Makala

Biashara ya mapambo yenye asili za Kiafrika yarejea miaka minne baada ya kusambaratishwa na Covid

Na SAMMY WAWERU November 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MIAKA minne baada ya taifa kukumbwa na janga la Covid-19 lililosababisha biashara nyingi kufungwa, Adele Dejak, kampuni inayounda bidhaa za mapambo zenye asili ya Kiafrika imefunguliwa tena.

Kampuni hiyo ilikuwa miongoni mwa thuluthi moja ya biashara ndogondogo na za kadri (MSMEs) zilizotatizwa na ugonjwa wa Covid, ambao miaka miwili na nusu baadaye, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza umedhibitiwa.

MSMEs inawakilisha asilimia 98 ya nguzo zinazosaidia ukuaji wa uchumi.

Baadhi ya mapambo ya Adele Dejak kwenye duka jipya la kampuni hiyo soko la Village Market, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Wakielezea kuridhishwa kwao na kufunguliwa tena kwa kampuni hiyo inayojikita kwenye uundaji wa bidhaa za sanaa kwa msingi wa fashioni ya kisasa na Kiafrika, wawakilishi wake wamesema wana imani mazingira ya sasa ya kibiashara yatasaidia Adele Dejak kurejea mahali ilipokuwa.

Julius Chilango, Msimamizi wa Mauzo alisema kampuni hiyo itatumia nguvu zake mpya kuafikia matakwa ya Wakenya kupata bidhaa endelevu zilizoundwa kwa fashioni ya kileo.

Kwenye mahojiano katika duka jipya la kampuni hiyo Village Market, Nairobi, afisa huyo alisema Adele Dejak inajituma kuweka paruwanja sanaa zenye asili ya Kiafrika kwa kutengeneza bidhaa zinazowakilisha mila, usanii na zenye mashiko.

Julius Chilango, Mkuu wa Mauzo Edele Dejak akionyesha baadhi ya bidhaa zinazouzwa na kampuni hiyo kwenye duka lake jipya eneo la Village Market, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Adele Dejak inajivunia kuuza bidhaa zilizoundwa kwa mikono, kama vile mkoba wa Kilamu unaoambwa kwa kutumia malighafi yaliyotupwa au yanayoonekana kutokuwa na thamani, ambao hutengenezwa kwa ushirikiano na wanawake waliobobea kisanaa na kiufundi kushona.

Mikoba hiyo huundwa kwa kutumia plastiki zilizotupwa, shughuli inayotekelezwa na wanawake kutoka Pwani ya Kenya wakiwa na lengo la kudumisha mila na utamaduni wa eneo hilo.

“Zinatengenezwa na mafundi wa Kenya kwa msingi wa mila na tamaduni za matabaka mbalimbali ya Kiafrika. Shabaha ni kunogesha brandi za tamaduni za Afrika,” Chilango akasema.

Mikoba maridadi inayouzwa na Adele Dejak. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, alisisitiza umuhimu wa Wakenya kukumbatia bidhaa zilizotengenezewa humu chini, katika kile alihoji hatua hiyo itasaidia kuangazia gapu ya ukosefu wa kazi na kupunguza hamu ya kuagiza vitu nje.

“Tunatafuta ajira na suluhu si kupeleka wafanyakazi nje ya nchi, ila ni kukuza na kuboresha kampuni tulizonazo kama taifa. Tukumbatie bidhaa zetu, na zikinunuliwa kwa wingi kero ya ukosefu wa ajira itaangaziwa pakubwa,” alielezea.

Kulingana na Florida Kanini, Msimamizi wa Uzalishaji, Adele Dejak inalenga kuinua na kupiga jeki wanawake kutoka Pwani ya Kenya kupitia utengenezaji bidhaa zenye asili ya Kiafrika na za fashioni ya kisasa.

Kampuni ya Adele Dejak huuza mapambo yenye asili za Kiafrika. PICHA|SAMMY WAWERU

Kanini alielezea imani yake kwamba hatua hiyo itasaidia kukabiliana na lindi la umaskini miongoni mwao.

“Tunapania kushirikisha wanawake wengi kupitia uundaji wa bidhaa, ambazo hazitaelezea hadithi yao kimaisha pekee, bali pia kukabiliana na umaskini na kuwapa mapato,” Kanini alisema.

Huku thamani ya Shilingi ya Kenya ikionekana kuendelea kuimarika, Adele Dejak ina matumaini miezi michache ijayo itaandikisha mapato na faida ya kuridhisha.

Mkoba ulioundwa na wanawake kutoka Pwani ya Kenya kwa kutumia malighafi ya plastiki na mengine yanayoonekana kutokuwa na thamani. PICHA|SAMMY WAWERU