Makala

Asake avunja kimya kuhusu kifo cha shabiki

Na WINNIE ONYANDO December 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWIMBAJI wa Nigeria Ahmed Ololadelisten almaarufu Asake hatimaye amevunja kimya kuhusu kifo cha shabiki kwenye tamasha lake Nairobi katika uwanja wa Nyayo mnamo Jumamosi Desemba 20, 2025.

Karen Lojore, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Daystar, anaripotiwa kuzimia wakati wa msongamano na mkanyagano kwenye ukumbi huo.

Alikimbizwa hospitali, ambapo alitangazwa kuwa amefariki.

Tukio hilo la kusikitisha limelaaniwa na Wakenya, ambao wanadai haki kwa Karen.

Kufuatia tukio hilo la ksikitisha, Asake alitoa taarifa Jumatatu Desemba 22, 2025 usiku, akiifariji familia ya Karen.

“Moyo wangu unaomboleza na familia, marafiki, na wapendwa wa Karen Lojore, na ninaahidi kuunga mkono na kufanya niwezavyo kuelewa kilichotokea. Waliohusika wanapaswa kuwajibika,” Asake alisema.

Mwanamuziki huyo mashuhuri alionyesha kusikitishwa na tukio hilo, akisema, “Muziki daima umekuwa njia yangu ya kushiriki upendo na furaha, na inavunja moyo wangu kwamba hilo lilitendeka.”

Kwa upande mwingine, waliosimamia hafla hiyo, Tukutane Entertainment, walizungumzia kero za wananchi siku mbili baada ya tukio hilo la kutisha.

Katika taarifa ya Jumatatu usiku, waandalizi walisema kuwa watashirikiana kikamilifu na huduma za dharura na mamlaka husika kuelewa kilichotokea.”

Tukutane Entertainment iliongeza kuwa usalama wa washiriki wao wa tamasha ni suala ambalo “wanalichukulia kwa uzito mkubwa”.

“Kwa heshima ya familia na uchunguzi unaoendelea, tumejitolea kukabiliana na hali hii kwa uangalifu, uwazi na uwajibikaji, na tutashiriki maelezo ya ziada kadri inavyofaa na kwa uratibu na mamlaka husika,” mratibu wa tukio aliongeza.