AKILIMALI: Mwanachuo maarufu katika uchoraji, asema sanaa hiyo huibua hisia mbali na kumpa riziki
Na RICHARD MAOSI
SANAA ya kuchora ni kipaji adimu ambacho kwa asilimia kubwa kimechangia kuwapa vijana ajira; hasa wale wanaopenda na kujivunia kazi za mikono yao.
Kwanza ni muhimu kukuza mchoro wa kile unachokifahamu katika hatua za kwanza, kabla ya kuendea kile kigumu. Ili kufanikisha haya msanii atahitaji jitihada kubwa.
Mchoraji awe tayari kujifunza kutokana na kazi za wenzake waliobobea, awe mwepesi wa kujifundisha na akubali kurekebishwa makosa akielekezwa.
Akilimali ilikutana na mwanachuo shupavu kutoka viungani mwa mji wa Nakuru anayetumia kipaji cha uchoraji kuteka hisia za wanajamii.
Daniel Ogutu, 22 anasema awali hakuona iwapo sanaa ingeweza kumbadilishia mtu maisha, lakini sasa anaamini kuwa kipaji kinalipa.
Baada ya kufuata nyayo za wachoraji maarufu ulimwenguni kama vile Edward Tingatinga wa Tanzania, aliyeanzisha stadi ya kubuni mitambo, Ogutu alijiongezea ujuzi na sasa anatumia uchoraji kujikimu.
Akiwa mwanafuzi wa shule ya upili alipenda kuangika michoro yake ukutani kujifurahisha, lakini sasa amebobea na kuweka bidhaa zake mtandaoni.
Anashangaa jinsi soko lake linavyozidi kutanuka, sio tu nchini bali kimataifa.
“Ninadhani itafika siku Wizara ya Michezo na Masuala ya Vijana, itawekeza katika uchoraji ili baadhi yetu tupate nafasi ya kujinadi pamoja na kuinadi kazi yenyewe kimataifa,” akasema Bw Ogutu.
Akizungumza na Akilimali, alieleza kuwa amejifundisha stadi ya kupaka rangi na kuoanisha hali halisi ya maisha kupitia michoro kama vile umaskini, ufisadi na uhifadhi wa mazingira.
“Pamoja na historia kubwa ya utajiri ulio barani Afrika, lengo langu kubwa ni kugusa na kubadilisha maisha ya waliokata tamaa,” anaongezea.
Akiwa mwanafunzi wa somo la Criminology katika Chuo Kikuu Cha Egerton, anasema sanaa ya uchoraji imemsaidia kulipa karo mbali na kumpatia umaarufu.
Hata hivyo, anaungama kuwa asilimia kubwa ya watu wanaoridhia kazi yake ni wageni, labda kwa sababu bado nchini Kenya watu wengi hawachukulii sanaa kama kazi.
Pia anajaribu kupuzilia mbali dhana potovu ya siku nyingi kuwa kuchora ni kazi inayohusishwa na Wazungu.
Anaona ipo haja kwa wanunuzi kupiga jeki michoro ya humu nchini inayoenda kwa bei nafuu, ikilinganishwa na ile inayonunuliwa Ulaya kwa bei ghali.
Kwa utafiti alioufanya anasema watu wengi wanapenda michoro inayogusa hisia zao moja kwa moja, ndiposa anawaomba chipukizi wajifundishe kuenda na matukio yanayohusu jamii.
Wengi wao siku hizi wanapenda kuchorwa wao wenyewe au mtu wa karibu katika familia ili wahifadhiwe kama kumbukumbu kwa siku za baadaye.
Ogutu anasema uchoraji ni sawa na muziki ambapo mchoraji huwa na mashabiki wengi wanaopenda kazi zake na wangependa kunasibishwa nazo.
Anawashauri wachoraji chipukizi kwanza kuelewa utamaduni wa mtu na mchango wao katika jamii kama vile kilimo, kabla ya kuchukua kalamu na karatasi kuchora.