Makala

BURUDANI: DJ aeleza jinsi Covid-19 ilivyoyumbisha mikataba, ana imani Desemba na Januari hali itakuwa shwari

November 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DIANA MUTHEU

KABLA ya janga la corona kuikumba nchi yetu, kwa kawaida ungempata Susan Wanjiru, 34 maarufu kama VJ Shiroh akiwatumbuiza watu katika hafla mbalimbali.

Lakini kwa sasa, yote hayo ameamua kuyaweka kando na kuingilia biashara zingine mbadala kujitafutia riziki, baada ya janga la corona kuharibu kazi yake ambayo amekuwa akiifanya kwa miaka mingi.

VJ Shiroh ni mmoja wa madijei tajika wa kike mjini Mombasa na katika mazungumzo na Taifa Leo Dijitali, anasema kuwa alianza safari yake mwaka wa 2012.

“Ilianza kama mchezo pale ambapo nilimtembelea rafiki yangu aliyekuwa akiwatumbuiza watu katika klabu moja mjini Nakuru. Nilimwelezea kuwa ningependelea anifunze kudijei, na baada ya kujipiga msasa kwa miezi miwili unusu, tayari niliajiriwa kazi pia katika klabu hiyo hiyo,” akasema VJ Shiroh.

Katika fani hiyo ya udijei, VJ Shiroh anasema kuwa amefanya kazi katika kaunti za Nakuru, Kakamega, Uasin Gishu, Mombasa, Kilifi, Kwale na Nairobi.

“Miaka hiyo ya nyuma, watu wengi walinishabikia sana manake ilikuwa nadra sana kumpata mwanamke ambaye ni dijei, na hiyo ilinipa motisha wa kuendelea na kazi hiyo,” akasema dijei huyo ambaye ni mama wa watoto wawili.

VJ Shiroh anaelezea kuwa hakupata taabu kuwa dijei kwani alipomwelezea mama yake wazo la kufanya kazi hiyo, alimkubalia.

“Zaidi, mume wangu alielewa kuwa DJ ni kazi na akanikubalia niifanye. Kama mama, huwa natumia muda mwingi mchana kukaa na watoto wangu, kisha jioni wanabakia na mjakazi kwa saa chache kabla nirejee nyumbani,” akasema huku akiongeza kuwa udijei ni kazi ambayo inalipa vizuri.

“Nimeifanya kazi hii kwa miaka minane, na nimevuna matunda yake,” akasema VJ Shiroh akiongeza kuwa katika fani ya udijei, walio na jina ndio hupata kazi kwa urahisi na pesa kwa wingi pia.

Susan Wanjiru, 34, maarufu VJ Shiroh. Picha/ Hisani

Kulingana na VJ Shiroh, kuwa DJ si lazima ucheze muziki katika kilabu peke yake.

“Nimefanya kazi katika harusi, sherehe za kuzaliwa, sherehe za wanandoa kukumbuka ni miaka mingapi wamekuweko katika ndoa, vilabu mbalimbali na sherehe zozote zile zinazohitaji muziki,” akasema huku akieleza kuwa siri kubwa ni kuwa na uwepo na umaarufu katika mitandao tofauti ya kijamii.

Licha ya dijei huyu kuimwagia sifa fani hii ya kazi, anasema pia ina changamoto zake. Anataja changamoto hizi kuwa nyingi pale ambapo DJ ni mwanamke.

“Kuna baadhi ya watu ambao huagiza kuwa na uhusiano wa kimapenzi kabla ya kumpa dijei wa kike kazi. Pia, baadhi ya waajiri huwa hawalipi pesa kwa muda ufaao ilimradi uwafuatilie kwa muda mrefu,” akasema huku akiongeza kuwa ameyapitia hayo yote lakini ameweza kuepuka mitego hiyo kwa kubakia na msimamo wa kuulinda utu wake na hadhi yake kazini na kuhakikisha kuwa wanaweka saini mkataba kabla ya kuanza kazi yoyote ile.

Zaidi, anasema kuwa janga la corona limeiathiri kazi yake pakubwa, jambo ambalo limesababisha afanye maamuzi ya kuiweka kazi hiyo pembeni, na kuingilia biashara zingine.

“Licha ya kuifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 12 sasa, janga la corona limeathiri kazi yetu sana. Tangu vilabu vifungwe na saa za kafyu kuanza mapema, hatuwezi kufanya kazi kwa muda mrefu. Zaidi, mikutano mingi imepigwa marufuku na hivyo kazi zetu haziwezi kurejea hali ya kawaida kwa sasa,” akasema VJ Shiroh.

Anaongeza kuwa sherehe nyingi na mikataba ambayo alikuwa ameweka saini kutumbuiza mwaka huu zilisitishwa.

Hata hivyo, ana matumaini ya kuwa msimu wa sherehe za Krismasi Desemba 2020 na shamrashamra za Mwaka Mpya ataweza kupata kazi kadhaa.

“Kwa kila jambo unalopenda kufanya, ni lazima uwe na matumaini. Lang utu ni kuomba kuwa janga hili litaisha, ili maisha yetu yarejee hali ya kawaida,” akasema.