• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:27 AM
Wenye saluni wajitetea ‘umbea’ wao si wa kubomoa familia

Wenye saluni wajitetea ‘umbea’ wao si wa kubomoa familia

NA WANDERI KAMAU

WAFANYAKAZI katika saluni wamejitokeza kujitetea dhidi ya madai ya baadhi ya wanaume kwamba gumzo linalopigwa wanawake wakitengenezwa nywele zao, kuna na aina nyingine ya urembo, huwafurisha vichwa na kukataa kuwaheshimu waume wao.

Hii ni baada ya wanaume wengi kuanza kuwaletea wake wao wasusi pale nyumbani badala ya kwenda kusukwa nywele zao katika saluni.

Wanaume ambao wameanza kuchukua hatua hiyo waliambia Taifa Leo kwamba mabibi wengi wanapotoshwa kimaadili na umbea ambao huwa unaendeshwa katika saluni.

Wanaume kadhaa waliozungumza na Taifa Leo katika eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu, walidai saluni zinaendelea kuwa majukwaa ya kuwapotosha wake kimaadili.

Mmoja wa wanaume ambaye amechukua hatua hiyo ya kuletea mke wake msusi pale nyumbani ni Bw James Gathemia.

Mkewe Bw Gathemia alijifungua mtoto mdogo miezi mitatu iliyopita.

Ingawa mtoto huyo amekua na kufikia kiwango ambacho anaweza kuachwa kwa saa kadhaa mikononi mwa mtu mwingine kando na mamake, Bw Gathemia anasema ameamua kumzuia mkewe kimakusudi kwenda kusukwa nje.

“Mke wangu hajaonyesha makucha lakini ninachukua tahadhari kwa sababu nimegundua wanawake wengi huanza kuwa wakaidi wanapobuni uraibu wa kuenda katika saluni,” akasema Bw Gathemia.

Ingawa hivyo, alisema anampa mkewe uhuru wake.

“Siwezi kumzuia mke wangu kuenda kusukwa kwenye saluni.  Hata hivyo, mijadala na umbea ambao huwa unaendeshwa katika maduka hayo umekuwa ukiwapotosha na kuwatia sumu, hasa kuhusu umuhimu wa kuwaheshimu waume wao,” akaeleza.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw John Mwangi, aliyesema mijadala mingi ambayo imekuwa ikiendelea katika saluni nyingi, ni kuhusu jinsi wanawake wanavyoweza kuendesha maisha yao bila kuwategemea waume wao, yaani kuwa ‘Miss Independents’.

“Ukisikiliza mijadala mingi ambayo imekuwa ikiendelea kwenye saluni nyingi, wanawake wengi wamekuwa wakishajiishana kuhusu namna ya kujiendeleza kimaisha bila kuwategemea wanaume. Binafsi, sipingi mijadala hiyo, ila inafaa kwa wanawake wasio kwenye ndoa. Ni kwa sababu hiyo ambapo, kando na mke wangu, nimewazuia mabinti wangu wawili dhidi ya kwenda saluni. Nina msusi maalum ambaye huja nyumbani ili kuwasuka,” akasema Bw Mwangi.

Hata hivyo, wasusi waliozungumza na Taifa Leo walipinga vikali dhana hizo, wakizitaja kuenezwa na wanaume wenye misimamo na itijadi za kizamani za taasubi ya kiume.

Walisema kwa kawaida saluni huwa majukwaa ya kijamii, ambapo wao hutangamana na wateja, kwa kujadili masuala tofauti yanayoihusu jamii.

Walisema ijapokuwa mijadala hiyo imekuwa ikiendelea, hilo halimaanishi hivyo ndivyo wamekuwa wakiwashauri wanawake kufanya.

Kulingana na Bi Janice Muli, ambaye ni mmiliki wa duka la ususi, mazungumzo yao mengi huwa ni ya kupitisha muda, na huwa yanarejelea masuala yanayoendelea katika jamii.

Anasema kuwa mwanamke yeyote anayechukulia masuala hayo kwa uzito anafaa kujilaumu mwenyewe.

“Sifa ya mtu hulingana na tabia au mienendo yake. Mtu mpotovu atafanya maovu hata bila kuwa mteja katika maduka haya. Hivyo, wanaume wanaotulaumu kwa madai ya kuwaharibu wanawake wao wanatukosea. Mtu mwovu ni mwovu, hata apelekewe msusi nyumbani kwake. Wanaume wanafaa kuwapa uhuru wanawake wao bila kuogopa lolote. Hivyo ndivyo watawajibika zaidi,” akasema Bi Muli.

  • Tags

You can share this post!

Kikwazo kipya kwa safari ya Raila AUC

Mchapishaji vitabu maarufu, Henry Chakava aaga dunia

T L