Makala

AUNTY POLLY…: Anihonga nifungue kisima, nifanyeje?

July 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA fleti ninamoishi kuna kijana fulani wa kiume ambaye amekuwa akinifuata kwa miezi kadha sasa huku akitaka niwe katika uhusiano naye. Nilikubali ambapo lazima nikiri kwamba kwa muda mambo yalikuwa mazuri. Hata hivyo, juma lililopita alianza kunipa zawadi na pesa huku akinisihi tuanze kushiriki mapenzi. Ningependa kujua ninachopaswa kufanya kijana wa kiume akijaribu kunihonga ili nishiriki naye mapenzi.

Everlyne, 17, Nairobi

Hongo ni mbinu ya kukufanya ushiriki ngono hata ikiwa hutaki. Katika hali yoyote ile, haya ni makosa. Hasa kwa upande wako, haujahitimu umri wa utu uzima na hivyo anachojaribu kufanya ni hatia hasa ikiwa amekuzidi kiumri.

Kuna wakati ambapo mhusika anaweza kuonekana kana kwamba ni mkarimu kwa kukupa zawadi au usaidizi bila kukuitisha chochote. Unapaswa kuwa mwangalifu kwani huenda anakuandaa ili katika siku za usoni akikuomba, basi hautakuwa na budi ila kumpa.

Hongo yaweza kuwa pesa au vitu vingine vya matumizi au kukufurahisha. Unapaswa kujua kwamba iwapo mwenzako amekuzidi umri hasa ikiwa haujahitimu miaka 18, anachofanya ni kinyume na sheria.

Kila unapopokea zawadi au pesa kutoka kwa mtu hasa ikiwa hujamuomba, hupaswi kuchukua kwani kuna uwezekano kwamba ataanza ‘kukudai’.

Kwa sasa ningekushauri uzungumze na mtu mkomavu unayemuamini kuhusiana na suala hili. Yaweza kuwa mzazi wako, mwalimu shuleni au mshauri nasaha.

Zungumza kuhusu hongo hiyo na uombe usaidizi. Huenda ukapata kitu unachohitaji kutoka kwa mmoja wa hawa watu niliokutajia.

Pia, huyo anayekushurutisha mshiriki mahaba atakanywa na kukomeshwa. Kumbuka ungali mdogo kiumri na endapo utaanza kujihusisha na masuala ya mapenzi, unajiweka kwenye hatari ya kushika mimba au ukaambukizwa maradhi ya zinaa.