• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
ANA KWA ANA: Stori yake ni kama telenovela

ANA KWA ANA: Stori yake ni kama telenovela

Na THOMAS MATIKO

KWENYE tuzo za injili za Groove Awards 2019 zilizofanyika mwezi uliopita, jina la msanii Revival lilikuwepo kwenye kitengo cha ‘Msanii wa Mwaka Chipukizi wa Kiume’.

Hakufanikiwa kushinda tuzo hiyo na ilimwendea Baraka Musiq. Lakini japo hakushinda, hatua hiyo ya kuhusishwa kwenye hafla hiyo iliishia kumsaidia kukutana tena na familia yake aliyokuwa ametengana nayo mwongo mmoja uliopita. Safu hii ilipiga naye stori.

Hebu tuanzie mwanzo

Revival: Mimi ni Manoah Nandunga, nilizaliwa Mumias kwa familia ya watoto watatu; dada mkubwa Terry Nandunga, mimi na kitinda mimba kaka yetu Antony Nandunga. Mama alifariki mwaka 1992 nikiwa na umri wa miaka mitatu. Ndugu zangu pia walikuwa wachanga kwa sababu tumeachana kwa mwaka mmoja na miwili katika usanjari huo. Miaka miwili baadaye naye baba yetu akafariki dunia.

Pole sana kwa misiba hiyo ya mfululizo?

Revival: (Machozi yakimlenga). Asante. Wazazi wangu walifariki kwa ugonjwa wa Ukimwi. Tulikuwa wachanga sana ila picha kamili tulipata ukubwani. Babangu alikuwa mwanamuziki wa kitamaduni, na mlevi wa bia na wanawake na ndivyo alivyoishia kuupata ugonjwa huo kisha akaja kumwambukiza mama.

Kilichofuata ni nini?

Revival: Baada ya wazazi kuaga tulikwenda kuishi na babu pamoja na bibi. Wao nao wakafariki 1998 na kutuacha mayatima. Hapo jamii ikawa haina jinsi ila kutuchukua. Tukagawanywa, dadangu akaenda kuishi na shangazi mmoja kule Mumias, kakangu akachukuliwa na mwingine kule kule Mumias, nami nikaishia Kitale kwa shangazi mwingine.

Endelea

Revival: Yalikuwa ni maisha magumu sana, hatukuruhusiswa kukutana. Tulibahatika kutangamana tu wakati wa hafla za mazishi.

Mbona ikawa hivyo?

Revival: Mwanzo kabisa baada ya kifo cha wazazi wetu kutokana na Ukimwi, tulitengwa. Kukawa na unyanyapaa dhidi yetu kutoka kwa wana jamii. Lakini pia wajomba zetu hawakutaka turithi kipande cha ardhi kilichostahili kumwendea baba kutoka kwa babu.

Mlistahimili vipi magumu hayo?

Revival: Hatukuwa na jinsi ila kufanya watakavyo. Baada yetu kumaliza kidato, kila mmoja wetu aliambiwa aondoke ajitafutie maisha. Tukaungana na kuamua kuomba urithi wa baba. Hapo ndipo tulifukuzwa na wajomba waliokuwa tayari wameshagawana kipande chake. Mmoja wao alituelezea kwamba hatukuwa wanafamilia kwa sababu baba yetu alikuwa ni mtoto wa kambo.

Baada yenu kufukuzwa?

Revival: Tulihamia mji mdogo uitwao Lukoye na kukodisha ‘kanyumba’ kadogo. Dada yetu akawa ndiye mlezi. Alikuwa mama mboga na ndio kazi aliyofanya kutulisha. Baada ya mwaka mmoja Disemba, 2009 niliyachoka maisha yale. Nikaamua kusafiri Nairobi kuja kukimbizana na maisha yangu ya muziki. Ndugu zangu hawakupenda ila nikawa kichwa kigumu. Dadangu alinitafutia Sh800 za nauli na ndivyo nilivyotia mguu Nairobi na kuishia mtaa wa Kayole na sikurudi nyumbani kwa kipindi cha miaka 10.

Mbona hukujitahidi angalau kwenda kuwacheki baada ya muda?

Revival: Maisha mjini hayakuwa mepesi kwangu. Nilibahatika kuajiriwa na muuza mboga aliyekuwa akinilipa Sh100 kila siku. Alichonipa ni chakula tu ila malazi nikawa najipanga mwenyewe. Kwa maisha hayo ningewezaje kurudi nyumbani? Kisha usisahau kilichokuwa kimenileta mjini ni kusaka maisha kupitia muziki ili niweze kuwasaidia.

Kwa hali hiyo mawazo ya kufanya muziki bado ulikuwa nayo?

Revival: Ndio tena kabisa. Sema sikuwa na ufahamu wa wapi pa kuanzia ila siku moja nikiwa kwenye kibarua akatokea mshikaji mmoja niliyesoma naye Kidato aitwaye Milton Bulimu. Alikuwa ni mwalimu. Ndiye aliyenitoa kwenye mahame yale na nikaanza kuishi naye huku nikiendelea kufanya kibarua changu. Ni kupitia koneksheni zake ndipo niliishia kukutana na Ulopa Ngoma, aliyenisaidia kurekodi nyimbo kadhaa bure baada ya kumpa stori yangu.

Ndiye aliyerekodi ‘Tena na Tena’ iliyokupelekea kuteuliwa kwenye tuzo za Groove?

Revival: Hapana! Baada ya kurekodi kazi kadhaa naye na kuona hazilipi kama nilivyokuwa nikitarajia, niliachana na muziki na kurudi kufanya vibarua, safari hii nikiwa mwosha magari. Ni kwenye pilka pilka hizo ndipo nilikutana na Muhubiri Paul Williams na baada ya kumwelezea ndoto yangu akanitia motisha. Baada ya kususia muziki kwa muda, nilirudi studio mwaka jana na kurekodi Tena na Tena na produsa Bizzy B. Paul ndiye aliyenigharimia kila kitu. Wimbo huo ndio uliishia kuniweka kwenye chati za Groove. Japo sikushinda, nashukuru ilinisaidia kuniunganisha tena na familia yangu.

Mlikutana vipi?

Revival: Miaka yote hiyo bila mawasiliano yoyote, ndugu zangu walidhania nilikuwa tayari nishafariki dunia. Wakawa wamekata tamaa. Ila wajua tuzo za Groove zilipoanza kulikuwa na shamrashamra kibao na mwenyewe nikabahatika kufanyiwa mahojiano kadhaa. Sasa nikiwa kwenye mahojiano na runinga ya NTV kwenye kipindi cha Crossover 101, kwa bahati kakangu alikuwa akitizama na ndipo aliniona. Mwisho wa mahojiano nilipeana akaunti zangu za mitandao ya kijamii na ndivyo alivyoweza kunifikia na nikakutana nao.

You can share this post!

KIKOLEZO: Walivyoacha mashabiki hoi

Punda nchini wapungua kwa viwango vya kutisha – ripoti

adminleo