Habida Moloney: Nilitumia Sh500,000 kwa tiba ya koo kurejesha sauti
NA SINDA MATIKO
MWANAMUZIKI Habida Moloney kafichua kuwa operesheni ya koo aliyofanyiwa mwezi Februari nchini India kuondoa uvimbe kwenye koromeo lake ilimdona kiasi kisichopungua Sh500,000.
Februari, staa huyo alisafiri hadi nchini India kwa ajili ya operesheni hiyo spesheli anayosema bila hiyo, alikuwa amepoteza tayari uwezo wake wa kuimba kabisa.
Tayari amepona kiasi cha kuweza kuzungumza vyema lakini bado hajaweza kuimba.
“Sababu ya kwenda India ni kutokana na ushauri niliopata kutoka kwa daktari Mkenya. Kwa sababu ilikuwa ni operesheni spesheli, nilishauriwa kwenda kukutana na daktari ambaye sio tu mpasuaji wa koo lakini anayeshughulika na upasuaji wa kurekebisha kodi za sauti,” Habida akasema.
Upasuaji huo uliogharimu saa nzima, ulimwacha Habida akiwa hawezi kuongea kwa siku saba.
“Teknolojia ya kisasa ilitumika ambapo uikuwa ni upasuaji uliotumia miale ya laser. Gharama zake hazikupungua Sh500,000 ukiachia mbali tiketi ya ndege na gharama za hotelini,” anasema.
Kwa sasa Habida anaendelea na mazoezi ya kujifunza kujua kuimba tena.