BENSON MATHEKA: Chanzo cha mgomo wa madaktari ni mapuuza
Na BENSON MATHEKA
Kwa miezi minane madaktari wanaogoma wamekuwa wakizungumza na serikali kuhusu maslahi yao hasa msimu huu wa janga la corona.
Ingawa maafisa wa serikali wamewalaumu kwa kususia kazi, ni muhimu Wakenya waelewe chanzo cha mzozo huo.
Madaktari walitoa ilani ya mgomo mazungumzo yalipokosa kuzaa matunda lakini wakaahirisha kwa siku 21 wabunge walipoashiria kuwapatanisha na serikali. Masaibu yao yaliwagusa baadhi ya wabunge waliowasikiliza hadi wakamwaga machozi.
Hata hivyo, kwa maafisa wa wizara ya afya na viongozi wanaopaswa kutatua mzozo huo, masaibu ambayo wahudumu hao wa afya wanapitia sio suala la kuwashtua.
Hii inadhihirishwa na kauli ya waziri wa afya Mutahi Kagwe kwamba wanaogoma wanafaa kufutwa kazi na wengine wapya kuajiriwa.Kwa waziri na viongozi wanaowakosoa kwa kuchukua hatua hiyo, suluhu ya mzozo huo ni kuwafuta kazi wahudumu hao kwa kukataa kufanya kazi.
Inasikitisha kwamba maafisa wa serikali hawashtushwi na vifo vya madaktari na wauguzi wanaoambukizwa corona wakiwa kazini kiasi cha kuwaambia sio wao wanaokufa peke yao.Inasikitisha kwamba serikali inashindwa kutatua mzozo huo ikijua kwamba ni Wakenya masikini watakaoumia kwa kukosa huduma za afya.
Badala ya kushughulikia malalamishi ya wahudumu wa afya, serikali ilianza zoezi la uhusiano mwema kwa kuwamiminia sifa katika kujitolea kwao kukabiliana na janga la corona kufanya watu kuamini ilikuwa inawajali.
Bw Kagwe alikuwa akikariri kwamba serikali imewapa wahudumu wa afya vifaa vya kujikinga dhidi ya corona, hadi ubora wa vifaa hivyo ulipotiliwa shaka walipoanza kuambukizwa virusi hivyo wakiwa kazini.
Mojawapo ya matakwa ya wahudumu hao ni kupatiwa vifaa bora za kujikinga na kusema kweli, wana haki ya kufanya hivyo.Kama wanavyosema viongozi wa vyama vya kutetea maslahi yao, kuhudumia wagonjwa bila vifaa bora vya kujikinga ni sawa na kujitia kitanzi.
Kwa maafisa wa serikali na viongozi wanaowakosoa, hili sio muhimu japo inahitaji nia njema tu na matumizi mazuri ya pesa kuwatimizia takwa hili.Tumeona serikali ikitoa pesa za kufadhili masuala na miradi mingine na kwa hivyo, ukosefu wa pesa haufai kuwa sababu ya kupuuza matakwa ya madaktari.
Pili, madaktari wanataka bima ya afya ili waweze kumudu gharama ya matibabu. Katika vikao vya kamati ya bunge kuhusu afya, ilibainika kuwa wizara ya afya ilirudisha pesa zilizotengewa mpango huo huku madaktari wakiendelea kuteseka.
Badala ya kuwakosoa na kutisha kuwafuta kazi, wizara inafaa kuwaomba msamaha kwa kukosa kutimiza takwa hili na kuwafanya wahangaike wakiugua.
Inasikitisha kuwa Bw Kagwe aliagiza serikali za kaunti kuwafuta kazi wahudumu wanaogoma ilhali anafahamu kwamba serikali hizo hazijapata pesa kutoka kwa serikali ya kitaifa kwa muda wa miezi mitatu sasa.
Hii inaonyesha kuwa serikali inakosa kutatua mzozo huo maksudi na kwa sababu inajua athari zake, inachotaka ni kuwatesa Wakenya wanaotegemea hospitali za umma kwa huduma za afya. Madaktari hawafai kulaumiwa kwa kugoma, ni serikali inayofaa kubeba lawama kwa kutojali maslahi ya raia wake.