BIDIIBUILD: Programu ya kurahisisha ufuatiliaji wa jinsi miradi ya ujenzi inavyoendelea
Na MAGDALENE WANJA
KUFUATILIA jinsi ujenzi wa nyumba unavyoendelea huwa kibarua kigumu wakati mradi uko katika sehemu ya mbali na alipo mmiliki.
Hii ni pamoja na changamoto ya kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati unaofaa.
Maswala haya yote yakizingatiwa, ni muhimu kuhakikisha kuwa unaweza kufuatilia kwa wakati mradi unapoendelea.
Ni kwa sababu hii ambapo vijana wabunifu wakiongozwa na Bw Kelvin Wachira, 28, kutoka nchi ya Kenya na Solomon Daboni, 30, wa Ghana wamebuni programu ya kurahisisha shughuli ya kufuatilia jinsi miradi inavyoendelea.
Wawili hao walikutana katika hafla ya MEST ambayo mada zilizojadiliwa ziliegemea zaidi katika kuwafunza vijana kutoka barani Afrika masuala ya uwekezaji.
Programu hiyo kwa jina BidiiBuild inawezesha kuwaleta pamoja mmiliki wa mradi, msimamizi na wajenzi katika mradi huo.
Tangu kuzinduliwa kwake mnamo Oktoba 2019 BidiiBuild imesimamia zaidi ya miradi 10 ya ujenzi ambayo tayari imekamilika.
Kampuni hiyo inajihusisha na miradi ya ujenzi kwa kiasi kikubwa nchini Kenya na Ghana huku wakiweka juhudi kupenya katika nchi zingine barani Afrika.
Kulingana na Daboni, programu hiyo inaweza kutumika kuokoa muda na fedha ambazo zingetumika vibaya wakati wa ujenzi.
“Ukiweza kuokoa muda wa dakika 10 kila siku kwa mradi ambao unafaa kuchukua miaka miwili kukamilika, unaweza kuokoa kati ya dola 8,000 na 10,000 hii ikiwa ni sawa na Sh800,000 na Sh1 milioni.