Anaokoa ndizi kwa kuchakata kripsi
KWA muda mrefu wakulima wanaotegemea mazao mabichi ya shambani wamekuwa wakihangaishwa na mabroka na mawakala, suala ambalo linatatiza azma ya kusaidia serikali kuangazia kero ya njaa na upungufu wa chakula.
Hilo, si tofauti na Seraphin Wanjiku, mkulima kutoka Kaunti ya Kirinyaga, ambaye amekuwa akikuza ndizi kwa zaidi ya miaka 10.
Sawa na wakulima wengi wa mashamba madogo nchini, safari yake haijakosa kushuhudia changamoto za mabroka. Ndizi ni zao linaloharbika upesi hivyo basi wanaozizalisha wanapaswa kuwa wamejipanga ipasavyo kukweka hasara ya kuoza.
Wanjiku hulima ndizi ya mapshi, maarufu kama Mkono wa Tembo kwa Kiingereza plantain bananas, eneo la Kerugoya, Kirinyaga. Anakumbuka mwaka 2023 alipopoteza mazao ya thamani ya maelfu ya pesa kwa kukosa wanunuzi.

Anasema soko lilikuwa mbaya kiasi kuwa mazao yake yaliharibika. “Kila mwezi nilikuwa napokea mavuno mengi, na mwaka 2023 mambo hayakuwa mazur vile,” Wanjiku anaelezea.
Kulingana naye, kila baada ya wiki mbili alikuwa akivuna kilo 150 za ndizi hivyo kwa mwezi alikuwa akigonga kilo 300. Awali, anasimulia kuwa mkungu wa kilo 10 za ndizi ulikuwa ukinunuliwa Sh100 ila bei ilishuka hadii Sh30.
“Kupata Sh300 kwa mkungu mzima ni hasara kubwa,” anasema, akikumbuka jinsi alivyopoteza mazao. Changamoto zake zinaakisi taswira ya wakulima wengi wa mazao mabichi Kenya, ambapo ukosefu wa miundomsingi kama vile majokofu ni kero kubwa.

Wanaishia kukadiria hasara bin hasara, licha ya mchango wao mkuu kwenye mtandao wa uzalishaji chakula nchini. Wizara ya Kilimo inakadiria kuwa karibu asilimia 30 ya mazao hupotea wakati na baada ya mavuno.
Wanjiku, kwenye mahojiano na Akilimali alisema hasara aliyopata ilimshawishi kuwaza kwa undani. “Nilikuwa nikiona kripsi zikiundwa kutokana na ndizi na viazimbatata, na ni mwanya nilioamua kuzamia,” akasimulia.
Bila mafunzo yoyote yale, akiongozwa na mtaji mdogo aliokuwa nao, alitumia vifaa vya jikoni kutekeleza hilo. “Nilianza na kifaa cha kukatakata karoti kuwa vipande vidogo, kuunda kripsi za ndizi,” akasema.

Kuzikaanga, alidokeza kwamba alitumia mafuta ya kawaida kupika na sufuria kwa minajili ya shughuli hiyo. Jaribio la kwanza, anasema lilifanikiwa. “Nilitengeneza pakiti 10 za gramu 200 na kuuza kila moja Sh200,” anasema.
Kiwango hicho iwapo angeuza kikiwa mazao mabichi kingemletea Sh200 pekee, lakini kripsi zilimpa Sh2, 000. Hapo ndipo safari ya uundaji vitafunwa hivyo ilipoanza. Miaka miwili baadaye, biashara yake imekua na kupanuka.
Aidha, kando na kuchakata kripsi za ndizi, Wanjiku pia huunda, unga wa ndizi uliochanganywa na ule wa mahindi, unga wa uji uliochanganywa na mtama na wimbi.

Aliambia Akilimali kuwa huchakata kilo 50 za ndizi kwa wakati mmoja, kilo moja ya kripsi akiuza Sh400. Masoko yake ni pamoja na Kaunti ya Kirinyaga, Embu, Nairobi, Nyeri na Nakuru, hasa baada ya bidhaa zake kuthibitishwa na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS).
Kutoka ekari moja ya ndizi, Wanjiku sasa anakuza matunda hayo kwenye ekari mbili.
Isitoshe, biashara yake sasa imeajiri wafanyakazi wanne wanaomtegemea kujiendeleza kimaisha. Akikadiria kila ekari kumpa kilo 300 kwa mwezi, anasema kiwango hicho hakitoshi kukithi mahitaji ya masoko aliyopenyeza.
“Nina kandarasi na wakulima 10, ambapo mmoja hunisambazia kilo 200 kila baada ya majuma mawili na waliosalia kati ya kilo 30 hadi 50 kila mmoja,” anadokeza. Kwa kila kilo huwalipa baina ya Sh50 hadi Sh100.

Mjasiriamali huyu alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara walioshiriki Maonyesho ya Kibiashara ya Wawekezaji Wadogo na wa Kati Ukanda wa Afrika Mashariki 2025, ndiyo East African Community (EAC) Micro, Small and Medium Enterprises (MSMEs) Trade Fair, yaliyofanyika kuanzia Novemba 7 hadi 16 Uhuru Gardens, Nairobi.
Kaulimbiu ya Makala hayo ya 25 ilikuwa “25 Years of EAC Integration: Advancing Innovation and Regional Value Chains for Competitive MSMEs towards Sustainable Development,” na Wanjiku alikiri kupata jukwaa kuvumisha bidhaa zake nje ya Kenya.