Makala

AKILIMALI: Mashine za kisasa zinavyopiga jeki wakulima wadogowadogo kuimarisha mazao

July 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MAOSI

JUHUDI za kuimarisha kiwango cha chakula kinachozalishwa humu nchini ni mojawapo ya ajenda za serikali kuu, na hali yenyewe inaonekana kuimarika kwa sababu wakulima wengi wameanza kushirikisha watafiti katika nyanja za teknolojia.

Mradi uvumbuzi wa kisasa unaweza kumpatia mkulima tija ya kutosha na kumwongezea kipato, hana budi kubadilisha mfumo wa kustawisha mimea. Anaweza kunyunyizia mimea maji, kupanda, kupalilia na kuvuna kidijitali.

Mataifa yaliyopiga hatua kubwa katika sekta ya kuzalisha chakula cha kutosha yanatumia dijitali kusimamia kila kitu ijapo katika shughuli za kuzalisha nguvu kazi.

Kwa CMC New Holland, mambo ni kama hayo, wamejihami kwa kubuni trekta za miundo ya kisasa zinazoweza kustahimili hali ngumu hasa maeneo kame yenye mawe.

Akizungumza na Akilimali, meneja Kenneth Mpaayei, mvumbuzi huyo anasema tayari CMC imewawezesha wakulima wengi kutoka mashinani kujizalishia mazao, wao wenyewe mara nyingi bila usimamizi.

Tulibaini kuwa miundo ya trekta za kisasa walizotengeneza ni kulingana na mahitaji ya mkulima, wanaolengwa zaidi wakiwa ni wakulima wadogo mashinani wasiokuwa na ujuzi wa kuendesha mashine.

Kenneth anasema mbali na trekta kutumika kulima shamba pia zinaweza kutumika kuzungushia mitambo inayozalisha umeme wa kawi kama vile genereta, katika mataifa yaliyoendelea baadhi ya trekta zimewekewa programu maalum inayompatia mkulima utaratibu wa kuitumia.

“Hata mazingira yawe kame kama vile kaunti ya Kajiado, kupitia serikali ya ugatuzi baadhi ya watu wameona haja ya kujifundisha namna mbalimbali ya kushirikisha mitambo bila kuharibu mimea,” akasema Kenneth.

Ufaafu wa trekta za kisasa kwa wakulima hauna kifani, kwa sababu mwendeshaji anaweza kujisitiri dhidi ya baridi kali au msimu wa jua kali.

Kufunikwa

Kulingana na Kenneth, trekta hizi huwa zimefunikwa vyema katika kila sehemu sawa na gari la kawaida ambapo mwendeshaji anaweza kufanya kazi yake wakati wowote bila kuathiriwa na ama baridi au joto kupindukia.

Katika eneo la Kabarnet Farm kaunti ya Nakuru, Boaz Barasa anasema yeye hutumia mtambo wa kukokota kuandaa shamba kwa misimu mitatu kila mwaka kupanda.

Aidha yeye hukodisha trekta kwa wakulima wengine wanaomzunguka na kujiongezea kipato, lakini cha msingi anawashauri wakulima kuhakikisha nati za tairi na sehemu za kushikia mitambo ya injini zimekazwa sawasawa.

“Hasara inayomfika mkulima ni pale baadhi ya sehemu zinapoanguka shambani na kupotea, na ikumbukwe kuwa sehemu hizi ni ghali,” Barasa akasema.

CMC Motors wamejaribu kutatua matatizo ya wakulima wadogo kama Barasa mashinani kwa kuvumbua mashine zenye uwezo wa kupanda, kupalilia kunyunyizia mimea dawa na kuvuna sawia. Mchakato mzima ukijaribu kuhakikisha kuwa mimea inapokea kiwango sahihi cha virutubishi muhimu visivyoweza kupatikana mchangani.