Makala

ANN NJOROGE: Filamu Kenya ina malipo duni lakini usife moyo

February 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA JOHN KIMWERE

‘MTAKA cha mvunguni sharti ainame.’ Ndivyo wahenga walivyologa na tangia zama zile ndivyo hali ilivyo hadi sasa. Ni msemo ambao umeonekana kuwa na mashiko kwa kiwango fulani miongoni mwa jamii.

Pia unaonekana unaendelea kudhihirishwa na kina dada wengi tu ambao wameamua kujituma mithili ya mchwa kwenye masuala tofauti katika harakati za kusaka riziki.

Miongoni mwao ni binti Ann Mugure Njoroge anayepania kuibuka kati ya waigizaji mahiri nchini miaka ijayo.

Msichana huyu ni mwigizaji anayeibukia ambaye ndio yupo mwaka wa kwanza anakosomea kuhitimu kwa shahada ya digrii katika masuala ya uigizaji kwenye chuo kikuu cha Multimedia (MMU).

”Kusema kweli tangu nikiwa mdogo nilitamani kuhitimu kuwa mwana habari, hata hivyo nakumbuka nilianza kushiriki maigizo kanisani kipindi hicho nilikuwa na umri wa miaka sita,” anasema Mugure na kuongeza kuwa analenga kutimiza ndoto ya kuwa kati wasanii hodari duniani.

Kadhalika anadokeza kuwa anapenda sana kufanya kazi kama mpiga picha za filamu.

Katika mpango mzima chipukizi huyu anasema analenga zaidi kushiriki uigizaji na kufanikiwa kufikia upeo wa kimataifa huku akifuata nyayo zake, Rita Dominic mzawa wa Nigeria.

Msanii huyo ambaye hushiriki filamu za Nollywood anajivunia kutwaa tuzo kibao katika maigizo. Katika shindano la ‘Africa Movie Academy mwaka 2012 alinasa tuzo ya mwigizaji bora.

Kadhalika Rita anajivunia kushiriki filamu kochokocho ikiwamo ‘Finding Mercy,’ ‘White Waters,’ ‘The Meeting’ na ‘Iyore’ kati ya zingine. Tukiachia hayo pia anasema anatamani kumfikia Lupita Nyong’o anayetesa katika filamu za Hollywood.

Msichana huyu ameshiriki kazi nyingi tu tangu ajiunge na tasnia ya filamu. Chipukizi huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa na kupata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga mbalimbali ikiwamo KUTV na Inooro TV.

Amefanya kazi na makundi tofauti ikiwamo Classic Fix Media, Samspine Production na Blood Moon kati ya zingine.

Anashauri wenzake watie bidii ili kuonyesha talanta zao katika masuala ya maigizo. Anataka mashirika yanayomiliki vyombo vya habari nchini kuanzisha vipindi zaidi kupeperusha filamu na muvi za humu nchini kusudi kuwapa ajira wasanii chipukizi.

Anasema kando na changamoto zingine sekta ya maigizo nchini ina malipo duni hali ambayo hufanya baadhi yao kusepa na kusaka ajira tofauti.

”Kusema kweli malipo duni ama kutolipwa kabisa hufanya baadhi ya waigizaji chipukizi kuvunjika moyo na kuzipigia chini shughuli za maigizo,” alisema.

Hata hivyo anashauri wenzake kutovunjika moyo upesi licha ya kukutana na pandashuka nyingi katika tasnia ya uigizaji.