Bambika

Sisemi bei ya saa, sipo tayari kwenda nyumbani- Jalang’o

Na FRIDAH OKACHI July 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANASIASA nchini huenda wanaepuka kutangaza bei ya mavazi au mapambo hadharani baada ya wananchi kulalamikia viongozi wengi kushindwa kutekeleza majukumu yao wakidai ni majivuno wanayoonyesha.

Mbunge wa Lang’ata Bw Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o alikwepa kujibu swali alilokabiliwa na mwanahabari akilenga kujua bei ya saa yake mkononi.

Mbunge huyo alidinda kutaja bei ya saa yake akidai huenda akafutwa kazi.

Hata hivyo Jalango aliweza kubainisha kuwa bei ya pambo alilovalia ni la kawaida tu bila kutaja bei yake.

“Unataka nifukuzwe kazi? Hii saa, si ya bei ghali sana bali kiasi tu,” alisema Jalang’o.

Mbunge huyo wa ODM alitania kuwa huenda pambo hilo alinunua miaka 10 au 30 iliyopita kabla ya kuwa mbunge.

Mbunge huyo anafahamika kuvalia saa ya zaidi ya Sh10 milioni.

Mwaka wa 2019, alichapisha kupewa zawadi ya saa ya Sh12 milioni na dadake. Pia, kabla ya kuondoka kwenye fani ya utangazaji mwaka 2020, alitangaza kupewa zawadi nyingine ya saa iliyo na thamani ya Sh3 milioni kutoka kwa mtangazaji mwenza.

“Huyu rafiki yangu hata baada ya kuacha kazi huwa ananitembelea nyumbani nami namtembelea. Alitumia Sh3 milioni kama zawadi ya siku ya kuzaliwa. Ni saa ambayo alinunua Amerika lakini kuangalia bei, nilitamani angenipa hizo pesa,” alisema Jalang’o (2021).

Wakenya wengi wamekuwa na ghadhabu kutokana na maisha ghali ambayo viongozi wamekuwa wakionyesha katika mitandao ya kijamii, kwa kuhisi kuwa wanawaringia na pesa za mtoa ushuru.

Hali hiyo ilizua mzozo baina ya wananchi wanaoishi katika maisha duni na viongozi wanaoonyesha mitindo mbalimbali ya mavazi.

Wiki mbili zilizopita, aliyekuwa Waziri wa Barabara na Uchukuzi, Bw Kipchumba Murkomen alikuwa miongoni mwa waliopoteza kazi baada ya Rais Ruto kulivunja baraza lote la mawaziri.

Wengi walionekana kufurahia mitandaoni kuhusu Bw Murkomen kufukuzwa kazi kwa kile walidai kwamba alikuwa akionyesha saa na suti ghali anazomiliki katika mtindo ambao haukuwafurahisha.

Kabla ya baraza la mawaziri kuvunjwa, Bw Murkomen alikiri kwamba anamiliki saa ya Sh900,000,  kiatu cha Sh70,000 na mshipi wa Sh50,000.