Makala

ATM ya kutema sodo inavyosaidia kupunguza mimba za utotoni

September 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Mtambo unaojiendesha maarufu ATM inayotumika kusambaza sodo imechangia kupunguza mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi, katika mtaa wa Dandora jijini Nairobi. 

Kulingana na mwalimu wa shule ya Upili ya Wasichana Dandora Bi Juliet Chelangat, kufikia sasa hajarekodi kisa cha mwanafunzi aliye na mimba ikilinganishwa na mwaka jana (2023).

 “Wakati kama huu, tulikuwa visa saba vya wanafunzi waliokuwa na mimba za mapema ila sasa hatuna. Mashine hii imesaidia shule kurekodi idadi ya juu ya wanafunzi wanaohudhuria masomo,” alieleza Bi Chelang’at.

Mashine hiyo inawahudumia wanafunzi zaidi ya 1000. Kulingana na Bi Chelang’at, baadhi ya wasichana waliacha shule kutokana na kujihusisha na mahusiano na watu walioamini wangeshughulikia hitaji lao la sodo.

“Kuna wale wasichana waliacha shule mwaka jana, ili kutafuta sodo. Pia, tulikuwa tukishughulikia masuala mengi ya mahusiano, uavyaji mimba, na kutoa mwongozo kwa wale ambao ni wazazi,” alidokeza Bi Chelang’at.

Umaskini wa sodo

Kulingana na Shirika la Kitaifa la Takwimu nchini, zaidi ya Wakenya milioni 25 wanaishi na umaskini, familia nyingi zikishindwa kutatua tatizo la hedhi pamoja na chakula.

Utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya wanafunzi milioni moja hukosa kuhudhuria shule katika ya siku tatu au nne kila mwezi.

Wanjiku mwenye umri wa miaka 17 katika Kidato cha tatu, aliambia Taifa Dijitali, alipata ujauzito wa mapema baada ya kujihusisha na ngono kutafuta pesa za kununua sodo kila mwezi ili kusalia shuleni. Hapo ndipo alipata ujauzito.

“Ukiishi kwenye mtaa, jua umaskini upo. Iwapo ningepata mashini hii mapema, singekuwa mzazi. Sitamani ndugu zangu kujipata katika hali hii. Kila mwezi tunapata sodo 16 hivyo huwa ninahakikisha pia nimechukua kwa niaba yao,” alisema Wanjiku.

Pia, alieleza jinsi ya kusalia shuleni iwapo hana sodo.

“Nikiwa shuleni, kila baada ya saa mbili nilikimbia msalani kuosha mavazi,” alieleza.

Mwanafunzi mwingine, 16, alisema kila wakati alimwambia mamake kuwa ni mgonjwa ili kuepuka aibu.

“Nakumbuka nikiwa kidato cha kwanza kuna wakati sikuenda shuleni kwa kukosa sodo. Nilimdanganya mama kuwa mimi ni mgonjwa. Nilihisi nikija shuleni wenzangu watanicheka,” alisema.

Mfadhili wa mashine hiyo Bi Alphine Juma, kutoka kundi la Sanaa Group, anasema wana uwezo wa kumfadhili msichana mmoja sodo 16 kila mwezi.

Wanaonufaika ni wasichana na wanawake waliosajiliwa ambao hutumia kadi iliyo na nambari maalum.

 “Takwimu za mashine hii ambayo hutumia WiFi, ili kutoa na kunakili, inaonyesha ni wasichana wenye umri wa miaka 16-24 ambao hutumia zaidi. Wakati wa jioni wanapoenda nyumbani ndio wakati ambao wengi huchukua,” alisema Bi Juma.

Bi Juma alilaumu viongozi wa kike kukosa kutafuta suluhu ya bei nafuu ya sodo hasaa kwa familia maskini.