AKILIMALI: Usipuuze ufugaji kondoo, bado bidhaa zake zina pato kubwa
Na RICHARD MAOSI
MKULIMA anapowatunza kondoo vizuri, matokeo yake huwa ni ya kutia moyo. Kwa upande mwingine wanyama wanaweza kuwa washirika wa karibu kwa binadamu.
Katika nchi yetu idadi ya wafugaji wa kondoo imepungua kiasi cha haja, labda ni kwa sababu ya uhaba wa malisho au desturi ya wakulima kupendelea mifugo wengine kama vile mbuzi na ng’ombe.
Miaka ya nyuma idadi ya wafugaji wa kondoo ilikuwa karibu sawa na ile ya wafugaji wa mbuzi lakini sasa mambo yanaelekea kuwa kinyume, kwa sababu wakulima wengi wameelekeza mapenzi yao kwa mifugo wengineo.
Akilimali ilizuri kaunti ya Nyandarua kutangamana na wafugaji waliojikita katika ufugaji wa kondoo. Hili likiwa ni eneo la nyanda za juu lenye baridi kali, spishi za kondoo hapa zikiwa za aina yake.
Aidha ni mchanganyiko wa spishi za asilia na zile za kisasa, ambazo huchukua muda mfupi kukomaa na mahitaji yao si mengi, bora mkulima awe na sehemu ya kuwafugia.
Tulikutana na mkulima Patroba Maranga, mtaalam wa kondoo aliyetufichulia namna ya kufanya kondoo waanze kuzaana baada ya muda mfupi kwa kutumia mchanganyiko wa lishe za kisasa na nyasi.
Alieleza kuwa kondoo wanapenda kula wakiwa pamoja katika makundi, hivyo basi sio jambo la busara kwa mkulima kuwatenganisha endapo ana nia ya kujinufaisha na ufugaji.
1. Mazingira ya kufugia
Patroba anahimiza kuwa sehemu wanamokulia kondoo iwe na nafasi ya kutosha, kuhakikisha kondoo wanaweza kuingia katika malazi yao bila msongamano na kuondoka bila kubana kwenye mlango.
Mkulima afanye juhudi kuhakikisha paa na kuta za banda la kondoo halina mianya itakayoweza kupitisha baridi kali au kuvuja wakati mvua inaponyesha.
“Aidha sehemu yenyewe iwe imeinuka kidogo ili kuzuia maji kutuama,” akasema.
Patroba alitufichulia kuwa ni jambo la msingi kwa mkulima kudumisha usafi wa hali ya juu, kwani hali hii itasaidia kuzuia mkurupuko wa maradhi ya kuwafanya kondoo waanze kukohoa, kuvimba kwato na hata kuvutia vimelea na wadudu ambao ni hatari kwa maisha ya mifugo.
Alisema ni mwafaka kinyesi kuondolewa kila wakati ili kufanikisha mzunguko wa hewa safi saa ishirini na nne kwa siku nzima.
Vilevile Patroba anawakumbusha wakulima kuwa na sehemu mbili za kuwalisha kondoo wake yaani nje na ndani ya malazi yao, akiamini itasaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga ambayo mara nyingi haiwezi kutabirika.
Sehemu ya kulishia iwe safi na aghalabu atumie lishe kavu isiyokuwa na umande, maji ya kunywa yawe safi na jiwe la kulamba mara mojamoja lenye madini ya chumvichumvi ili kuwapatia kondoo hamu ya chakula.
2. Mchanganyiko wa aina ya lishe
Wakati mwingine mkulima anashauriwa kuwaruhusu kondoo wakatafute majani ya miti, mizizi na matawi katika vichaka.
Ni muhimu ikumbukwe kuwa kondoo wanaopatiwa lishe duni, wanaweza kushambuliwa na maradhi ya aina mbalimbali.
Mtaalam huyu anasema uwezo wa kondoo jike kushika ujauzito unategemea kwa asilimia kubwa malisho anayopokea. Ndiposa mkulima anashauriwa ajaribu kuchanganya aina yote ya malaji kama njia ya kuongeza kinga dhidi ya maradhi yanayoweza kuchangiwa kutokana na ukosefu wa lishe bora (wanga, protini na vitamini).
“Kondoo akilishwa vibaya kiwango cha maziwa katika chuchu kinaweza kushuka na kuwafanya wanakondoo kuwa dhaifu,” akasema.
3. Kuwakinga
Kulingana na Patroba ni wazi kuwa kondoo hawaogopi mvua kama mbuzi au ngombe, hii ni kwa sababu miili yao imejaa sufu.
Lakini anatoa tahadhari kuwa mkulima ajaribu kuhakikisha kuwa kondoo wake hawasimami kwenye mvua kwa muda mrefu kwani unyevu mwingi kupita kiasi unaweza kufanya mifugo wake waanze kuugua maradhi ya kuoza kwato za miguu.
Wakati mwingine manyoya katika mwili huanza kuchakaa na kupukutika moja kwa moja endapo ujuzi wa kitaalamu hautazingatiwa.
Patroba anasema ni sharti mkulima awe na ujuzi wa kutambua kuwa kondoo wana minyoo endapo watabugia chakula kingi kupita kiasi cha kawaida.
Jambo linaloweza kuwafanya kondoo wako wasiweze kushambuliwa na maradhi kila wakati, ni kuhakikisha kuwa hawali chakula katika sehemu moja kwa muda mrefu unaoweza kupita wiki mbili.
“Kwa mfano endapo mkulima anamiliki ekari moja ya shamba anaweza kugawanya sehemu hiyo mara nne kisha akawalisha kondoo wake kwa mzunguko,” akaongezea.
Nao kondoo wasiwe wengi katika sehemu ya kula kwani wanapokanyaga malisho yao sana hali hii inaweza kusambaza maradhi ya midomo wanapocheua majani yenyewe usiku.
Kwa kawaida kondoo dume wasiwe wengi kuliko kondoo jike katika kibanda cha kuwafuga kwa kuwa nia ya mkulima ni kuzalisha kondoo wengi baada ya muda mfupi.
Utaratibu wa kuwafuga kondoo unahitaji mtaji mkubwa kuanzisha kwa mfano kila kondoo jike wanne wanaweza kuhudumiwa na dume mmoja.
Lakini cha msingi kondoo jike wanaposhika ujauzito inashauriwa watengewe sehemu ya mbali na kondoo wa kawaida ili kuwakinga dhidi ya usumbufu wa kondoo wengine.