ANA KWA ANA: 'Baiskeli ina faida tele kipindi hiki cha janga la Covid-19'
Na WANGU KANURI
KIPINDI hiki cha janga la Covid-19 watu wengi wanakabiliwa na matatizo mbalimbali kuanzia kwa changamoto za kifedha hadi kwa msongo wa mawazo.
Watu wengi wameshauriwa kukaa nyumbani kuepuka misongamano katika maeneo ya umma ambayo inaweza ikachangia pakubwa kuenea kwa ugonjwa huu. Lakini kufanya mazoezi kama ya uendeshaji baiskeli yumkini kunaweza kukamsaidia mtu. Hapa tumezungumza na kijana ambaye amegeuza baiskeli kifaa cha muhimu si tu kwa usafiri, lakini kwa mazoezi ya kusaidia kuimarisha afya na viungo.
Tueleze kwa kifupi kukuhusu
KIOKO: Maurice Kioko ni kifungua-mimba katika familia ya Bi Joyce Kioko. Nina umri wa miaka 30 na ninafanya kazi katika Chuo Kikuu cha Daystar nikiwa msajili wa kitaaluma.
Ulianza kuendesha baiskeli lini na ni nini kilikuchochea?
KIOKO: Nilianza kuzingatia sana kuendesha baiskeli Aprili 2020 baada ya Wizara ya Afya kuweka masharti na kanuni kuzuia watu kutangamana na wengine kiholela kwa lengo la kupunguza na hata kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19. Ilinibidi nitafute njia mbadala ya kujifurahisha na kwa hivyo nikaanza kuendesha baiskeli.
Unajivunia nini kutokana na kuendesha baiskeli?
KIOKO: Kuendesha baiskeli kumenifanya nifurahishwe na mandhari yaliyoko nchini Kenya. Isitoshe, nimeweza kupiga tizi hivyo basi kuimarisha mwili wangu kimaumbile na kiafya.
Je, mtu anapaswa kula chakula gani akiendesha baiskeli?
KIOKO: Unapoendesha baiskeli hufai kuwa umekula chakula kupita kiasi lakini unapaswa kula vitafunio vinavyokupa nguvu kwa haraka.
Je, mtu anapaswa kujiandaa vipi kabla ya kuendesha baiskeli?
KIOKO: Mwendeshaji baiskeli anapaswa kuvalia jezi, glavu, helmeti na viatu vinavyofaa. Pia anapaswa kuhakikisha kuwa magurudumu yana pumzi ya kutosha, breki zinafinyika na taa za baiskeli zinawaka.
Uendeshaji wa baiskeli umekuvunia marafiki wa aina gani?
KIOKO: Kupitia kuendesha baiskeli, nimeweza kutangamana na wenzangu niliosoma nao miaka iliyopita katika Chuo Kikuu cha Daystar na nimejiunga na vikundi vya waendeshaji baiskeli.
Kwa kuwa barabara nyingi za Kenya hazijatengenezwa kukidhi waendeshaji baiskeli, unajihisi vipi kutokana na suala hili?
KIOKO: Si haki kwa waendeshaji wa baiskeli kwani hamna kitengo chao barabarani licha ya kwamba wao ni miongoni mwa wanaotumia barabara. Kwa hivyo ninairai Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini (KenHA) kujenga barabara kwa kuzingatia waendeshaji baiskeli sio tu kwa wanaotembea kwa miguu na wenye magari.
Kuendesha baiskeli katika barabara za Kenya ni sawa na kujichimbia kaburi kwa kuwa huheshimiwi na wenye magari, je wewe huzingatia nini unapoendesha?
KIOKO: Ndio; kuna baadhi ya madereva wasiowaheshimu watumizi wengine wa barabara na kuna wale huwaheshimu. Kwa hivyo, wewe kama mwendeshaji baiskeli inakulazimu uwe makini zaidi barabarani. Kama hujajasirika katika kuendesha baiskeli kwenye barabara kuu ambapo pana msongamano wa magari, tumia sehemu ya barabara iliyotengewa wanaotembea kwa miguu lakini jihadhari kutokana na kitu chochote kinachoweza kuifanya baiskeli kupata pancha.
Wewe umeweza kuendesha baiskeli kwa umbali wa kilomita ngapi na uliutumia muda wa saa ngapi?
KIOKO: Umbali ambao nimeweza kuendesha baiskeli tangu Aprili ni kilomita 178 na kwa kadri muda wa saa nane.
Uendeshaji baiskeli ni spoti ambayo haijavuma nchini Kenya. Je, unafikiri ni nini Wizara ya Michezo na Turathi za Kitaifa inaweza kufanya ili umaarufu wake ujulikane?
KIOKO: Wizara inaweza kuanzisha miradi ya waendeshaji basikeli kwa kuwa na mashindano miongoni mwao na kuwatuza. Hii itawapa wengi moyo wa kujiunga na spoti hiyo.
Ushauri wako kwa vijana ni upi?
KIOKO: Ninawashauri vijana wajitose katika uendeshaji baiskeli na wajivunie spoti hiyo kwani licha ya kuwa njia murua ya kuwasaidia kufanya mazoezi, inawapa fursa nzuri ya kutalii na kuangalia mandhari yaliyoko nchini Kenya pasi na gharama.