Makala

AWINO: Magavana waache unafiki katika sheria mpya ya kilimo

October 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AG Awino

Nilizungumza kwa mapana na marefu na aliyekuwa mwakilishi wa wakulima kwenye Bodi ya Sukari Bw Okoth Obado kuhusu maoni yake juu ya miswada mipya kuhusu kuvunjiliwa mbali kwa Halmashauri ya Kilimo (AFA).

Bw Obado ambaye pia ni Gavana wa Migori kabla ya kuwa Gavana alikuwa mwakilishi wa wakulima kwenye Bodi ya Sukari. Alinipa historia ya kuundwa kwa AFA.

Kwa wakati huo na kabla ya 2013, alisema, aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Dkt Sally Kosgei ndiye aliasisi mpangilio wa kubuniwa kwa AFA. Hatimaye mwenzake Felix Kosgei alihimitisha safari Dkt Sally alikuwa ameanzisha.

Bw Obado aidha alikumbuka kwamba walipinga kubuniwa kwa AFA kwa sababu walihofu nia ya wakuu hawa.

Kwa mtazamo wake, kutokana na hali ilivyo nchini, kila mmea unastahili kuwa na bodi yake binafsi kutokana na mahitaji tofauti ya mimea hiyo.

Kwa hivyo, licha ya Waziri wa Kilimo, Bw Munya kupendekeza kubuniwa kwa bodi mpya ambazo zitaangalia masuala aina tofauti ya mimea hiyo, ingekuwa bora kama kila mmea ingebuniwa bodi yake badala ya kuunganisha. Kwa mfano mikonge na mimea mingine itakuwa chini ya usimamizi wa bodi moja.

Hata hivyo, kabla sheria hizi kuanza kazi, magavana wakiongozwa na Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo katika Baraza la Magavana, sasa wameanza kupinga mapendekezo katika sheria mpya wakidai kwamba sheria haikufuatwa.

Ingawa Bw Njuki haswa anapinga mabadiliko yaliyokusudiwa katika sekta ya chai, madai yake yalinikumbusha kisa kimoja nilichoshuhudia mjini Mombasa mnamo mwaka wa 2016 kwenye mkutano ulioandaliwa na Tume ya Ubinafshishaji.

Lengo la kongamano hilo lililoandaliwa kwenye hoteli ya Kifahari ya Travellers, lilikuwa kuwaeleza magavana kuhusu mikakati ambayo ilikuwa imewekwa katika kutafuta wawekezaji katika sukari.

Baadhi ya waliohudhuria walikuwa: hayati Nderitu Gachagua ambaye kwa wakati huo alikuwa Gavana wa Nyeri, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, kaimu Waziri wa Kilimo kwa Wakati huo Aden Mohamed ambaye pia alikuwa Waziri wa Viwanda.

Ubishi na vuta nikuvute ulipoanza miongoni mwa wanasisasa hao ambao walikataa mapendekezo ya tume hiyo, Bw Oparanya alichipuka ghafla na kuhutubia wanahabari nje ya jumba la mkutano akisisistiza ya kwamba hakukubaliana na maafikiano yaliyokuwa yameafikiwa kwenye mkutano huo.

Kwa ghadhabu, Bw Aden alimwangalia Oparanya kwa uso na kumuuliza: “Wakati wa kupendekezwa kwa mikakati ya kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo, wewe ndiye ulikuwa Waziri wa Mipango ya Kitaifa na ulipitisha mapendekezo ya kuinua sekta ya kilimo, imekuwaje leo unakataa mapendekezo ambayo uliyatia saini wewe mwenyewe?”

Imekuwa desturi katika nchi hii kwamba iwapo hupendi jambo au mikakati yoyote inayopendekezwa, jambo la kwanza ni kukimbia mahakamani ili kusitisha kabisa maendeleo yoyote katika hoja husika. Wanajua kwamba mambo hayaendi kwa kasi korti za humu nchini.

Unafiki wa kutumia sheria kukwamiza mabadiliko wafaa kukoma kwani ni ishara tu ya jinsi wanavyojijali wao wenyewe wala siyo wananchi.

Bw Awino ni mwanamawasiliano anayeandika kuhusu maswala ya kilimo

[email protected]