Makala

AKILIMALI: Nyasi maalum za mifugo zisizoathiriwa na kiangazi

December 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

Hatimaye KARLO (Kenya Agricultural Research and Livestock Organisation) wamekuja na mtindo mwafaka wa kuboresha na kuhifadhi lishe ya mifugo katika maeneo kame hususan Samburu, Garissa na Kajiado.

Lishe hii ambayo ni sampuli ya nyasi (Bracharian na Rhode grass) zinazokuzwa baada ya kipindi fulani na baadaye zikakaushwa katika mazingira yenye joto jingi huanzia kupoteza unyevu ili zipate kudumu bila kuharibika.

Sababu kuu ya taasisi ya KARLO kuanzisha mchakato mzima ilikuwa ni kulenga wakulima wadogo wanaopata changamoto nyingi katika swala la kutafuta malisho ya mifugo msimu wa kiangazi.

Nyasi hizi ambazo asili yake ni nchi ya Brazil zimepenya na kupokelewa vizuri na wakulima nchini.? Akizungumza na Akilimali mtaalam kutoka taasisi ya KARLO Lanet Nelima Rose Nekesa alisema siku hizi gharama ya kupata lishe kwa mifugo imepanda kwa asilimia kubwa.

Wakulima kutoka maeneo yanayoshuhudia kiwango kidogo cha mvua ndio wamekuwa wakiathirika zaidi. Hili limefanya iwe desturi kwao kushuhudia hasara katika sekta ya ufugaji. Anahimiza wakulima kujifunza kutokana na historia ya ukame nchini ili waanzishe mipango ya kujihifadhia lishe kwa siku za usoni.

Nelima anasema kuzalisha lishe ya kutosha ni tatizo sugu ambalo limekuwa likiwakabili wakulima wanaofuga ng’ombe wa maziwa na nyama. Nyasi za kiasili haziwezi kutosheleza mahitaji yote ya mifugo. Ndio sababu uchunguzi wa maabara katika shirika la KARLO kwa ushirikiano na serikali kuu umekuja na Bracharian, nyasi zinazoweza kukomaa haraka, wala hazihathiriki na makali ya kiangazi.

Shamba la KARLO Lanet tasisi ya serikali ambapo nyasi za Rhodes hukuzwa na hatimaye kuvunwa kwa trekta kabla ya kuhifadhiwa. Picha/Richard Maosi

Hukuzwa katika maeneo ambayo mchanga una rutuba ya kutosha na ufaafu wake ni wa hali ya juu. Tayari majaribio yamefanyika katika maeneo ya Marigat na inaonyesha kuwa spishi hii ya nyasi inaweza kufanya vizuri endapo mkulima atazikuza kwa kuzingatia unyunyizaji maji wakati zinapokua.

Nelima anasema kuna aina nyingi ya mimea inayoweza kutumika kama lishe. Nyingi yazo zikiwa ni nyasi za kawaida, punje za mtama, mashina ya migomba na napier grass za kisasa. Baada ya kuvuna nyasi mkulima anaweza akazihifadhi bila kupoteza virutubishi muhimu kwa kuzitengea sehemu maalum. Kwanza mkulima azikaushe katika jua kali au azihifadhi ndani ya kitalu ili ziweze kupoteza unyevu. Joto jingi huharakisha uwezekano wa kukausha Rhode na Brachacharian.

Hata hivyo, Nelima anawashauri wakulima wajitahidi kukausha nyasi zao ndani ya kitalu kwani hazipotezi virutubishi. Pia athari ya bakteria na maradhi mengine huzuilika pakubwa. Aidha, usafi wa kiwango cha juu huwa umezingatiwa.Baadaye lishe hii inaweza ikaongezewa molasses na kuwa bora zaidi kwa ajili ya matumizi.

“Huu ndio ubora tunaozungumzia na husaidia mifugo kusaga chakula kwa urahisi pindi iingiapo kinywani,” Nelima alisema. Nyasi zilizokaushwa ni rahisi kusafirishwa kutoka eneo moja hadi jingine. Harufu nzuri inayotokana na lishe zilizokaushwa huongezea mifugo hamu ya kula. Mkulima anayefuga ng’ombe, mbuzi, nguruwe na kondoo anaweza kuthibitisha hili endapo amekuwa akitumia lishe hizi zilizoongezewa virutubishi.

Tukizungumza na mkulima Solomon Njoroge kutoka eneo la Dundori alisema amekuwa akitumia lishe yenyewe kwa miaka sita sasa baada ya kuhudhuria makongamano ya kilimo katika taasisi ya kilimo na kupata ujuzi.

Alipata mbegu zake zilizohifadhiwa katika pakiti na akazikuza shambani mwake. Anaungama kwamba kukausha nyasi za Rhode na Bracharian kumesaidia wakulima wengi wadogo wanaohofia kiangazi msimu wa joto jingi.

Anasema yeye huvuna nyasi na kuongezea zile alizonunua kutoka kwenye maduka ya mnada kisha akazifanya kuwa matuta ya lishe.