Makala

AUNTY POLLY…: Mbona navamiwa na chunusi usoni?

March 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KWA miezi kadha sasa uso wangu umekuwa ukifunikwa na chunusi kiasi cha kuvutia macho ya watu kila ninapotembea, suala linaloudhi sana. Ningependa kujua kwa nini nakumbwa na chunusi?

Nimo, 16, Mombasa

Ningependa kukufahamisha kwamba ukiwa katika umri wa kubalehe ni kawaida kukumbwa na chunusi kwani hii inaashiria kwamba unazidi kukomaa. Vijana wengi wakiwa katika umri huu hutatizika na suala hili kiasi cha kupoteza ujasiri wa kuzungumza na watu. Japo mara nyingi ni vigumu kukabiliana na tatizo hili kuna mbinu ambazo waweza kutumia kuzipunguza au kuzuia. Ili kupunguza chunusi, nawa uso angalau mara mbili kwa siku kwa kutumia sabuni na maji yaliyopashwa moto. Koma kugusagusa uso wako kwani unapofanya hivi unatatiza ngozi na vinyweleo. Jaribu kutumia ‘cleanser’ kila wakati. Punguza matumizi ya vipodozi lakini ikiwa lazima uvitumie nunua vya ubora wa hali ya juu. Unapotumia mafuta ya nywele, hakikisha kwamba hazigusani na uso wako.

 

Naomboleza kifo cha dada yangu aliyefariki miezi miwili iliyopita lakini kinachoudhi kabisa ni kwamba katika familia yetu yote, ni kana kwamba ni mimi pekee ninayeomboleza. Naona wazazi na ndugu zangu wamerejelea shughuli zao za kawaida ilhali mimi nimeshindwa kabisa kumakinika ambapo kila mara najipata nikilia. Naomba ushauri.

Karis, 19, Nairobi

Kwanza kabisa nakupa pole kwa kifo cha dada yako. Bila shaka miezi miwili ni michache sana kumsahau mtu. Lakini pia ningependa kukujulisha kwamba watu huwa na mbinu tofauti za kuomboleza. Kuna baadhi ya watu wanaoamua kuendelea na maisha yao ya kawaida baada ya kifo, suala linalowafanya waonekane kana kwamba hawajaguswa na mkasa huo, ilhali kuna baadhi wanaozidi kuhuzunika kwa muda mrefu. Unapaswa kufahamu kuwa ni kawaida na vyema kuomboleza, lakini pia sharti maisha yaendelee. Chukua muda wako kuangazia kumbukumbu ya dadako lakini usiache hisia hizi zitawale maisha yako kwani kifo ni kitu ambacho hauwezi kubadilisha na wakati mmoja itakulazimu uendelee na maisha. Ningependa kukushauri upate mawaidha kutoka kwa mshauri nasaha kufahamu mbinu za kukabiliana na hisia zako wakati huu.