Makala

Aliyejifungua ndani ya ambulensi msituni Boni, ageuka balozi wa kupigania afya na barabara nzuri

Na KALUME KAZUNGU July 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMKE aliyejifungua mtoto ndani ya ambulensi akikimbizwa hospitalini Lamu miezi saba iliyopita sasa amegeuka kuwa balozi wa kusukuma miundomsingi ya uchukuzi na afya iboreshwe eneo hilo.

Bi Amina Mohamed,19, kutoka kijiji cha Mswakini kilichoko ndani ya msitu wa Boni, mnamo Januari 2 mwaka huu, alilazimika kuzaa mtoto wake ndani ya ambulensi.

Hii ni baada ya gari hilo kumchukua muda mfupi kutoka kijijini kwao kwa minajili ya kumfikisha hospitalini Mokowe kujifungua.

Ikumbukwe kuwa eneo la Mswakini na msitu wa Boni kwa jumla kuna changamoto za tangu jadi, hasa barabara mbaya na ukosefu wa hospitali na zahanati za kuhudumia wagonjwa.

Eneo hilo pia linatambuliwa kutokana na utovu wa usalama unaochangiwa na Al-Shabaab.

Mnamo 2014, hospitali na zahanati zote zaidi ya tano za msitu wa Boni zilifungwa na madaktari na wauguzi kutoroka eneo hilo kwa kuhofia mashambulio kutoka kwa magaidi hao.

Kwa sasa ni zahanati mbili pekee za Kiangwe na Mangai ambazo zinahudumia wakazi japo vituo hivyo vya afya vinakabiliwa na changamoto tele ya uhaba wa dawa na ukosefu wa wahudumu wa kutosha wa afya.

Katika mahojiano na Taifa Leo juma hili, Bi Mohamed alisema aliafikia kuhubiri umuhimu wa miundomsingi ya afya na uchukuzi, hasa barabara kuboreshwa na hospitali na zahanati kujengwa, kutokana na kile kilichomkumba Januari mwaka huu.

“Kwetu hakuna vituo vya afya karibu nasi. Uchungu wa kuzaa ulipowadia sikujua la kufanya. Niligaagaa bila matumaini. Namshukuru dadangu Bi Habiba Ali kwani alipigia kituo cha majanga mjini Mokowe ambacho kilileta ambulensi na wahudumu wa afya walionibeba kunikimbiza hospitalini,” akasema Bi Mohamed.

Aliongeza, “Barabara mbaya ilisababisha ambulensi kufika kijijini Mswakini kuchelewa. Isitoshe, waliponibeba walilazimika kuendesha gari pole pole kutokana na barabara mbovu. Barabara yetu ina mashimo, matope na vidimbwi vya maji kila mahali. Ndio sababu mtoto alianza kutoka tumboni hata kabla nifike hospitalini. Nawashukuru wahudumu waliokuwemo ndani kwa kunisaidia. Nilijifungua salama.”

Bi Mohamed alisisitiza haja ya serikali kujenga vituo vya afya kwenye vijiji vyote vya msitu wa Boni ili kuwawezesha wakazi kupata pa kukimbilia wakati majanga au dharura inapotokea.

“Nitazidi kuirai serikali ijenge hospitali na kuzikarabati barabara zetu. Kukiwa na miundomsingi hiyo, maisha yatakuwa rahisi,” akasema Bi Mohamed.

Jumatano, Meneja wa Majanga na Uokozi, Kaunti ya Lamu, Bw Shee Kupi aliongoza kikosi cha kituo cha majanga (EOC) kutoka Mokowe, ambapo walimtembelea mama huyo na mtoto kijijini kwao Mswakini, ndani ya msitu mkuu wa Boni katika harakati za kutathmini hali yao.

Kikosi cha kituo cha majanga kikiongozwa na Meneja wao,Shee Kupi (Wa tatu kutoka kushoto) wakati walipomtembelea mama huyo kijijini Mswakini ndani ya msitu Wa Boni. Picha| Kalume Kazungu

“Tunafanya hayo yote ili kuona kwamba wale wanaosaidiwa na kituo chetu wanatiwa moyo na kujenga imani zaidi kuhusiana na huduma zitolewazo kituoni,” akasema Bw Kupi.