Makala

AUNTY POLLY: Mama anibebesha mzigo wake, nisaidie

March 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PAULINE ONGAJI

KWA miaka sasa nimekuwa nahisi kana kwamba mama yangu amenitwika majukumu yake kama mzazi. Kila siku baada ya kurejea nyumbani kutoka shuleni napata ameniachia kazi zote ikiwa ni pamoja na kusafisha nyumba, vyombo na kuwashughulikia ndugu zangu wadogo. Naelewa kwamba ana mzigo mkubwa wa kutulea bila baba lakini suala hili linaathiri masomo yangu hasa ikizingatiwa kwamba sina wakati wa kusoma na kufanya kazi zangu za ziada. Nifanyeje?

Lynn, 17, Mombasa

Unapaswa kumuelewa mama yako. Huenda sio kupenda kwake kukuachia majukumu haya na pengine hata hatambui kwamba anakukwaza na kuathiri masomo yako. Katika muktadha wa Kiafrika, watoto wanapaswa kuwasadia wazazi wao kufanya kazi za nyumbani, lakini haimaanishi kwamba sasa huu unapaswa kuwa mzigo wako. Ndiposa unapaswa kuzungumza naye kuhusu hisia zako. Umezungumza naye kuhusu jinsi ambavyo kazi hizi zinahujumu masomo yako? Hata hivyo, wakati unafanya hivyo, jaribu kumuelewa mamako. Huenda amezidiwa na majukumu ya kinyumbani hasa ikizingatiwa kwamba anawalea bila mzazi mwenzake. Pia, itakuwa vyema ikiwa utaimarisha mazungumzo na uhusiano baina yenu ili kila unapokwazika, unazungumza naye badala ya kulalamika.

 

Kwa miaka kadha nimehisi kana kwamba mamangu amekuwa akinidhulumu kiakili na sasa nimeamua kwamba nimechoka na nataka kuhama lakini sidhani kisheria naruhusiwa kufanya hivyo. Naomba usaidizi.

Kenfrey, 16, Nairobi

Kwanza kabisa pongezi kwa kujitokeza na kuzungumzia suala hili. Sio rahisi unapohisi kudhulumiwa na mtu unayemuamini kama mzazi. Hata hivyo, itakuwa vyema kwanza kueleza ni mambo gani hasa ambayo anakutendea yanyokufanya udhani kwamba anakudhulumu kiakili. Je, ni jambo ambalo linahatarisha afya na usalama wako? Wajua kuna wakati mwingine ambapo mzazi anaweza kukuadhibu pasipo kujua kwamba anakudhulumu. Umejaribu kumzungumzia kuhusu hisia zako? Ikiwa unaogopa kumwambia unayopitia, tafadhali zungumza na mtu mkomavu uliye na uhusiano wa karibu naye ili aweze kuzungumza kwa niaba yako.