• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
AKILIMALI: Ufugaji ng’ombe haukumpa faida aliyotazamia, akajaribu kuku na sasa hajuti kamwe

AKILIMALI: Ufugaji ng’ombe haukumpa faida aliyotazamia, akajaribu kuku na sasa hajuti kamwe

Na DUNCAN MWERE

KABLA ya kujitosa mzimamzima kwenye ufugaji wa kuku na ndege wa kila aina, alifahamika na wengi kutokana na kufuga ng’ombe.

Baada ya kuwaza na kuwazua alionelea ni heri kilimo cha kuku kingemzolea faida na pesa nyingi kama njugu.

Sasa mkulima Nixon Muchiri ni kati ya wakulima watajika wa kufuga ndege wa aina mbalimbali hususan kuku. Mnamo mwaka wa 2000 Muchiri alianza ufugaji wa nyuni hawa japo walikuwa wachache sana lakini sasa wameongezeka zaidi.

“Nilipogura kilimo cha ng’ombe wa kisasa nilianza kufuga kuku wakati huo wakiwa 50 na miaka kumi na sita baadaye wameongezeka na kufikia 3,000,” aeleza Muchiri katika shamba lake lililo kwenye kitongoji cha Ruthagati, viungani mwa mji wa Karatina eneobunge la Mathira kaunti ya Nyeri. Safari yake katika zaraa hii imekuwa ya milima na mabonde licha ya kupata ufanisi maishani.

Mwaka wa 2010 alibadilisha aina za kuku wa kienyeji na kuwa na wale walioboreshwa chini ya mradi wa Kienyeji improved Chicken Institute unaojulikana kama KARI. Mradi huu ulikuwa na maskani katika mji wa Naivasha alikoagiza vifaranga. Baada ya kufanya vyema alipanua kazi yake na kuagiza vifaranga kutoka jijini Kampala katika taifa jirani la Uganda. Kwa sasa Muchiri aliyeajiri wafanyikazi zaidi ya kumi na mmoja amekuwa akiagiza baadhi ya vifaranga wake kutoka kampuni ya Rainbow Roosters Chicken licha ya kuotamia vifaranga kivyake.

Alidokeza Akilimali kuwa kuku wa aina hii hawakabiliwi na matatizo mengi ikilinganishwa wa kuku aliofuga hapo awali. Hii ikiwa ndio sababu kuu ana wateja chungu nzima.

“ Licha kuwa ninajivunia tuzo la mkulima bora wa kuku katika ukanda wa Mlima Kenya kwenye maonyesho ya kilimo ya Nyeri yaliokamilika juzi katika uwanja wa Kabiruini nina wateja kote nchini,” anasema.

Anawapata wanunuzi haswa kutoka Nairobi, eneo la Bonde la Ufa, Magharibi na Mashariki.

Vile amepata wanunuzi zaidi kupitia mitandao ya kijamii. Aidha amekuwa akitoa huduma hii kwa mahoteli na shule nyingi za eneo hili. Pia wageni hawakosekani katika boma lake na duka lake lililo mjini Karatina linalofahamika Boston Chicken Centre.

Bei ya kuku hutegemea umri kwa mfano kifaranga wa siku moja ni sh 100 huku wa wiki moja ni sh 150 naye wa mwezi mmoja ni sh 300. Kuku wa kike aliyekomaa ni sh 1,000 naye jogoo ni sh 1,500.

Kuhusu bei ya mayai, yai moja hugharimu Sh30 huku ‘tray’ ikigharimu sh 900. Muchiri anaeleza kuwa yeye huuza zaidi ya vifaranga 1000 kila wiki na kuku 300 mia tatu.

Awashauri wafugaji wenzake

Hata hivyo mkulima huyu anawashauri wafugaji wa kuku wawe waangalifu na makini kwani kuku wanahitaji kushughulikiwa kila wakati.

Mojawapo wa mambo ya kimsingi wanahitaji ni kula na kunywa kwa wakati.

Mahitaji mengine ni chanjo ambayo inafaa kutolewa wakati ufaao.

Hitaji jingine kwa viumbe hawa ni usafi. Chumba cha kuku hao kinastahili kunadhifishwa mara mbili kwa siku.

“ Mwaka wa 2013 kuku wangu waliambukizwa ugonjwa wa ‘Gumboro’ na asilimia hamsini wakafa ni hapo nilipata funzo ya kuwachanja kwa wakati,” aeleza Muchiri aliye na mikakati ya kuasisi chuo cha mafunzo ya ukulima.

Muchiri ndiye aliyepewa jukumu la kutoa mafunzo na mawaidha kuhusu ufugaji wa kuku wa kisasa kwenye maonyesho ya kilimo uwanjani Kabiruini kaunti ya Nyeri.

Muchiri huandaa warsha kuhusu kilimo bora cha kuku na ndege wengineo ambapo kila anayepata mafunzo haya hutozwa ada ya Sh500 kwa siku. Kuhusu maswali na mawaidha Muchiri anawaomba walio na maswali kumfikia kwa nambari hizi : 07224-77575 au 0721-336187. Pia yeye amefuga nyuni wengine kama vile Kanga, Bata bukini, Bata mzinga, Bata, Bantans na Silky Chicken.

You can share this post!

Mahakama yakubali Philip Murgor kumtetea Sarah Wairimu...

Ujenzi wa soko la Githurai waanza

adminleo