Makala

AKILIMALI: Kuku wa kienyeji wana faida

April 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

SAMUEL Kago anatabasamu anapohudumia kuku wake katika makazi yao na wengine aliowaachilia kujitafutia lishe.

Ni wa kienyeji, ambao amewafuga kwa minajili ya mayai na nyama eneo la Ngobit, kaunti ya Laikipia.

Kabla ya kuanza ufugaji wa ndege hawa wa nyumbani, Bw Kago alikuwa ametafuta ajira kwa muda wa miaka mitano mfululizo bila mafanikio.

Bw Samuel Kago, ambaye kwa sasa amefanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji; alisomea Stashahada ya Masuala ya Utalii. Picha/ Sammy Waweru

Amesomea Stashahada ya Masuala ya Utalii.

Alifuzu mwaka wa 2008, ndipo safari ya kuanza kutafuta kazi ikang’oa nanga.

“Kwa kipindi cha miaka mitano nilichokuwa kiguu na njia kutafuta ajira, kufikia sasa hakuna majibu niliyopokea licha ya kutuma wasifu wangu na vyeti vya kufuzu, katika mashirika na kampuni mbalimbali nchini,” anasimulia Kago.

Kulingana na barobaro huyu ni kwamba alipoona juhudi zake hazikuzaa matunda, alikata kauli ya kufanya vibarua vya kulimia watu mashamba Nyeri kwani ndiko ametoka.

Anadokeza kwamba kwa siku alikuwa akilipwa Sh400.

Shughuli hiyo aliifanya kwa muda wa miaka miwili, ambapo alifanikiwa kuweka akiba kuanza kufuga kuku. Anafichua kuwa iligharimu mtaji wa Sh25, 000 kuanza mradi huo mwishoni mwa 2015.

“Kuunda makazi ilinigharimu Sh7, 000. Nilinunua kuku 400,” anaelezea. Hata hivyo, 10 walifariki kwa ajili ya magonjwa. Changamoto kuu ilikuwa kudhibiti magonjwa.

Ugonjwa unaoshuhudiwa sana kwa kuku na kuwahangaisha ni Coccidiosis. Huharibu viungo vya kupumua dalili zake zikiwa kuhara, kukosa ladha ya kula, manyoya hafifu na kupukutika, damu na kamasi kwenye kinyesi. Dalili zingine ni kupungua kwa kiwango cha maji mwilini, na hata kuku kufariki kiholela.

Ili kukabili magonjwa, Okuta Ngura, mtaalamu wa masuala ya ufugaji hasa kuku, anashauri mfugaji kuhakikisha kizimba cha kuku kinasalia safi kila wakati.

“Usafi wa mazingira, chakula, maji, na vifaa vya kuwatilia lishe na maji, uwe wa hadhi ya juu,” anasisitiza Bw Ngura.

Viroboto kwa kuku si jambo geni na kulingana mtaalamu huyu ni kwamba wanadhibitiwa kwa kuweka makazi safi kila wakati. “Baada ya kufanya usafi, kuna dawa ya kupulizia sakafuni, ukutani na makazi yake ili kuua viroboto na vimelea wengine hatari kwa kuku hasa waliojificha,” anafafanua mdau huyu.

Wakati wa ujenzi wa makazi, kuku mmoja aratibiwe nafasi ya futi 2 mraba, ili wasisongamane na hata kumuwezesha mfugaji kufanya usafi ipasavyo. Kizimba pia kinafaa kuwa na mianya ya kuruhusu hewa safi, ya Oxijeni kuingia, na wanayotoa kutoka.

Licha ya milima na mabonde aliyopitia Bw Samuel Kago, amefanikiwa kustawisha mradi wake wa kuku wa kienyeji, na ambao kwa sasa umemuimarisha kukimu familia yake. Anasema kwa sasa ana zaidi ya kuku 100 wanaotaga.

Hii ina maana kuwa mfugaji huyu kwa siku hukusanya kreti tatu za mayai. Soko lake ni la kijumla, ambapo kreti moja huuza Sh550. “Sibagui wateja rejareja. Yai huwauzia Sh20, kwa kuwa pia nao wameniinua,” asema.

Kwa muda ambao amekuwa katika biashara ya kuku, Kago anasema kuku mmoja kwa siku hula chakula cha wastani wa Sh5. “Wao ndio hujinunulia lishe na kujitibu kupitia mapato yao, pamoja na kunipa faida,” anaeleza. La kutia moyo ni kwamba anapowafungulia majira ya adhuhuri kujivinjari, hujitafutia lishe katika mazingira yake.

Kuku anapaswa kulishwa mlo kamili, ambao ni mkusanyiko wa vyakula mbalimbali vyenye virutubishi au madini yanayotakikana.

Aidha, chakula cha kuku kiwe na madini ya Protini, Wanga, Vitamini na Mafuta. Wataalamu wa masuala ya ndege wanapendekeza Protini iwe zaidi ya asilimia 18.

Madini hii ni muhimu kwa sababu kuku hufugwa kwa minajili ya mayai na nyama, mazao ambao ni miongoni mwa yanayohitajika kwa binadamu kwa ajili ya Protini. Madini hii ni muhimu katika kusaidia uundaji wa mayai na nyama.

Wanga hupa kuku nguvu na kumuwezesha kula bila matatizo, kucheza pamoja na kumpa nguvu za kutaga. Madini ya Vitamini nayo hulinda mwili dhidi ya magonjwa ibuka, na Mafuta-kuupa joto la kutosha

Maji ni kiungo muhimu sana kwa wanyama. Kuku wakilishwa kisha maji yakosekane, wanaweza kufariki upesi. Itakuwa vigumu chakula kile kusagiga tumboni na kuenda haja. Ikumbukwe kuwa haja ndogo na kubwa kwa kuku hutoka pamoja

Mbali na kupata faida kupitia uuzaji wa mayai, mfugaji Kago pia huuza kuku wanapokomaa. Jogoo hugharimu zaidi ya Sh1, 000 na koo, kuku wa kike, Sh8, 000.