AKILIMALI: Mkojo wa sungura ni muhimu katika uboreshaji udongo wa kilimo
Na SAMMY WAWERU
SUALA la udongo wenye asidi kupita kiasi ni kizingiti kikuu kwa wakulima wengi nchini Kenya.
Waliozingirwa na changamoto hii wameishia kupigwa na dafrau la hasara, ambapo wanapata mazao kiduchu na ya hadhi ya chini.
Wataalamu wa kilimo wanasema hili linasababishwa na utumizi wa mbolea haswaa fatalaiza na dawa zenye kemikali.
“Fatalaiza na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, zenye kemikali zikitumika kilele chake ni kuharibu udongo,” anaonya mtaalamu na afisa wa kilimo Kirinyaga Bw David Kariuki.
Kulingana naye matokeo hayashuhudiwi pindi zinapotokana, ila baada ya muda fulani ambapo udongo hupoteza rutuba.
“Wadudu muhimu wanaosaidia kudumisha rutuba udongoni wakipuliziwa dawa zenye kemikali pamoja na fatalaiza, wanafariki. Isitoshe, asidi itokanayo na fatalaiza na dawa itazidi udongoni,” anafafanua mtaalamu huyu.
Wakulima wamekuwa wakishauriwa kuepuka matumizi ya pembejeo za aina hiyo, himizo likiwa; wakimbatie mfumo asilia au kilimohai, katika jitihada nzima kuendesha kilimo.
Himizo hilo linajumuisha kutumia mbolea ya mifugo, au mboji-ya mifugo iliyochanganywa na majani na matawi.
Pia, ni muhimu kutumia nyasi za boji (mulching) ili kukwepa kero ya wadudu na kuzuia walioko shambani kushambulia mimea na mazao.
Katika jukwaa hilohilo la mfumo wa kilimohai, mkojo wa sungura unaaminika kuwa tiba ya suala la asidi kuzidi kwenye udongo.
Rabbits Urine Extra, ni mboleahai ya maji inayotengenezwa kwa mkojo wa wanyama hawa wa nyumbani.
Robinson Runyenje, mtafiti, anasema mkojo wa sungura una madini ya aina yake, na yanayodumisha rutuba udongoni ikiwa ni pamoja na kudhibiti usambaaji wa magonjwa na wadudu.
“Wakulima wengi wamekuwa wakitumia fatalaiza yenye Calcium, Potassium, Nitrogen na Ammonia, kufanya kilimo hususan kwa minajili ya kuongeza mazao. Hilo linaweza kutatuliwa na mkojo wa sungura,” anasema mdau huyu.
Bw Runyenje pia anasema kinyesi – droppings – cha sungura pia ni mboleahai bora katika shughuli za kilimo.
Rabbit Genus Ltd, ni kampuni ya ufugaji wa sungura Juja, Kaunti ya Kiambu, inayomilikiwa na vijana watatu na ambayo inavuna mapato mazuri kupitia uuzaji wa mkojo wa wanyama hao.
“Tafiti zimebainisha kwamba mkojo wa sungura ni tiba ya changamoto zinazofika udongo, hasa kuzidi kwa kiwango cha asidi. Pia, hutumika katika uundaji wa mboleahai ya maji,” anasema msimamizi wa utendakazi Rabbit Genus Ltd, Bw Antony Mwangi.
Makazi ya mradi huo yametengezwa kwa muundo unaowezesha kuteka mkojo wa sungura kutekwa.
Sungura hula chakula maalumu aina ya pellets.
Pia, hulishwa majani ya mboga, makwekwe salama na hata masalia ya chakula cha binadamu.
Katika mazingira ya Rabbit Genus Ltd, kuna bustani wanayokuza mboga ambazo hulisha sungura wao.
“Hutumia kiasi kidogo cha mkojo tunaoteka kumwaga kwenye udongo, huwa hatutumii fatalaiza yoyote kuzalisha mboga, wala dawa dhidi ya wadudu na magonjwa,” anaeleza Bw Mwangi, akiongeza kwamba mbolea ya wanyama hao pia huitumia katika shughuli za kilimo.
Waasisi wengine wa Rabbit Genus Ltd ni mkurugenzi Rose Wanjiru, na mwanachama Esther Wanjiku.
Kampuni hiyo pia huuza nyama ya sungura na ngozi inayotumika katika kutengeneza bidhaa kama ngoma, mishipi na viatu.
Mwangi anasema lita moja ya mkojo ni takribani Sh100.
“Kwa wanaofahamu madhumuni ya mkojo wa sungura yana mapato,” anasema.
Mtaalamu wa masuala ya kilimo, David Kariuki, anahimiza wakulima kurejelea mfumo asilia kuendesha shughuli za zaraa ili kudumisha usalama wa udongo.
Pia, anashauri wakulima kupimiwa kiwango cha asidi cha udongo katika maabara, kabla ya kuanza kilimo.
Kuna mbinu maalumu kutibu udongo usioafikia vigezo vifaavyo.