Makala

AUNTY POLLY: Ana mimba na siko tayari kuitwa ‘baba’

April 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

NINA mpenzi wangu ambaye ameniambia kuwa ana mimba. Ninaashuku sana iwapo mimba hii ni yangu kwani awali alikuwa amenifichulia kwamba kwa kawaida hedhi yake haiji kila mwezi, na mara ya mwisho kabla ya kushiriki tendo lenyewe la kukidhi haja za kimwili naye, mwezi huo hakuwa ameshuhudia hedhi. Nimeshikwa na hofu kwani siko tayari kuitwa baba. Je, inawezekana kwa msichana kushika mimba licha ya kutoshuhudia hedhi kila mwezi?

John, 18, Mombasa

Kulingana na wataalamu wa masuala ya uzazi, wakati wowote msichana ambaye amewahi kushuhudia hedhi anaposhiriki ngono bila kinga, anaweza kushika mimba. Unapaswa kujua kuwa msichana ambaye hashuhudii hedhi kama kawaida bado anatoa mayai na hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kushika mimba. Wasichana wote hasa wasioshuhudia hedhi kama kawaida wanaweza kutoa mayai wakati tofauti, na hivyo kufanya iwe rahisi kutambua wakati upi ambapo ana uwezekano mkubwa wa kushika mimba. Hedhi zisizokuja kulingana na ratiba aidha hufanya iwe vigumu kwa msichana kutambua iwapo ameshika mimba. Zaidi ya yote unapaswa kujua kwamba unaposhiriki tendo la ndoa bila kinga kuna hatari zingine mbali na msichana kushika mimba. Hatari hizo ni pamoja na maradhi ya zinaa kama vile kisonono, kaswende na hata Ukimwi.

 

Hivi majuzi rafiki yangu alinifichulia kwamba anashuku kuwa ameambukizwa maradhi ya zinaa. Cha kushangaza ni kuwa anasisitiza kwamba hakushiriki tendo la ndoa na mhusika anayedaiwa kumuambukiza. Anasema kwamba kuwa huenda aliambukizwa kupitia busu. Kuna uwezekano wa maradhi ya zinaa kusambazwa kupitia njia hii?

Jane, 17, Nairobi

Kulingana na wataalamu wa kiafya, naam waweza kuambukizwa maradhi ya zinaa kwa kumbusu mtu. Kwa mfano unaweza kuambukizwa maradhi ya herpes kwa kumbusu mtu mdomoni. Pia, licha ya kuwa wataalamu wa kiafya wanaamini kuwa uwezekano wa kuambukizwa virusi vya HIV kwa kubusiana mdomoni ni finyu, ikiwa wahusika wana majeraha au kidonda katika sehemu hii kuna uwezekano mkubwa wa maambukizi kutokea. Kumbuka kuwa maradhi ya zinaa yaweza kuambukizwa kwa njia zozote za ngono hata mgusano wa sehemu nyeti. Kwa hivyo ikiwa ni lazima mtu ushiriki tendo la ndoa basi lazima asisitize matumizi ya kinga.