Atunga wimbo wa mahadhi ya Kihindi kuangazia corona
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
WENYE hamu ya nyimbo za mahadhi ya Kihindi wanaendelea kuusikiliza wimbo uliozinduliwa siku chache zilizopita na mwimbaji Nassir Mohamed Abdalla unaoangazia janga la corona.
Wimbo huo kwa jina la ‘Corona’ na ambao ameigiza mahadhi na muziki kutoka wimbo wa Kihindi wa ‘Tere Naam’, Abdalla almaarufu Brother Nassir, anawasihi watu wafuate maagizo yanayotolewa ya kuwaokoa wasikumbwe na janga hilo.
“Namshukuru Mola kwa kuuwezesha wimbo wangu huu nilioimba mara mbili na ambao umewavutia watu 33,000 na 14,000 katika YouTube kufikia sasa, kiwango ambacho kinalingana na nyimbo zingine maarufu katika Bara Afrika,” anasema Nassir.
Anafahamisha kuwa katika kibao chake hicho, ameeleza kuwa corona imeanzia China na sasa iko dunia nzima hivyo anamwomba Mungu awaepushe waja na janga hilo lisiendelee kuwaadhibu.
“Nimemuomba Mungu atusamehe kwa maovu tunayotenda ya kumuasi yeye na kutuepushia janga hili la corona ambalo limeshapoteza maisha ya wengi. Nimemuomba Mungu atuhifadhi na kutuokoa lisiendelee kutuadhibu,” anasimulia.
Nassir kati ya wasia aliotoa katika wimbo huo ni kuwaomba watu wawe wakisafisha mikono kila mara na kutosahau kutumia sabuni.
Pia sehemu moja ya utungo katika wimbo huo inasema: “Tusitoke tubaki karantini, tuswali Ilahi tuMuogopeni, ya Mannani Rahamani, tusaidie ya Rabbana!”.
Mwimbaji huyo anaamini kuwa amefikisha ujumbe huo muhimu kwa wale wanaopenda muziki na amefurahikia kuwa ujumbe wake umeanza kuenezwa kwenye magari ya matatu, tuk tuk na majumbani.
“Tuko katika hatari ya janga la corona hivyo nimeona nina wajibu mkubwa wa kutuma ujumbe ambao nina hakika umewafikia wengi na utazidi kuwafikia wengine ili uweze kukabilika ipasavyo na utoweke na maisha yapate kuendelee kama kawaida,” akasema Nassir.
Kwa mwimbaji huyo anasema ni mwiko kuimba nyimbo kwa kutumia lugha ambao ni kinyume na maadili ya Kiafrika.
Brother Nassir analaumu wasanii wenye kupendelea kuimba nyimbo zao kwa kutumia maneno ambayo kwa kawaida hayafai kutumika kwani ni kinyume na maadili na utamaduni wa Kiafrika.
Brother Nassir anasema kuna umuhimu kwa waimbaji wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini na kanda ya Afrika Mashariki kutumia maneno ama mashairi mazuri ambayo yatakuwa yenye kusikilizwa na watu wa umri wowote wakiwemo watoto wadogo.
“Kuna uhimu kwetu sisi wanamuziki na watunzi kutumia lugha yenye maneno mazuri yasiyopotosha jamii. Kwa wasanii wenye fikra kuwa wanapotumia maneno ya upotofu ndio wanapata umaarufu wa haraka, mawaomba waache tabia hiyo kwani ni kinyume na maadili yetu,” anasema msanii huyo.
Brother Nassir anasema kuna maneno ama mashairi waimbaji hawafai kuyatumia ni yale ambayo watoto huyashika haraka na wakaimba mbele za wazazi wao bila ya kufahamu kuwa maneno hayo wanayoyatumia huwa ni ya kukosa heshima.
Kwake anasema hupendelea kuimba nyimbo kwa kutumia maneno ambayo hata watoto wanapoyatumia maneno yaliyomo, huwa si ya ukosefu wa adabu.
Hayo ni pamoja na maneno ya mapenzi ambayo mwimbaji anaweza kuyatumia na yakawa hayana madhara hata kama yataimbwa na watoto.
Mwimbaji huyo huimba nyimbo za mahadhi ya Kihindi, kizamani, za kizazi kipya pamoja na tungo za Qasida.
Kuhusu lawama kwa kutumia midundo katika tungo zake hasa zile za Qasida, Brother Nassir anasema anawaheshimu wale wanaomkosoa lakini akafahamisha kuwa kila mtu ana mtizamo wake na anavyoamini kwake lipi la sawa ama la makosa.
“Kwangu, najua nini ninachokifanya kwani naamini utungo wa wimbo unakuwa haramu kwa sababu ya ujumbe ulioko kwenye kazi hiyo. Ikiwa ujumbe wa wimbo wowote una mafunzo ndani yake, nawaomba wanaopinga, wachukulie ujumbe na wasahau midundo,” anasema.