vituo vya biashara mkoani Pwani.
Anasema biashara ya kuuza kahawa ina mikwanja kibao kutokana na kwamba mkoani Pwani unywaji kahawa chungu au tamu nyakati za jioni ni kama uraibu.