• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 3:42 PM
BIASHARA MASHINANI: Kilimo cha sukumawiki na nyanya chamfaa mkulima

BIASHARA MASHINANI: Kilimo cha sukumawiki na nyanya chamfaa mkulima

Na SAMUEL BAYA

UKIFIKA katika kijiji cha Ruiru-Solai, kuelekea Nyakinyua, Kaunti ya Nakuru, utaona kipande cha ekari moja na nusu ambacho kimejaa mboga aina ya sukumawiki.

Kipande hicho cha shamba kinapakana na bwawa la Nyalu ambalo lilijengwa na serikali kuu kuwezesha wakazi wa eneo hilo kuendeleza kilimo cha kunyunyuzia mashamba maji.

Ni katika shamba hili ambapo mkulima Maina Karethi amekuwa akiendeleza kilimo cha sukumawiki na kuendeleza maisha yake.

Kisha umbali wa kilomita moja mbele, mkulima huyu anamiliki robo tatu ya ekari ambapo amelima na kukuza nyanya, mboga hizo vilevile zikiendelea kumletea faida tele.

“Kilimo kinalipa sana, mara nyingi hata kuliko kazi ya kuajiriwa na ndio maana unaniona ninaamka na kushinda katika mashamba haya yangu,” hiyo ndiyo iliyokuwa kauli yake ya kwanza tulipomhoji kuhusu azma yake ya kuingilia ukulima wakati vijana wengi wanasukumana mijini kutafuta kazi.

Kwenye mahojiano na Akilimali, Bw Kareithi alisema kuwa alianza shughuli za kilimo baada ya kuacha masomo akiwa katika kidato cha tatu.

Sababu za yeye kuacha masomo alisema ni ari ya kufanya ukulima, hivyo kukosa muda mwafaka wa kuzingatia masomo darasani.

“Niko na miaka 22 na nilianza mambo ya ukulima mwaka wa 2013 na kilimo kimenifaidi kwa sababu nimenunua ploti na hata kujenga nyumba ya kudumu. Vilevile nimefaulu hata kuanzisha kampuni yangu. Ninapanda sukumawiki na nyanya ambazo zinaniletea faida tele siku hizi,” akasema.

Alisema wakati fulani akizunguka katika eneo la Solai alikutana na shamba moja ambalo lilikuwa limejaa mboga na alipojaribu kuuliza ndipo aligundua kwamba biashara hiyo inalipa.

Bw Kareithi alisema kuwa sukuma huvunwa mara moja kwa wiki na kwa wiki moja, huvuna mboga za kiasi cha Sh20,000 na hilo humpa faida tele.

“Sisi huwa tunavuna mboga kila wiki na tunapovuna, huwa tunapata magunia 20 ya kilo hamsini na tunapouza, inatuletea pesa nzuri,” akasema Maina.

Alisema kuwa kwa sasa yuko na miaka minne katika biashara hiyo ya kulima mboga na amefaulu kuajiri vijana wenzake watatu ambao wanafanya kazi katika mashamba yake.

“Kuna vijana ambao nimeajiri na hiyo pia ni njia mojawapo ya kuleta ajira nchini,” akasema.

Aliambia Akilimali kuwa wateja wake wengi ni wakazi wa mitaa ya Banita, Majani Mingi na Maramu.

“Pia kuna wakazi ambao hufika kutoka mtaani kununua hii mboga,” akasema Bw Maina.

Hata hivyo alisema kuwa kuna changamoto ambayo inamsukuma zaidi ikiwa ni wadudu ambao huvamia mboga zake.

“Kuna wadudu ambao wametuvamia na kuuma na kuozesha baadhi ya mboga na hivyo kutupatia hasara. Tumejaribu kuwawekea dawa ili waangamie lakini bado wanaendelea kutusumbua. Hii ni mojawapo ya changamoto ambazo zinatukabili,” akasema Bw Kareithi.

Na ili kuhakikisha kwamba shughuli zake za ukulima hazifeli, kijana huyu ambaye ni wa sita na kitinda mimba katika familia yao aliamua kununua mashini ya kupiga maji kutoka bwawa la maji la Nyalu hadi katika mashamba yake mawili.

“Kazi yoyote ile lazima uwe unaipenda ndipo utakapoweza kuifanya kwa ustadi zaidi. Niliamua kununua mashini hii ya kupiga maji kwa Sh140, 000 na imenisaidia sana tangu wakati huo. Serikali ilipotujengea bwawa hili, lengo lilikuwa ni kuwasaidia wakulima wanyunyizie mashamba yao maji na hilo ndilo ambalo ninafanya kwa sasa,” akasema Bw Kareithi.

Baada ya kuangalia ukulima wake katika shamba analokuza sukumawiki, kijana huyu alitupeleka hadi katika shamba lake la nyanya ambako huko pia ameuza nyanya na kujipatia fedha nyingi.

Katika shamba lake la nyanya, tuliona baadhi ya nyanya ambazo ziko tayari kutundwa na kupelekwa sokoni. Analima ekari moja ya nyanya na hajutii kwa vile biashara hiyo inalipa vyema.

“Nilianza kulima nyanya tangu mwaka wa 2014 na ukulima huu uko na manufaa mengi. Kwa mfano kwa ekari moja unaweza kutoa masanduku 400 na unapopeleka sokoni unaweza kupata hata Sh1 milioni. Hii ni faida kubwa sana kwa kila mkulima ambaye anataka kunawiri katika kilimo,” akasema.

 

Mkulima wa nyanya na sukumawiki Maina Karethi aonyesha baadhi ya nyanya ambazo alivuna katika shamba lake katika kijiji cha Ruiru-Solai, Nakuru. Picha/ Samuel Baya

Hata hivyo, alisema kuwa ukulima wa nyanya huwa na changamoto sana; hasa katika mtaji.

“Katika ekari yangu moja hii, nyanya zinachukua muda wa miezi miwili na nusu tokea siku ile inapopandwa. Hapo ndio tunapoanza kuvuna na tunavuna kila wiki na inaendelea kupanda kila unapovuna. Unaanza kwa kreti tano au sita na utafikia wakati unavuna na kujaza lori nzima aina ya kanta. Ni biashara inayolipa na yenye faida,” akasema.

Hata hivyo, alikiri kwamba kuna mdudu ambaye huvamia nyanya na kuziharibu sana hivi kwamba mara nyengine anawaharibia soko.

“Tumejaribu hata kumchanganyia madawa ili aweze kuepukana na nyanya lakini mdudu huyo anaendelea kuziharibu kila kukicha. Tumefanya bidii kumkabili lakini hataki kamwe na hili limekuwa mojawapo ya changamoto. Hata hivyo kilimo hiki kwa kweli kimenisaidia sana,” akasema.

Aliwataka vijana waachane na tamaa ya kutaka kazi za kuajiriwa wakati kuna fursa ya wao kujiendeleza na kunawiri katika maisha yao kupitia kwa shughuli za kilimo.

“Kwa mfano mimi nilipogundua kwamba akili yangu haikuwa kwa masomo, niliacha kusoma na nilikuwa katika kidato cha tatu. Lakini ninaweza kusema kwamba kwa sasa nimefaulu sana kupitia kwa kilimo hiki cha mboga huku Nakuru,” akasema.

 

You can share this post!

UJUZI NA MAARIFA: Mradi wa biogesi ulivyopunguza gharama ya...

AKILIMALI: Kilimomseto kinavyowafaa marafiki watatu

adminleo