AUNTY POLLY: Mimi na mamangu hatupatani, nisaidie
Na PAULINE ONGAJI
UHUSIANO kati yangu na mamangu umekuwa ukididimia kila kuchao. Kwa muda sasa umekuwa ukizidi kuwa mbaya na chochote ninachofanya kutatua shida hii hakionekani kuzaa matunda. Nakiri kwamba awali nilikuwa na kiburi na tabia zangu hazikuwa zinafurahisha. Lakini hii ilikuwa kutokana na sababu kwamba nikiwa shuleni nilikuwa nadhulumiwa na wanafunzi wenzangu kutokana na uzani wangu, kauli ambayo pia mamangu aliizidisha kwa kunitusi. Hata hivyo bidii yangu ya kutaka kumuonyesha kwamba nimebadilika imekuwa ikikumbana na shutuma na ukosoaji wake. Nahitaji usaidizi.
Clara, 18, Nairobi
Kwanza kabisa pokea pole zangu kwa yale unayokumbana nayo. Ni vigumu sana kurejelea hali yako kihisia baada ya kudhulumiwa, hasa ikiwa mmoja wa wanaozidisha uchungu huu ni mzazi wako.
Ni jukumu la mamako kusimama nawe na kukupa moyo maishani licha ya hali yako kimwili, kihisia na kimawazo.
Je umejaribu kumwambia kwamba haufurahii matusi yake? Tafadhali fanya hivyo na ikiwa waona ni ngumu tafuta mtu mkomavu unayemuamini umtumie kumfikishia mamako ujumbe huu.
Zaidi ya yote kuwa na subira na mamako kwani kama ulivyosema kuna wakati ambapo tabia zako hazikufurahisha, na huenda bado hajaamini kwamba umebadilika.
Zidi kufanya wema na kumuonyesha kwamba unawajibika, na baada ya muda hatakuwa na budi ila kukubali kwamba kwa kweli umerekebika.
Kwa miezi kadha sasa wazazi wangu wamekuwa wakipigana na kurushiana matusi huku kila mara wakitishana kwamba watatalikiana. Ni jambo ambalo limeniathiri mimi na dadangu kiasi cha kwamba kila mara tuna wasi wasi, na hata tumeanza kurudi nyuma kimasomo. Tufanyeje?
Charlie, 17, Mombasa
Pole sana kwa yale ambayo wewe na dadako mnapitia. Ni makosa kwa wazazi kutusiana na kupigana mbele ya watoto. Ikiwa haya yanafanyika ni dhihirisho kwamba uhusiano wao sio mzuri kwenu.
Huwa ngumu kwa watoto, wazazi wanapokosana na kutalikiana lakini wewe na dadako mnapaswa kuelewa kwamba wakati mwingine ni vyema kwao kuwa mbali.
Hii haimaanishi kwamba watakoma kuwa wazazi wenu kwani upendo utasalia kuwa huo huo.
Nasema hivi kuwaandaa endapo wawili hao wataishia kutalikiana.
Huo hautakuwa mwisho wa maisha na watazidi kuwapenda kama watoto wao.
Ni rahisi kwa watoto kukasirika wazazi wao wanapoamua kuachana lakini unapaswa kuelewa kwamba wakati mwingine uhusiano ukiwa mbaya basi ni vyema utakatizwe.