AUNTY POLLY: Ninawashwa baada ya kunyoa sehemu nyeti
Na PAULINE ONGAJI
MIMI ni mvulana mwenye umri wa miaka 16. Kwa miaka michache sasa nimeshuhudia nywele za sehemu zangu za nyeti zikiota. Nimekuwa nikizipuuza lakini hivi majuzi nilizinyoa na cha kushangaza ni kwamba kwa siku kadha sasa nimekumbwa na mwasho katika sehemu hii. Naomba uhauri.
Japheth, 16, Eldoret
Kuna mambo mengi yanayosababisha mwasho baada ya kunyoa nywele hasa za nyeti. Mojawapo ya mambo makuu ni ukavu kwenye ngozi unaponyoa. Ukavu huu unamaanisha kunyoa nywele hizi bila maji na sabuni, krimu ya kunyoa au jeli. Pia yaweza kuwa unatumia kifaa kikuu au kisicho na ukali wa kutosha. Aidha, tatizo hili laweza tokea ukinyoa nywele hizi kwa kutumia mwelekeo ambao nywele zinaota. Lakini pia, yaweza kuwa ni kutokana na maambukizi katika sehemu hii, kumaanisha kwamba unapaswa kutafuta ushauri wa kimatibabu. Kuhusu masuala niliyotaja awali, kabla ya kujinyoa hakikisha umeoga kwa maji moto. Unapofanya hivyo hakikisha aidha unatumia jeli maalum ya kunyoa vile vile ujipake krimu (after shave) baada ya kunyoa. Lakini kabla ya kununua bidhaa hizi hakikisha kwamba huna mzio (allergy) wowote. Na kuzuia maambukizi, hakikisha unatumia vifaa safi katika shughuli hii.
Mimi ni msichana wa shule moja ya upili eneo la Pwani. Rafiki yangu wa karibu wa kike shuleni alifichua kwamba ana virusi vya HIV, ambapo inasemekana kwamba alizaliwa navyo. Je, ninapaswa kumaliza uhusiano huu?
Aggy, 19, Mombasa
Bila shaka la! Virusi vya HIV havisambazwi kupitia urafiki na hiyo ni hali tu ya kiafya. Haimzuii mwenzako kuendelea na maisha ya kawaida. Haitakuwa vyema kumtenga mwenzako kutokana na hali yake ya kiafya. Huo utakuwa ni unyanyapaa. Kwanza, huu ndio wakati wa kumuonyesha upendo hata zaidi. Virusi vya HIV hupitishwa kupitia ngono, au kupitia damu unapotumia kwa pamoja vifaa kama wembe, kisu, mswaki na sindano, miongoni mwa mambo mengine. Uhusiano wa kirafiki haukuweki katika hatari yoyote ila tu mnapaswa kuwa waangalifu mnapotumia vifaa vilivyotajwa hapo juu.